Home news PAMOJA NA KUONA SIMBA IKIMCHAPA MTU GOLI 6-0…PRISONS WADAI WATAIFANYA ‘KITU MBAYA’...

PAMOJA NA KUONA SIMBA IKIMCHAPA MTU GOLI 6-0…PRISONS WADAI WATAIFANYA ‘KITU MBAYA’ LEO…

 


KOCHA Mkuu wa Tanzania Prisons, Patrick Odhiambo amesema vipigo walivyopata katika mechi mbili mfululizo vinatosha na sasa shughuli inahamia dhidi ya Simba kuhakikisha wanafanya kweli, huku akiwataka matraika wake kubadilika.

Odhiambo alitua kwa ‘Wajelajela’ hao hivi karibuni akichukua mikoba ya Salum Mayanga aliyejiunga na Mtibwa Sugar na katika mechi mbili alizosimamia zote amekumbana na vichapo huku wakifungwa jumla ya mabao 6-0.

Timu hiyo inatarajia kuwa kibaruani kuwakabili Wekundu wa Msimbazi, leo kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam ukiwa wa raundi ya 14 kwa timu hizo.

Hata hivyo, timu hizo zinakutana huku kila upande ukiuguza majeraha ya kupoteza mechi iliyopita, baada ya Simba kulala 1-0 dhidi ya Kagera Sugar huku Prisons wakila kisago cha mabao 4-0 mbele ya Azam.

Odhiambo amesema kuwa matokeo waliyopata katika mechi mbili nyumbani hayakuwa mazuri, hivyo mchezo ujao na Simba lazima kieleleweke.

Alisema makosa yaliyofanywa na vijana wake haswa sehemu ya kipa na ushambuliaji ameifanyia kazi huku akiwataka washambuliaji kuwa makini katika kumalizia mipira ya mwisho.

“Siyo matokeo mazuri, lakini nimeona wapi tuliteleza na nimefanyia kazi tangu mechi na Azam, kwa sasa tunajipanga kumalizia hasira kwa Simba, naamini tutarejesha furaha kwa mashabiki,” alisema Odhiambo.

Straika na kinara wa mabao kikosini humo, Jeremia Juma alisema licha ya kwamba mchezo huo utakuwa mgumu, lakini lolote linaweza kutokea.

“Tumepoteza mechi mbili lakini si kwamba hatuwezi kushinda mchezo unaofuata, dhidi ya Simba, tunafahamu ugumu wake ila lolote linawezekana na hii ni ligi, tunaenda kwa umakini na tahadhari,” alisema Juma.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUTOA KAFARA YA NG'OMBE ...MISRI WACHEZESHWA 'NDOMBOLO' NA CONGO...

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here