Home Habari za michezo EDO KUMWEMBE – SIMBA WAKIDHARAU IMEKULA KWAO…MANULA ANAPENDA KULALAMIKA SANA…

EDO KUMWEMBE – SIMBA WAKIDHARAU IMEKULA KWAO…MANULA ANAPENDA KULALAMIKA SANA…


TUANZE na wapi? kuhusu Aishi Manula au namna ambavyo kundi la Simba limekaa baada ya Wekundu wa Msimbazi kuambulia kichapo cha mabao 3-0 pale Benin kutoka kwa wababe wa soka la Ivory Coast, Asec Mimosas. 

Tuanze katika kundi lenyewe halafu tuje kwa Aishi. Utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kwamba hali bado ni nzuri kwa Simba. Wanahitajika kushinda katika pambano lao la mwisho dhidi ya US Gendermarie kisha watapita kwenda robo fainali.

Hofu yangu ilikuwa kama Berkane wangeshinda katika pambano dhidi ya Gendermarie. Hii ina maana kwamba wangefikisha pointi tisa. Ina maana hata kama Simba wangeshinda pambano la mwisho, basi wangetimiza pointi 10. Hapa nadhani katika pambano la mwisho kati ya Berkane na Asec basi wangeweza kuamua kufanya uhuni na kutoka sare tu. 

Timu zote tatu Simba, Berkane na ASEC zingekuwa na pointi 10 na Simba ingeondolewa katika michuano. Michuano hii kitu kinachoangaliwa cha kwanza ni matokeo yetu kati ya mimi na wewe. Kama wangeangalia hivi Simba hawapo vizuri kwa Asec wala Berkane. Mechi ya Berkane wamepigwa 3-0 ugenini wakati wao walishinda 3-1 pale Temeke.

Mechi dhidi ya Berkane walipigwa 2-0 pale Morocco halafu wao wakashinda 1-0 pale Temeke. Na sasa ni wazi kwamba Gendermarie wameifanyia kazi nzuri Simba. Ushindi wowote utaipitisha Simba bila ya kujali kile ambacho kitatokea pambano la Berkane dhidi ya Asec.

Hata hivyo, Simba inabidi wawe makini. Gendermarie wanaonekana kuwa bora katika ufungaji hasa kwa kupitia kwa mshambuliaji wao anayeitwa Adebayor. Inawezekana yeye ndiye ambaye anaweza kuamua mechi Uwanja wa Mkapa. 

Akibanwa vyema basi Simba itapita. Asipobanwa vyema tunaweza kuwa na msiba mwingine kama ilivyotokea katika mechi dhidi ya UD Songo au Jwaneng Galaxy ya Botswana. Mara nyingi tuna kumbukumbu nyingi nzuri za Simba dhidi ya wakubwa kama Al Ahly, AS Vita, JS Saoura na wengineo katika Uwanja wa Mkapa. Hata hivyo, huwa tunaamua kusahau kumbukumbu hizi mbaya ambazo zaidi zilikuwa mechi za kufa na kupona kwa Simba.

Tuchague kumbukumbu hizi mbaya kwa ajili ya kuwakumbusha Simba kazi ambayo inawakabili mbele yao. Hawa wote wawili walionekana kuwa vibonde kwa Simba na kama vile wangekufa nyingi Uwanja wa Mkapa, lakini hadithi ikawa tofauti. 

Turudi katika pambano la juzi na tumkumbuke Aishi Manula. Simba walichapwa mabao matatu halali na bado Aishi alikuwa mchezaji bora wa mechi. Aliokoa penalti mbili halafu akaokoa michomo ya kutosha tu. Asec wangeweza kushinda hata 7-0 kama Aishi asingekuwa makini.

Kinachotokea ni kwamba Aishi analipa uwekezaji wetu kwa umakini mkubwa. Umri wake umesogea kidogo na ndio wakati ambapo anatakiwa kuwa bora zaidi. Hii ni kawaida kwa makipa. Wote tunafahamu kwamba kadri umri unavyosonga mbele ndivyo wanavyokuwa bora. 

