Home Makala SENZO AVUNJA UKIMYA ISHU YA MABADILIKO YANGA…AFUNGUKA THAMANI HALISI YA YANGA..HAJI AJA...

SENZO AVUNJA UKIMYA ISHU YA MABADILIKO YANGA…AFUNGUKA THAMANI HALISI YA YANGA..HAJI AJA NA HILI..


Senzo Mazingisa, mtendaji mkuu wa Yanga anasema kwa ukubwa wa timu kama Yanga hauwezi ukaanza msimu wakiwa hawana malengo ya kumaliza nayo wakina na taji lolote.

Katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwanaspoti, Senzo anasema baada ya kupoteza Kombe la Mapinduzi wamejiwekea lengo kuchukua Ligi Kuu Bara na lile la Shirikisho la Azam huku wakiweka mkazo katika kila mechi.

“Mapinduzi ilishapita na sasa tunaendelea kusonga mbele zaidi. Tunafanya kazi kubwa sio tu kwa wachezaji, bali kila mtu katika timu hii na lengo likiwa ni kuchukua mataji,” anasema.

Akizungumzia usajili anasema waliufanya kwa umakini wakihakikisha wachezaji wanaisaidia Yanga kutimiza malengo iliyonayo.

ISHU YA MABADILIKO

Senzo anasema wapo kwenye hatua nzuri kuhusu mabadiliko ya uendeshaji wa klabu baada ya kuruhusiwa na mamlaka husika juu ya katiba mpya.

“Yanga haipo tu kwa BMT bali ipo pia kwa TFF na baada ya katiba yetu kukamilika tuliipeleka kwao na wao wametupa sisi miezi sita na wametuambia kila kitu kilichopo kwenye katiba kikamilike ndani ya miezi hiyo.” Senzo anasema jambo la kubwa ni mashabiki wa timu hiyo kubadilika na kuwa wanachama na hawana muda wa kupoteza kwani tayari mchakato huo unaendelea vizuri.

“Tumeanza kusajili wanachama wetu na namba zinaenda vizuri. Mpaka sasa tunaona mabadiliko yanaenda vizuri na kutakuwa na mabadiliko ya kimuundo kwenye uongozi wa Yanga na lengo likiwa ni kupata muundo wa timu,” anasema.

THAMANI YA KLABU

Senzo anasema baada ya kukamilika kwa usajili wa wanachama watageukia upande wa thamani halisi ya klabu ili wawekezaji wapate picha kamili ya Yanga kabla ya kuweka pesa zao.

“Tutaweka thamani halisi ya Yanga na tutaita watu ambao watakuja kutusaidia kwenye kuweka sawa. Katika mchakato huu moja kwa moja kutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye upande wa uongozi.”

Senzo anasema hakutakuwa na mwenyekiti wala makamu tena, badala yake kutakuwa na rais wa timu na hakutakuwa na cheo hicho bila kuwapo kwa uchaguzi huru ndani ya klabu.

“Kupitia matawi tutakuwa na viongozi wa matawi ambao watatoka kwa ajili ya kwenda kwenye uchaguzi huu na hili linatakiwa lifanyike ndani ya miezi sita kuanzia sasa. Jambo la kushukuru ni mabadiliko yanaendelea vizuri na lengo kuifanya timu kuwa kwenye levo nyingine,” anasema Senzo.

“Hauwezi kuwa mwanachama wa timu kama haupo kwenye tawi. Ukiwa nje ya nchi unatakiwa kuhakikisha unajisajili kwenye tawi na ukiwa huko utapokea meseji ambayo inakupa taarifa na hii imetokana na kuwekeza kwenye upande wa dijitali.”

Mtendaji huyo anafunguka zaidi na kusema mambo yote ya mabadiliko yatazidi kwenda vizuri kupitia matokeo ya uwanjani yakiwa mazuri kwa sababu vitu hivyo vinakwenda pamoja.

MFIKIRWA AWEKA SAWA

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala Yanga, Haji Mfikirwa ambaye aliyeambatana na Senzo katika mahojiano haya anasema muundo wa kidijitali kwa wanachama ni mzuri kwa sababu unasaidia kujua wana wanachama wangapi tofauti na ilivyo sasa.

