Home Habari za michezo MASAU BWIRE: TUSIDANGANYANE..WALE WASAUZI SIO WEPESI KIIVYO..SIMBA MSIPOJIPANGA NI KILIO TU…

MASAU BWIRE: TUSIDANGANYANE..WALE WASAUZI SIO WEPESI KIIVYO..SIMBA MSIPOJIPANGA NI KILIO TU…


NIKIWA nimelala usingizi usiku wa Aprili 6, 2022, kuna kitu nilioteshwa. Ilikuwa ni ndoto ndefu kidogo iliyokuwa na mambo mengi mazito Simba ikiwemo. Nilioteshwa ndoto ya mechi ya Simba na Orlando Pirates kwenye robofainali ya Shirikisho Afrika. 

Pamoja na mambo mengine meengi ambayo yalikuwa kwenye ndoto ile ambayo nimeyasahau kwavile badae nilikuja kushtuka, moja ninalolikumbuka ni mashabiki waliokuwa wakinitaka nihamasishe na kuwatia moyo Watanzania wenzangu, kuwakumbusha kuisapoti na kuishangilia Simba katika mchezo huo muhimu. 

Walinisifia kwa mambo mengi lakini wakataka nizungumze chochote kwa sauti yangu kuhusiana na mchezo huo uliobeba masilahi mapana ya Taifa.

Nilishtuka kutoka usingizini na katika ndoto hiyo nikatazama saa kwenye moja ya simu zangu ikionyesha ni saa 6.33 usiku. Hapohapo kwa kutumia simu hiyo nikaanza kutekeleza takwa hilo kuandika ujumbe huu ili niwahamasishe na kuwakumbusha Watanzania wote wazalendo kuisapoti na kuishangilia Simba katika mchezo huo mgumu dhidi ya timu hiyo ngumu kutoka Afrika Kusini.

Kabla sijaenda mbali zaidi kuhusu hamasa niliyoelekezwa kwa Watanzania kupitia ndoto katika usingizi mzito, usiku mnene, nianze kwa kuwapongeza wachezaji wa klabu ya Simba kwa kupambana kwao katika hatua ya makundi na kuiwezesha timu hiyo kufuzu hatua ya robo fainali ikiwa katika nafasi ya pili nyuma ya RS Berkane iliyoongoza Kundi D lililokuwa na timu nne, nyingine mbili ambazo hazikufuzu zikiwa ni Asec Mimosas na US Gendermerie.

Wachezaji wa Simba hongereni, mlijitoa na mlijituma mno kuipambania timu hadi kuiwezesha kufikia hatua iliyopo sasa – hatua ya robo fainali ya mashindano hayo hasa mchezo wa mwisho dhidi ya US Gendermerie, Uwanja wa Benjamin Mkapa uliohitaji ushindi ili kufuzu. Mkafanya kweli, mkawapapasa mipapaso minne bila majibu wageni hao kutoka Niger. Bila uongozi thabiti na imara, wenye mipango na mikakati inayosimamiwa vyema siyo rahisi kuyafikia mafanikio makubwa na mapana yaliyofikiwa na klabu hiyo ya Msimbazi, uongozi wake.

Binafsi nikiri kwamba uko vizuri. Kuna mshikamano na ushirikiano miongoni mwao. Kwa ujumla wao niwape kongole kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya katika kuiongoza kwa malengo klabu yao. Kundi jingine ambalo nisipolipongeza kuhusu mafanikio ya Simba nitakuwa bado sijakamilisha pongezi zangu ni la wanachama, mashabiki, wadau, wapenzi wa Simba na Watanzania wote wazalendo ambao wamekuwa wakijitoa kikamilifu wakitumia muda na fedha zao kwenda uwanjani timu inapocheza, kuisapoti na kuishangilia kuhakikisha kupitia kelele zao hamasa na morari kwa wachezaji uwanjani vinaongezeka na kuchagiza ushindi.

Sisi sote ni mashuhuda kauli ya ‘kwa Mkapa hatoki mtu’ inashamirishwa na mashabiki. Mashabiki wanapoujaza uwanja makelele ya ushangiliaji yakasikika hakika humtia hofu mgeni, mpinzani wao huyo humpoteza mwelekeo na umakini wa mchezo, hivyo kuwezesha mpapaso laini na mololo kwake. Hatua hiyo ya robo fainali iliyofikiwa na Simba na timu nyingine saba kutoka mataifa mengine matano ni kubwa mno inayoiheshimisha Wekundu wenyewe pia nchi kwa ujumla katika soka la Afrika.

Katika hatua hiyo ya robo fainali Misri imeingiza timu mbili ambazo ni Al Masry na Pyramids, kadhalika Libya nayo imeingiza timu mbili – Al Ittihad na Ahli Tripoli; pia kuna Orlando, Simba, TP Mazembe na RS Berkane.

Katika droo iliyochezeshwa nchini Misri, Aprili 5, 2022, Simba ilipangwa kucheza na Orlando – mchezo wa awali utachezwa kwa Mkapa Aprili 17 na baadaye wa marudiano utakaochezwa Uwanja wa Orlando, Afrika Kusini, Aprili 24 mwaka huu.