Tumefanya uwekezaji kwa Aishi kwa sababu naamini mpaka sasa atakuwa amecheza mechi zaidi ya 50 za kimataifa akiwa na Simba na timu za taifa za vijana na kisha timu ya wakubwa ya taifa, Taifa Stars. Kwanini awe mbovu nyakati hizi? Isingekuwa sawa.

SOMA NA HII  CEO WA SIMBA ATUSAIDIE...HIZO LOGO MBILI ZA MO XTRA NI ZA NINI KWENYE JEZI..?

Simba imempa mechi nyingi za kimataifa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na alipaswa kuimarika zaidi na kuonyesha kiwango bora zaidi. Na ndicho ambacho bahati nzuri amekuwa akifanya kwa sasa na juzi tena katika milingoti ya uwanja ule wa Benin alifanya vilevile.

Aishi pia amekuwa hawezi kukosekana katika mlango wa Taifa Stars. Kuna wakati Juma Kaseja alirudi akasimama, lakini bado Aishi amerudi tena. Hii ina maana kwamba Aishi amekuwa Tanzania One lakini pia amekuwa kipa tegemeo wa Simba.

Hakuna kipa wa Tanzania aliyecheza mechi nyingi za kimataifa zaidi ya Aishi. Unategemea aimarike zaidi. Kama angekuwa anao-nyesha udhaifu mwingi nadhani angestahili kulaumiwa na kupondwa kwa sababu kucheza mechi hizi nyingi ni kama vile Simba na Taifa Stars wamefanya uwekezaji kwake. Simba wangeweza kuamua kutafuta kipa wa kigeni katika nafasi yake, lakini waliamua kumuamini na kisha nafasi hiyo ya kipa wa kigeni wakaipeleka kwa mchezaji wa ndani. Ni Jambo jema kwa sababu ungekuwauamuzi wao binafsi na hapana shaka Aishi asingeimarika.

Ndani ya mechi hizi za kimataifa Aishi amekuwa akishambuliwa vilivyo. Amekutana na mikikimikiki mingi ambayo pengine imemuacha akiwa bora zaidi. Inawezekana kuna makipa wengi wana vipaji zaidi yake hapa nchini, lakini kwa sasa Aishi amewaacha mbali kutokana na mikikimikiki ambayo amekuwa akikutana nayo kila kukicha. 

Kitu kimoja kikubwa ambacho Aishi anapaswa kuimarika langoni ni kupiga kelele na kuwapanga wachezaji wake vyema. Mara nyingi Aishi huwa analalamika sana baada ya wenzake kukosea, lakini huwa hawapangi wenzake mapema kabla ya tatizo kutokea. Aishi sio mkali wakati timu yake haina mpira. Hapigi kelele wala haipangi timu yake vyema. Makipa wengi wazuri huwa wananusa hatari mapema kabla ya tukio halijatokea. 

Aishi anaweza kujifunza kwa Juma Kaseja ambaye amekuwa hodari wa kunusa hatari wakati timu yake haina mpira. Katika mabao matatu ambayo amefungwa juzi hakuna bao ambalo unaweza kumlaumu, lakini wakati mwingine wachezaji huwa hawajioni. Kama angeweza kuipanga vyema safu yake ya ulinzi si ajabu wenzake wangeweza kuokoa hatari kabla mpira haujamfikia.

Vinginevyo lango la Taifa Stars na Simba lipo salama kwa muda mrefu ujao. Natamani tu kama Yanga na Azam nao wangekuwa na makipa wa kizawa wenye uwezo mkubwa kwa ajili ya kumpa changamoto Aishi. Hata hivyo wao wameamua kwenda kwa wageni baada ya wazawa kutoonyesha uwezo.

Mara nyingi makipa wazawa wanaocheza katika timu kubwa ndani ya nchi huwa wanapeana presha kubwa ya kufanya vizuri kwa sababu kunakuwa na kundi kubwa la mashabiki ambao wanasimama nyuma yao na kutoa sapoti.

Makala haya yameandikwa na Edo Kumwembe na kuchapishwa kwanza kwenye wavuti la Mwanaspoti

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here