“Hata huko nyuma klabu ilikuwa na wanachama lakini mfumo huu unakuja kuipa faida kwa kujua tuna wanachama kiasi gani wakati wowote. Kwenye mabadiliko yetu kuna kipengele cha uhusiano mzuri na wanachama,” anasema Mfikirwa.

“Kipindi cha nyuma tukiwa na La Liga (Ligi Kuu ya Hispania) na klabu ya Sevila tuliulizwa tuna wanachama kiasi gani, lakini hatukuwa na jibu kamili. Kila mtu alikuwa na jibu lake, sasa kitendo tunachofanya ni kuwa na kumbukumbu ya wanachama ambao wataweka kila kitu chao kwenye fomu.”

Mfikirwa anasema faida ambayo wanachama wataipata ni kununua bidhaa zao moja kwa moja kutoka Yanga kwa sababu rekodi zao zitakuwapo.

“Matawi zaidi ya 500 yamejisajili mpaka sasa na kwenye kila tawi kunatakiwa kuwe na wanachama 100 na kwa upande wa juu ni wanachama 500. Mwitikio ni mkubwa na tunafanya hili kwa nguvu kubwa na mwisho wa siku tuje kupata viongozi,” anasema.

“Katiba inasema sio wanachama wote wanakuja kwenye uchaguzi, lakini kupitia matawi wao ndio watachagua watu wa kwenda katika uchaguzi mkubwa na mwezi wa saba tunatakiwa tuwe na viongozi wapya kwa mujibu wa katiba.”

BILA ADA INAKULA KWAKO

Zamani ilikuwa ni kawaida kwa mwanachama wa Yanga kutolipia kadi yake mpaka muda wa uchaguzi mkuu ndio wengi hulipa, lakini kupitia mabadiliko suala hilo limeondolewa.

Mfikirwa anasema katiba mpya inasema mwanachama hai ni yule ambaye analipia kadi na kupitia matawi ndio itasaidia kujua uhai wa wanachama.

“Haya matawi tunataka yawe hai muda wote. Tunataka kuona uhai wa mwanachama na usipolipa ada kwa muda wa miezi sita sifa yako inaondoka. Fomu ya mwanachama kujaza gharama yake ni Sh2,000 na pesa hiyo inabaki katika tawi ili kusaidia hapohapo,” anasema Mfikirwa. ”Wanachama ambao wapo kwenye matawi watakuwa na bei punguzo ya kununua vitu halisi kutoka Yanga kwa sababu watakuwa wanapata moja kwa moja kutoka kwenye klabu. Hii itakuwa rahisi kupitia matawi kwa sababu tutakuwa tunawasiliana.”

SOMA NA HII  IMEFICHUKAA..HII NI ZAIDI YA KUFURU...SIMBA KUMLIPA ZAIDI YA BILIONI 1 KOCHA MPYA..MLOLONGO UKO HIVI..

Upande wake Senzo anasema kitendo cha kuweka rekodi ya wanachama ni sehemu ya Yanga kupata pesa kwa sababu hata wakienda kwa wafadhili wakitaja wingi wa wanachama watawapata wengi na thamani halisi ya klabu itajulikana.

“Kama Haji alivyosema wanachama watakuwa hawapati tena jezi feki kwa sababu watakuwa wanaweka oda ya mapema kwenye jezi moja kwa moja Yanga na hii itasaidia kupata pesa,” anasema.

CHANGAMOTO

Mfikirwa anasema changamoto ambayo timu nyingi za Tanzania zinakutana nazo ni kutomiliki viwanja na hiyo inawanyima uhuru wa kufanya mambo mengi kwani duniani kwenda uwanjani ni kama vile unatoka ‘out’ na familia yako.

“Kama vile ambavyo tunafanya Siku ya Wananchi ilitakiwa iwe kila siku kwenye mechi watu waje na familia zao kufurahia timu yao, lakini haijatukatisha tamaa tuna imani kubwa kupitia hii kujua wanachama wetu tutafanikiwa,” anasema.

Anasema wana mawazo mengi mazuri na kwa kuanzia kwenye kusajili wanachama kutafungua mipango mingi mizuri ambayo mwanzoni ilishindwa kutimia.

