Home Habari za michezo BAADA YA KUWAONA YANGA WALIVYOCHEZA JUZI…PABLO KAGUNA MARA TATU….KISHA AKASEMA JUMAMOSI KAZI...

BAADA YA KUWAONA YANGA WALIVYOCHEZA JUZI…PABLO KAGUNA MARA TATU….KISHA AKASEMA JUMAMOSI KAZI IPO AISEE…


KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco, juzi alikuwa miongoni mwa wapenzi wa soka waliojitokeza kushuhudia mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Biashara United na Yanga, ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba, hiyo ikionekana ni njia mojawapo ya kuwasoma wapinzani wake kabla ya Jumamosi timu hizo kukutana kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA.

Mechi hiyo ilipigwa ikiwa ni siku moja baada ya kikosi chake cha Simba kupata matokeo kama hayo uwanjani hapo dhidi ya Geita Gold FC, huku Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, naye akiwa ni miongoni mwa walioshuhudia mechi hiyo ya Ligi Kuu pia.

Hata hivyo, baada ya Nabi kuisoma Simba, ambayo siku hiyo ilimpumzisha beki wake wa kati, Henoc Inonga, ambaye amekuwa akimnyima raha ya kutetema, mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele, Wanajangwani hao nao juzi walipumzisha mastaa wao wengi.

Mastaa wa Yanga ambao walipumzishwa na Yanick Bangala, Khalid Aucho na Kibwana Shomari, ambaye amekuwa katika kiwango cha juu hivi karibuni.

Baada ya kumaliza kusomana, jana Pablo alimwambia mwandishi wetu kuwa ana kazi ya kufanya katika safu yake ya ushambuliaji kwa kuwapa mbinu za kiufundi kuweza kutumia vizuri nafasi wanazotengeneza ili kupata mabao kwenye mechi hiyo  Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), dhidi ya Yanga.

Kikosi cha Simba jana asubuhi kilianzia mazoezi gym ili kuweka miili yao sawa kabla ya jioni kujifua Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, ikiwa ni maandalizi kuelekea mchezo huo dhidi ya Yanga utakaopigwa katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Pablo alisema licha ya kuwapo kwa changamoto ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini wamepania kutetea Kombe la Shirikisho.

Alisema kulingana na ukubwa wa Simba ulivyo, aina ya mashindano wanayoshiriki anahitaji kuona kila mchezaji anakuwa kwenye ubora ikiwamo mechi za ligi zilizobaki na dhidi ya Yanga katika mchezo wa nusu fainali ya Shirikisho.

“Kuna makosa ambayo yamekuwa yakijirudia katika mechi dhidi ya Azam FC tulitengeneza nafasi na kushindwa kufunga, sasa tunafanyia kazi hilo kuhakikisha hatukosi vyote kwa msimu huu, tuhakikishe tukikosa ligi basi tunatetea Kombe la Shirikisho,” alisema Pablo.

SOMA NA HII  MBRAZILI SIMBA AJIAPIZA KUANGUSHA TEMBO LEO....ATAKA HESHIMA AFRIKA MZIMA...

Alisema kwa namna hiyo wanatakiwa kuwekeza nguvu zao na kufanyika kazi mapungufu yao ili kupambana kuhakikisha wanashinda dhidi ya Yanga na kucheza fainali ya kombe hilo.

Pablo alisema hatakubali kirahisi kupoteza mataji yote, hivyo wanaingia vitani kuboreshwa madhaifu yao hasa safu ya ushambuliaji kuhakikisha wanakuwa makini na kumalizia nafasi wanazotengeneza kuzaa mabao.