Home Habar za Usajili Simba HUU HAPA ‘UMAFIA’ WA TRY AGAIN…ALICHOWAFANYIA TSHABALALA NA YANGA NI ZAIDI YA...

HUU HAPA ‘UMAFIA’ WA TRY AGAIN…ALICHOWAFANYIA TSHABALALA NA YANGA NI ZAIDI YA UJASUSI…


KAMA mabosi wa Simba wakitaka kumbakiza, Aishi Manula klabuni kwao, licha ya mkataba wake kuelekea ukingoni, unadhani kuna mtu anaweza kuwazuia?

Ukitaka kujua hilo, sikia kilichowakuta Yanga walipojaribu kutaka kuwasajili mabeki wa pembeni wa Simba, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Msimu uliopita Yanga iliwapigia misele mabeki hao hususani, Tshabalala na ilibaki kidogo tu atue Jangwani, lakini dili lilikwama jioni na beki huyo kumwaga wino na kubaki Msimbazi.

Inaelezwa, sio ajabu tena Manula pamoja na kuwindwa na timu nyingi lakini ataendelea kubaki Simba pamoja na mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu huu, kwani Simba in watu wenye kuijua kazi yao ya kuwasomesha wachezaji na kueleweka.

Inaelezwa Mwenyekiiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ aliupiga mwingi mbele ya Yanga na kuwaacha solemba kwenye dili la mabeki hao na kusalia kikosini.

Try Again aliweka watu wa kufuatilia ishu nzima ya kujua Kapombe na Tshabalala wanafanya makubaliano gani na Yanga, kisha akawajuza akiwaambia mavazi waliyovaa, muda waliokwenda Yanga hadi mazungumzo yaliyofanyika, kisha akamaliza ishu yao kirahisi kwa dau ambalo waliahidiwa kupewa upande wa pili.

Aliyefichua hilo ni Meneja wa Tshabalala, Herry Mzozo alisema kwanini mteja wake hakufanikiwa kuvaa uzi wa njano na kijani msimu wa 2021/22 wakati mazungumzo yalifika mbali.

“Asikwambie mtu Try Again ni ‘mafia’, narudia tena ni ‘mafia’, maana nishaongea na Yanga kila kitu baada ya kushindwa kuelewana na marehemu, Zacharia Hanspope lakini dakika za lala salama ndiye aliyeweza kufanikisha hilo,” alisema Mzozo na kuongeza; “Nakumbuka Hanspope (marehemu) alinipigia simu akaniita ofisini kwake Mbezi Beach nilienda na Tshabalala, lakini kulikuwa na dharau fulani hivi kuanzia mapokezi hadi ofisini, akaniambia nakupa Sh 80 milioni miaka miwili nilimkatalia nikamwambia kuna ofa Yanga zaidi ya hiyo.”

“Niliondoka na mchezaji lakini nilimwambia kwa kuwa nyie ndio timu yake nawapa wiki moja mnipe majibu, maana mchezaji wangu kabakiza mwezi mmoja kisheria kama meneja naruhusiwa kuzungumza na timu nyingine alidhani masihara kumbe nilikuwa namaanisha,” alifafanua.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA NYUMA GAZETI LA CHAMPIONI IJUMAA

Alisema baada ya wiki kupita hakuona kinachoendelea aliamua kuwa bize na Yanga, ndipo Simba waliposhtuka na Try Again akamwendea hewani na kumtaka wakaonane. Alipofika aliweka dau lake mezani na alikubali na biashara ikaisha.

“Kusema ukweli nilishangaa kuona anajua kila kitu kilichofanyika kule Yanga, nilibaki kimya na ndipo alipofanya uamuzi palepale wa kumbakiza Tshabalala na mchezaji aliridhia kubaki alipopazoea kuliko ugenini alikohitajika,”alisema.

Mzozo aliwataka viongozi wa klabu kubwa kuhakikisha zinakuwa makini na kuthamini wachezaji wao hasa wanaowaona wana umuhimu ndani ya kikosi kwa kulinda mikataba yao mapema.