Home Habari za Usajili Yanga BAADA YA BIGIRIMANA….YANGA WAMTUPIA NDOANO USENGIMANA…NI BEKI LA KAZI HASWA….

BAADA YA BIGIRIMANA….YANGA WAMTUPIA NDOANO USENGIMANA…NI BEKI LA KAZI HASWA….


BAADA ya Yanga SC kuwa na wakati mzuri wa kuipata saini ya kiungo wa Kiyovu ya Rwanda, Obed Bigirimana, inaelezwa kwamba, pia wanakaribia kumsajili beki kisiki wa Polisi FC na Timu ya Taifa ya Rwanda, Faustin Usengimana.

Usengimana mwenye uwezo wa kucheza beki wa kati, kulia na kushoto, alijiunga na Polisi FC Julai Mosi 2020 akitokea Buildcom ya Zambia.

Chuma hicho chenye umbo kubwa, anatajwa kuwa ndiye atakuwa mchezaji sahihi wa kucheza sambamba na nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto.

Eneo la ulinzi la kati ndani ya Yanga, kwa sasa lipo chini ya Mwamnyeto ambaye amekuwa akicheza pacha na Dickson Job, wakati mwingine Yanick Bangala.

Mabeki wengine wa kati wa timu hiyo ni Ibrahim Abdallah Hamad ‘Bacca’ na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambao hawana nafasi kubwa ya kucheza.

Chanzo chetu kutoka Yanga, kimeliambia Spoti Xtra kuwa, kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi, amewaagiza viongozi kuhakikisha wanasajili beki wa kati ambaye ana uwezo wa kuingia kikosini moja kwa moja.

“Nabi amelazimika kutafuta beki mwenye umbo refu na mwili wa kutisha ili kuifanya safu hiyo kuwa na watu wenye uwezo mzuri katika mipira ya juu na chini, hivyo hapa ninapoongea na wewe tayari Injinia Hersi na kocha wetu Cedric Kaze wapo Rwanda wakimfuatilia beki huyo wa Polisi FC,” kilisema chanzo hicho.

Spoti Xtra lilimtafuta mmoja wa viongozi wa Polisi FC ambaye aligoma kuanikwa jina lake, huku akisema: “Ni kweli tumepata taarifa za ujio wa viongozi hao wa Yanga na kwamba nimesikia habari ya kumtaka beki wetu wa kati, Faustin Usengimana.

“Siku nyingi wamekuwa wakimtaka kutokana na kumfuatilia na kuridhishwa na uwezo wake akiwa anaweza kucheza nafasi zote za beki kwa maana ya katikati, kulia na kushoto, pia ana umbo la mpira.”

Spoti Xtra lilipomtafuta Usengimana kuhusiana na ishu hiyo, alisema: “Ni kweli nimesikia kuna viongozi wa Yanga wamenifuata kuhitaji kuzungumza na mimi, lakini mpaka sasa (jana), sikuwa nimekutana nao.”

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YA LEO DHIDI YA RUVU...MATOLA AVUNJA UKIMYA SIMBA...AFUNGUKA HALI ILIVYO NDANI...