Michezo mingine itakayochezwa katika hatua hiyo ambayo ni ya mtoano ni pamoja na utakaozikutanisha timu zote za Libya – Al Ittihad dhidi ya Ahli Tripoli; Pyramids dhidi ya TP Mazembe na Al Masry dhidi ya RS Berkane. Kwa mujibu wa droo hiyo hatua ya nusu fainali, mshindi kati ya Simba na Orlando atacheza na mshindi kati ya Al Ittihad na Ahli Tripoli, mshindi kati ya Pyramids na TP Mazembe atacheza na mshindi kati ya Al Masry na RS Berkane.

SOMA NA HII  ZA NDAANI KABISAA...MASHINE HII YA MAGOLI YANUKIA MSIMBAZI...MABOSI SIMBA WAMWAGA PESA...

Hatua hiyo kwa macho na fikra za kimapenzi na kishabiki unaweza ukaiona nyepesi kwa timu yako kupenya, lakini ukweli ni kwamba ni ngumu na ili ufanikiwe, upenye, uingie nusu fainali lazima ujipange, ujizatiti na upambane kwelikweli.

Wapo watakaosema Simba inacheza na timu ambayo kwa sasa siyo imara, haina ubora kama enzi hizo, imefuzu robo fainali kwa kuwa kundi lake lilikuwa na timu dhaifu, tutashinda tu na tutafuzu nusu fainali. Hayo yakiwa mawazo na timu ikasafiri nayo Watanzania mapema tu tutaduwazwa, tutang’olewa mchana kweupe.

Orlando ni timu kubwa ina uzoefu wa kutosha katika mashindano ya Kimataifa. tusiidharau hata kidogo, tujipange na tukapambane kwa nguvu na maarifa yote.

Timu zote zilizofika robo fainali hazikufika kwa kubahatisha ni uwezo na kupambana, hivyo Simba msifanye mzaha kuwadharau Orlando. Kazeni mwanzo – mwisho ushindi upatikane.

Furaha ya wana Simba, Watanzania wote wazalendo ni kuona timu inafuzu nusu fainali ambayo kwa kweli haiji kirahisi hivyo itatokana na timu kupambana, wachezaji kujitoa na kujituma kuhakikisha ushindi dhidi ya Orlando kwa vyovyote vile, kwa jasho na damu unapatikana.

Niombe na kusihi sana Simba utumieni vizuri uwanja wa nyumbani, Benjamin Mkapa kama ilivyo jadi yenu ‘kwa Mkapa hatoki mtu’ ipambanieni. Orlando asitoke kweli, tena ushindi dhidi yao uwe wa magoli mengi kwa uchache yasipungue matatu, ili mchezo wa marudiano huko kwao uwe rahisi kwenu na ngumu kwao kupenya.

Viongozi, benchi la ufundi, wachezaji, wanachama na mashabiki wote wa Simba, Watanzania wote wazalendo ebu kila mmoja kwa nafasi yake tuipambanie timu, tuhakikishe inapata matokeo chanya katika mchezo huo muhimu na mgumu.

Kwenye umoja mafanikio hupatikani. Katika mchezo huo Watanzania tuungane, tuwe wamoja, tuisapoti, tuishangilie timu ya nchini kwetu tuiwezeshe kupata ushindi na kusonga mbele.

Ifike wakati tubadilike, tujifunze, tuige na tufurahie mafanikio ya wenzetu ndani ya nchi, tusaidiane na kushirikiana nao katika vita yao, tuwape mbinu, tuungane nao, tuhakikishe wanashinda. Simba wako vitani tusiwaache wapigane wenyewe. Watanzania wote wazalendo tuungane nao kwa namna fulani hivi, tupigane nao vita yao, ushindi wao ni faida kwetu na sifa kwa nchi yetu.

Utafaidika nini ukimsapoti Orlando Pirates ili ashinde dhidi ya Simba na utapata hasara gani ukiiunga mkono Simba ikamshinda Orlando Pirates na kusonga mbele nusu fainali ya mashindano hayo. Umuhimu wa Simba kushinda mchezo huo ni mkubwa mno.

Ushindi wa Simba SC una tija kubwa kwa nchi, hivyo ni vizuri tukashikamana Watanzania tuiombee mema na ushindi katika mchezo huo, kuiombea mabaya Simba SC wakati ushindi wake unatunufaisha sote ni kukosa utu na uzalendo.

Binafsi nina imani kubwa na uwezo wa Simba SC. Wana uwezo mkubwa wa kushinda mchezo huo, lakini waandaliwe na kujengewa uwezo zaidi wa ushindi. Wajiamini na kuamini kwamba wanaweza, ila kamwe wasiwadharau wapinzani wao, Orlando Pirates.

Makala haya yaliandikwa na Masu Bwire na kuchapishwa kwanza kwenye Wavuti la MwanaSpoti.