“Miradi inakuwa ngumu kufanyika mara nyingi ukiwa hauna namba ya wanachama, lakini kwa sasa tuna imani kubwa tutafanikiwa kwa sababu tuna watu ambao wana mapenzi makubwa na klabu yao.”

KAUNDA NA KIGAMBONI

Yanga ilianzisha miradi ya ujenzi viwanja viwili eneo la Kaunda na Kigamboni, lakini imeonekana kutokuwa na mwendelezo kama ambavyo ilitambulishwa awali.

Mfikirwa anasema miradi hiyo ilikuwa ngumu kufanyika kutokana na kutokuwa na kumbukumbu halisi ya wanachama wake kiasi cha kuwafanya washindwe kupata pesa za mikopo.

“Bila fedha utabaki kuwa na ndoto huku hujui lini utaikamilisha. Tuna miradi mingi na yote inahitaji fedha. Huwezi kwenda kwenye benki halafu ukasema una mashabiki ukiwa unataka mkopo hivyo ni ngumu kufanyika. Tulijaribu kwa siku nyuma kutembeza bakuli, lakini hatukufanikiwa kwa kiwango kikubwa na ndio maana tumekuja na mfumo mpya,” anasema Mfikirwa.

“Tunaona mwanga mzuri mbele tunapoenda na imani yetu tutakuwa miongoni mwa timu kubwa barani Afrika.”

ZAHERA ATAJWA

Uongozi wa Yanga umemrejesha aliyekuwa kocha wao, Mwinyi Zahera, lakini alirejea kama mkurugenzi wa ufundi na maendeleo ya soka la vijana katika timu hiyo.

Senzo anasema lengo kubwa la uwepo wa Zahera ni kuwa na muundo mzuri wa ukuaji wa wachezaji kuanzia katika upande wa soka la vijana kwenye ngazi za chini za miaka 15, 17 na 20.

“Lazima uwe na mipango ya ukuaji wa vijana kwenye timu. Kwenye miaka minne nyuma hatukuwa bora katika hilo na ndio maana tumeweka nguvu huko na kupitia wafadhili wetu wametusaidia katika hilo,” anasema.

Senzo anasema nguvu nyingine ipo kwenye upande wa timu ya wakubwa kuhakikisha inafanya vizuri kisha ndipo wanageukia katika upande mwingine.

“Hatujaisahau timu ya wanawake lakini lazima uwe na mpangilio kwenye uendeshaji. Ndio maana tumeanzia huku na kila kitu kikisimama tutageukia huko na hautakiwi kumaliza tatizo kwa malengo mafupi bali kutumia malengo marefu,” anasema Senzo.

Hata hivyo, Mfikirwa anakazia akisema: “Kuna muda tulikuwa na wachezaji lakini baada ya miaka miwili wanaondoka na ndio maana tumekuja na mpango mwingine. Hauwezi kuwa na timu kila siku mpya ni ngumu mno kuendeleza utamaduni wetu na ndio maana kwenye usajili wapo wachezaji wa kucheza sasa na wengine kwa ajili ya miaka ijayo ili wazoee tamaduni zetu na ndio maana tunataka kutoka kwenye usajili wa muda mfupi.”

SUBIRA KWA MASHABIKI

Mfikirwa anasema mambo mazuri hayataki haraka, hivyo mashabiki wawe na subira wakati viongozi wanapambana kuitengeneza timu iwe na muundo mzuri na kupata matokeo bora.

“Waswahili wanasema ukiona vinaelea ujue vimeundwa na kwenye miradi hii kuna siku tutashuka na siku tutapanda kama barabara ndefu itakuwa na kona na milima,” anasema.

“(Wanachama) waendelee kuisapoti timu na viongozi. Tumekaa muda mrefu bila mataji lakini tukiwa pamoja na kila mtu akitimiza wajibu wake tutafikia malengo yetu.”

Senzo anatia msisitizo akisema, “kitu kikubwa ni kupata ushindi na pointi tatu. Nawaomba mashabiki waisapoti timu kwa kuja viwanjani na kuwapa nguvu wachezaji, unajua hata wachezaji wataona wanasapotiwa vizuri. Wakati huohuo waendelee kujisajili.”