Home Habari za michezo ISHU YA AJIB NA NDEMLA …NI SAWA NA MMOJA KUCHAGUA PEPO NA...

ISHU YA AJIB NA NDEMLA …NI SAWA NA MMOJA KUCHAGUA PEPO NA MWINGINE KABURI…AZAM WALIPASWA KUANGALIA HILI…


MAISHA yanaenda kwa kasi sana. Yanaenda kasi zaidi kwa baadhi ya wachezaji wa soka nchini. Wapo wanaopanda kwa haraka na wengine wanaanguka. Kila mtu anachagua njia yake. Hivi ndivyo ilivyo kwa nyota wawili wa zamani wa Simba, Said Ndemla na Ibrahim Ajibu. Kila mmoja amechagua njia yake. Mmoja ameamua kwenda peponi na mwingine kaburini.

Mwanzoni mwa msimu huu ilionekana wazi, Ndemla na Ajibu hawana nafasi katika kikosi cha Simba. Kuna namna ubora wa Simba ulikuwa juu sana, halafu wao wakawa chini. Sote tunakubaliana kuwa hawa ni wachezaji wenye vipaji vikubwa sana. Lakini tatizo lao ni moja. Hawajitumi sana. Wanacheza kawaida.

Ndemla alipoona nafasi yake imepotea kabisa pale Simba akaamua kwenda Mtibwa Sugar. Hakuwa na mwanzo mzuri sana. Inawezekana ni kwa sababu za kisaikolojia.

Hakuwaza kama maisha yake pale Simba yangekwisha haraka namna ile. Tangu ameanza kucheza soka, Ndemla amecheza Simba. Hakuwahi kuwaza kama ipo siku atacheza katikati ya mashamba ya miwa pale Manungu.

Lakini angefanya nini? Pale Simba viungo karibu wote walimzidi uwezo. Halafu bado akasajiliwa Sadio Kanoute. Ndemla angecheza wapi? Hakuna. Ilikuwa ngumu kwa Ndemla kuamini kuwa sasa anacheza Mtibwa. Na ndio sababu ilimchukua muda mrefu kucheza kwa ubora. 

Lakini baada ya kujikubali sasa tumeanza kumuona Ndemla yule wa 2014. Wa moto kweli kweli. Mtibwa imeanza kumrejeshea heshima yake iliyokuwa imepotea. Amekuwa mchezaji muhimu tena. Anacheza kila siku katika kikosi cha kwanza cha Mtibwa. Kwanini asirejee kwenye makali yake? Mchezaji ili uwe bora ni lazima uwe unacheza kila mwisho wa wiki. 

Hiki Ndemla alikuwa anakikosa pale Simba. Hakuwa akipata nafasi kila wiki. Alipata nafasi chache pia kila mwezi. Lakini pale Mtibwa Sugar sasa ana uhakika wa kucheza kila siku. Kwanini asiwe bora? Hii ndiyo sababu umeanza kusikia Azam FC inamtaka Ndemla. 

Unaweza kusikia pia Simba ikitaka kumrejesha. Kwanini? Kwa sababu anacheza kila siku. Ndemla alichagua Mtibwa kwa sababu aliamini katika ubora wake. Aliamini anahitaji kucheza ili kurejesha makali yake. Ukweli ni kwamba anarudi kwa kasi sana.

SOMA NA HII  HUU HAPA UKWELI KUHUSU KIFO CHA DK GEMBE...ALIKUWA TIMU KUBWA YA SIMBA AKASHUSHWA MPAKA TIMU YA WATOTO...

Wakati Ndemla akichagua sehemu ya kunyanyua kiwango chake, Ajibu wala hakujali. Akaendelea kusalia pale pale Simba. Akaamini atapata nafasi ya kucheza. Nini kilitokea?

Alipewa nafasi kwenye mechi chache za mwanzoni. Baada ya hapo akarudi kule kule alipotoka. Akawa mchezaji wa benchi. Baadaye akawa mchezaji wa jukwaani. Mchezaji wa mazoezini tu.Mwisho wa siku Simba ikaamua kuachana naye. 

Ilikuwa rahisi kuyaona haya. Mwisho wa Ajibu ulishaonekana mapema. Utaendeleaje kusalia Simba kama huchezi? Tena kwa mchezaji anayelipwa fedha nyingi. Bahati mbaya zaidi kwa Ajibu akachagua kwenda Azam. Akaamini kuwa anaweza kuwa chaguo la kwanza pale Chamazi. Nini kimetokea?

Alianza kuwa mchezaji wa benchi na sasa amerudi tena jukwaani kama ilivyokuwa pale Simba. Inashangaza sana. Wakati Ndemla akirejesha ubora wake kwa kasi kubwa, Ajibu amezidi kuisha. Kwanini? Ni kwa sababu hachezi. 

Ajibu na Ndemla walikuwa na tatizo moja. Ni wachezaji wasiojituma sana. Lakini kwa Ndemla mambo yamebadilika ila Ajibu ameendelea kuwa vilevile. Ukweli Ajibu hajitumi. Bado hana nidhamu ya kutosha mazoezini. 

Bado hana jitihada kwenye mechi. Hili ndio tatizo lake kubwa. Azam walipaswa kuliona hilo kabla ya kumsajili. Ni kweli Ajibu ana uwezo mkubwa, lakini ni mpaka atakapoamua kucheza kwa kujituma. Ni kama tu alivyo Bernard Morrison. 

Anaweza kucheza vizuri leo, lakini utasubiri sana kuuona ubora uleule. Namuona Ndemla akirejea kuwa mchezaji mkubwa kama zamani. Lakini Ajibu mwisho wake ni kama umekaribia. Azam watamchoka siku sio nyingi. Ni ngumu kukaa na mchezaji asiyejituma