Home news KWA MARA NYINGINE TENA…SIMBA WAZIDI KUNG’ARA AFRIKA KUPITIA MANULA…ISHU NZIMA IKO HIVI…

KWA MARA NYINGINE TENA…SIMBA WAZIDI KUNG’ARA AFRIKA KUPITIA MANULA…ISHU NZIMA IKO HIVI…


KIPA Aishi Manula ameweka rekodi ya kibabe katika mechi mbili za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na bila shaka itawapa Simba hali ya kujiamini katika mchezo ujao utakaopigwa Morocco Jumapili hii dhidi ya RS Berkane ya huko.

Licha ya uwepo wa makipa wenye majina makubwa wanaochezea timu maarufu katika michuano hiyo kuliko Simba, Manula hadi sasa ndiye kinara wa kuokoa hatari nyingi langoni mwake kuliko yeyote katika raundi mbili za makundi hayo.

Kwa mujibu wa mtandao wa www.fotmob.com, Manula katika mechi mbili alizoichezea Simba dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast na US Gendarmerie ya Niger, ameongoza kwa kuwa na wastani wa kuokoa hatari nyingi ambazo kwa wastani ni hatari 5.5 kwa kila mechi.

Kiujumla katika mechi mbili, Aishi Manula ameokoa hatari 11 akimuacha anayemfuata kipa wa RS Berkane, Hamza Hamian Akbi mwenye wastani wa kuokoa mashuti 5 kwa mchezo huku kiujumla akiwa ameokoa mashuti matano.

Nafasi ya tatu inashikiliwa na kipa CS Sfaxien ya Tunisia ambaye ameokoa jumla ya hatari sita huku akiwa na wastani wa kuokoa hatari 3 kwa mechi.

Mechi dhidi ya Gendarmerie Nationale ugenini Jumapili iliyopita ambayo Simba ilipata sare ya bao 1-1 ndio imembeba zaidi Aishi Manula kwani katika mchezo huo aliokoa jumla ya hatari nane na kuisaidia timu yake kupata pointi moja muhimu huku hatari nyingine tatu akiziokoa katika mechi dhidi ya Asec Mimosas.

Lakini hakuishia kuokoa hatari nyingi tu kwenye mechi hiyo ya Gendarmerie bali pia Manula alishika nafasi ya tatu kwa makipa waliopiga pasi nyingi sahihi ambapo alipiga jumla ya pasi 21 zilizofikia walengwa kwa usahihi kati ya pasi 29 alizoelekeza kwa wenzake ikiwa sawa na 72%.

Katika viwango vya ubora kwa mchezaji mmoja mmoja katika raundi ya pili ya hatua ya makundi ya Shirikisho, Manula ameshika nafasi ya tatu katika orodha ya makipa waliofanya vizuri akipata alama 6.8 chini ya 10, nyuma ya kipa wa Al Masry, Ahmed Massoud aliyepata 7.8, huku nafasi ya pili akienda kwa kipa wa Pyramids FC, Sherif Ekramy, aliyepata 7.3.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMATATU

Mafanikio hayo ambayo Manula ameanza nayo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ni kama muendelezo wa kung’aa kwa nyota yake katika miaka ya hivi karibuni ndani na nje ya nchi.

Kipa huyo hadi sasa ndiye anaongoza kwa kucheza idadi kubwa ya mechi za ndani bila kuruhusu bao katika misimu mitano mfululizo iliyopita ambayo minne kati ya hiyo mitano alishinda tuzo ya kipa bora na mara moja hakukuwa na zawadi kwa washindi.

Manula aliyejiunga na Simba mwaka 2017, ameshinda mataji manne ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports, taji la Ngao ya Jamii mara tatu taji moja la Kombe la Mapinduzi na kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili tofauti.

Akizungumzia kiwango bora anachokionyesha, Manula alisema ni matokeo ya kujituma, ushirikiano na mbinu bora za benchi la ufundi.