Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI NA SIMBA…NABI AWALISHA KIAPO WACHEZAJI WAKE …ADAI LAZIMA...

KUELEKEA MECHI NA SIMBA…NABI AWALISHA KIAPO WACHEZAJI WAKE …ADAI LAZIMA ‘WAMPASULE YAI’….


Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddin Nabi amefichua siri nzito kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba SC, utakaopigwa Jumamosi (April 30), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Young Africans inayoongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 54, itakua mwenyeji wa mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka kila pande ya nchi.

Kocha Nabi ambaye hatokua sehemu ya Benchi la Ufundi siku ya mchezo kutokana na adhabu ya kufungiwa michezo mitatu, amesema tayari wameshakubaliana na wachezaji wake kuhakikisha wanashinda mchezo huo, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Amesema mbali na upande wa wachezaji, pia Uongozi na Maafisa wengine wa Young Africans wamejizatiti kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri ili kufikia lengo la kuondoka na alama tatu muhimu Jumamosi (April 30).

“Tumeshakubaliana na wachezaji kuhakikisha tunashinda mchezo wetu dhidi ya Simba SC, lengo ni kupata alama tatu ambazo zitaendelea kutuweka katika mazingira ya kutwaa ubingwa msimu huu.”

“Viongozi na hata Maafisa wengine wa Young Africans nao wanajua umuhimu wa mchezo huu, hivyo kila mmoja amejipanga kufanya kazi yake ili kufanikisha lengo la kushinda dhidi ya Simba SC.” Amesema kocha huyo kutoka nchini Tunisia.

Katika hatua nyingine Nabi amewataka wachezaji wake kuhakikisha wanabadilika na kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo uliopita, na kama watashindwa kufanya hivyo basi itakua ngumu kwao kufikia lengo la kuiadhibu Simba SC.

“Tunapaswa kubadilika ili kuifunga Simba SC siku hiyo, wenzetu wana timu nzuri yenye wachezaji bora na imara, tukifanya makosa hawatasita kutuadhibu, hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunabadilika kwa kuondoa kasoro zilizojitokeza siku za nyuma.” Amesema Nabi.

Young Africans Jumamosi (April 23) iliifunga Namungo FC mabao 2-1, huku Mshambuliaji wao hatari kutoka DR Congo akifunga bao lake la 12 msimu huu, na bao lingine katika mchezo huo likifungwa na Kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’.  

SOMA NA HII  HAYA HAPA MAJUKUMU MAPYA YA CARLINHOS YANGA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here