Home news HIVI NDIVYO MORRISON ALIVYOZIGEUZA SIMBA NA YANGA KUWA KITEGA UCHUMI CHAKE..AKOMBA NUSU...

HIVI NDIVYO MORRISON ALIVYOZIGEUZA SIMBA NA YANGA KUWA KITEGA UCHUMI CHAKE..AKOMBA NUSU BILIONI KILAIINI…


BERNARD Morrison kwa sasa amesimamishwa na Simba kwa kosa la utovu wa nidhamu huku ikidaiwa watani wao wa jadi, Yanga wako katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa kumrejesha nyota huyo wa Ghana kundini.

Inatajwa kuwa mabosi wa Jangwani wamemuandalia Morrison dau nono la Dola 10000 (Sh 231 milioni) na mshahara ha Dola 6,000 (Sh 13.8 milioni) kwa mwezi ili wamshawishi asaini mkataba wa kuitumikia tena Yanga baada ya kuachana nayo mwaka 2020 na kujiunga na watani wao Simba katika uhamisho ambao ulikuwa na utata mkubwa.

Uhamisho huo wa Morrison kwenda Yanga ikiwa utakamilika utakuwa ni muendelezo wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29 kuvuna kirahisi fedha kwa klabu hizo mbili kubwa nchini baada ya kufanya hivyo katika kipindi cha miaka miwili aliyokuwepo nchini.

MAMILIONI BILA JASHO

Katika kipindi cha miaka miwili ambayo Morrison amekuwepo hapa nchini amevuna kiasi kikubwa cha fedha huku akiwa hajazitumikia vya kutosha timu hizo mbili kulinganisha na baadhi ya wachezaji ambao wanalipwa kiasi kiduchu cha fedha.

Pamoja na kupata mamilioni ya usajili na mishahara, mchezaji huyo hajazitumikia timu hizo kwenye michezo mingi kwa nyakati tofauti ikiwemo ile muhimu na hata mingi aliyocheza hakuonyesha kiango bora na kutoa mchango mkubwa.

Fedha za usajili tu ambazo Morrison amevuna kutoka kwa Simba na Yanga ndani ya miaka miwili ni kiasi cha takribani Dola 160,000 (Sh370 milioni) huku akizichezea jumla ya mechi 54 kati ya 95 ambazo alipaswa kuzichezea katika kipindi hicho.

BAO MOJA MIL 20 YANGA

Katika miezi sita ambayo Morrison aliichezea Yanga kabla hajajiunga na Simba, mchezaji huyo alicheza michezo 16 tu ya mashindano mbalimbali huku akikosa jumla ya mechi 11.

Ndani ya mechi hizo 16 alizoichezea Yanga, ‘Mzee wa Kuwakera’ alihusika na mabao tisa tu akifunga manne na kupiga pasi tano za mwisho.

Dau lake la kujiunga na Yanga kwa mkataba wa miezi sita lilikuwa ni Dola 60,000 (Sh139 milioni) na kwa mwezi mshahara wake ulikuwa ni Dola 3,000 (Sh6.9 milioni).

Ukijumlisha mishahara ya miezi sita na dau la usajili, kwa ujumla Morrison alichuma kiasi cha Dola 78,000 (Sh 180 milioni) ambazo ukigawa kwa idadi ya mabao tisa aliyohusika nayo, sio dhambi ukihitimisha kwa kusema Yanga ilimlipa Morrison kiasi cha Sh 20 milioni kwa kila bao alilohusika nalo kipindi hicho wakati anaichezea.

BAO MOJA MIL 35 SIMBA

Simba ndio inaonekana imekombwa fedha nyingi na Bernard Morrison kwani katika kipindi cha miezi 19 aliyoichezea tangu alipojiunga akitokea Yanga, amelipwa kiasi cha Dola 195,000 (Sh 451 milioni) ambacho ni makusanyo ya mshahara na dau la usajili.

SOMA NA HII  TAKWIMU ZINAONGEA...HIVI NDIVYO YANGA WANAVYOIBURUZA SIMBA MSIMU HUU...

Morrison alisajiliwa na Simba kwa Dau la Dola 100,000 (Sh 231 milioni) huku akilipwa mshahara wa Dola 5,000 (Sh 11.6 milioni) kwa mwezi ambapo kwa miezi 19 aliyoichezea, amevuna kiasi cha Dola 95,000 (Sh 219.8 milioni).

Katika kipindi hicho ndani ya Simba hadi sasa, Morrison amecheza jumla ya mechi 38 tu huku akikosa jumla ya michezo 30.

Kwenye michezo 38 alizoichezea Simba, Morrison amehusika na mabao 13 ambapo amefunga mabao saba na kupiga pasi za mwisho sita.

Jumla ya fedha kiasi cha takribani Sh451 milioni ambazo Morrison amekusanya kutoka Simba kupitia mishahara kwa muda aliosajiliwa hadi sasa pamoja dau la usajili ukigawa kwa mabao 13 ambayo amehusika nayo ndani ya timu hiyo, ni sawa kusema kuwa Simba imemlipa Morrison kiasi cha Sh 35 milioni kwa kila bao ambalo amehusika nalo.

AKOMBA NUSU BILIONI

Kiujumla fedha ambazo Morrison amezipata kutoka Simba na Yanga kwa mishahara pamoja na fungu la usajili ndani ya miaka miwili ni takribani Sh631 milioni.

Ukigawa fedha hizo kwa miezi 24, unapata jawabu kwamba katika kila mwezi, Simba na Yanga kwa pamoja zimemlipa Morrison kiasi cha Sh29 milioni, sawa na takribani Sh8 milioni kwa siku na takribani Sh333,000 kwa saa.

Mchezaji wa zamani Simba, Boniface Pawasa anasema Morrison ni mchezaji anaangalia zaidi maslahi yake na huenda hili linaloendelea na klabu yake inawezekana ni kushindwa kuendana na matakwa katika mkataba wake.

Pawasa anasema mkataba wa Morrison unaelekea mwisho kwa mfano wachezaji kama Mario Baloteli walikuwa watukutu lakini michango yao uwanjani ilikuwa inaonekana.

“Muda mwingine inahitajika busara zaidi kuishi na mchezaji wa aina yake kutokana na kipaji alichokuwa nacho uwanjani ila muda mwingine anapofanya makosa zaidi haina jinsi kuachana nae,” anasema Pawasa na kuongeza:

“Morrison kuna muda kama anakuwa na homa za vipindi wakati mwingine anatulia na kuna baadhi ya mechi moja mbili anacheza vizuri baada ya hapo anapotea moja kwa moja kama hayupo vile na michezo mingine hucheza kawaida tu.”

Mchezaji wa zamani Yanga, Simba na Azam, Ivo Mapunda anasema kwa hadhi ya mchezaji wa aina yake ni kama asiyeweza kujitambua kwa sababu wapo wachezaji wenye viwango vya kawaida lakini nidhamu zinawabeba.

“Nilitegemea aina ya wachezaji kama Morrison kuwa mfano kwa wengine kwanza wa kigeni, amesajiliwa kwa pesa nyingine lakini amekuwa akifanya mambo ambayo hayana ulazima nje na ndani ya uwanja,” anasema Mapunda

“Nidhamu aliyonayo inamfanya kuonekana mchezaji wa kawaida wakati kama angekuwa anajitambua ni mwenye kipaji kikubwa na mambo anayofanya si aina ya wachezaji ambao wanaotakiwa kuwa timu yoyote nchini.”

CREDIT: Mwanaspoti