Home Habari za michezo KISA MECHI ZA TIMU KUBWA….HIVI NDIVYO WAAMUZI WA BONGO WANAVYOROGWA NA KUROGANA...

KISA MECHI ZA TIMU KUBWA….HIVI NDIVYO WAAMUZI WA BONGO WANAVYOROGWA NA KUROGANA KICHAWI….


Na Masau Bwire.

TAKRIBANI matoleo mawili ya nyuma, katika safu hii ya Mpapaso wa Masau Bwire, tumehabarishana kwa ufupi kuhusu ushirikina na uchawi katika soka letu Tanzania.

Tuligusa na kutazama namna ambavyo baadhi ya timu katika ligi, madaraja mbalimbali zinavyojihusisha na kujishughulisha zaidi katika ushirikina na uchawi kama moja ya vyanzo vikubwa vya mafanikio na ushindi katika michezo.

Tuliangalia pia baadhi ya wachezaji wanavyojikita katika ushirikina na uchawi wakiamini kwamba kwa kufanya hivyo watafanikiwa kisoka na watakuwa bora, wenye viwango vya juu katika kusakata kandanda.

Katika mpapaso wa leo nitaangazia zaidi waamuzi wa mchezo wa mpira wa miguu ambavyo baadhi yao wamewekeza kwenye ushirikina na uchawi kwa matarajio ya ufanisi wa kazi yao. Awali, kabla ya kueleza chochote kuhusu urozi na wanga kwenye soka kwa waamuzi, nianze kwa kuwataka radhi wapenzi wasomaji wa gazeti hili na safu hii ya Mpapaso kutokuwa hewani wiki iliyopita.

Nilipokea simu na ujumbe mwingi kutoka kwa wasomaji wakihoji sababu za Mpapaso kutochapishwa wiki hiyo iliyopita katika gazeti hili. Samahani na poleni sana wasomaji wa safu hii kilichotokea na kusababisha hayo kilikuwa nje ya uwezo, hivyo ikalazimika kuwa hivyo. Tutajitahidi hali hiyo isitokee mara nyingine tena. Baada ya samahani hiyo ambayo naamini wasomaji wangu mmeipokea na tayari mmesamehe tujikite kwenye hoja ya leo namna baadhi ya waamuzi wa mpira wa miguu wanavyojihusisha na kuhangaika mchana na usiku kuusaka ushirikina na uchawi ili wafanikiwe katika kazi.

Amini usiamini hawa jamaa – waamuzi wa soka hawapo nyuma baadhi yao nao ni hatari wako ‘sharp’ mno katika kusaka mafanikio kwenye kazi hiyo kwa njia ya ushirikina na uchawi. Katika uchunguzi wangu nikizungumza na baadhi ya waamuzi na wadau wa karibu wa kada hiyo wakiwemo baadhi ya waliowahi kuwa maofisa wa Bodi ya Ligi (TPLB), wakufunzi na viongozi wa mpira wa miguu nimebaini misukosuko mingi waamuzi wanayopambana nayo ya ushirikina na uchawi katika kazi.

Nimeelezwa baadhi ya waamuzi wanapokuwa kwenye mitihani ya mchujo na kupendekezwa kuchezesha ligi katika madaraja mbalimbali, ushirikina na uchawi hutumika na ni mwendo wa ndumba kuhakikisha hakuna kufeli na wanaamini bila hirizi ‘power bank’ hakuna kufanikiwa.

“Siku moja katika mtihani wa kukimbia wa waamuzi Uwanja wa Benjamin Mkapa, muda mfupi kabla ya mbio hizo kuanza nilikuwa na mwamuzi mmoja wa kike. Rafiki yangu sana. Alifunga hirizi katika mkono wake wa kushoto jirani kabisa na kwapa. Akaifunika kwa nguo aliyoivaa aliniambia bila hiyo hawezi kutoboa,” alinambia mdau mmoja wa soka aliyewahi kuwa ofisa wa TFF na kuongeza:

“Inamuongezea nguvu, hachoki, lakini pia ni kinga kwa yeyote atakayejaribu kufanya lolote baya kwake ili afeli mtihani huo. Pia akadai kwamba inawapofusha, kuwashawishi na kuwapumbaza wasimamizi wamuone anafaa na kumchagua.” Mmoja wa waamuzi hao kwa sharti la kutomtaja jina aliniambia waamuzi wengi wanatumia ushirikina na uchawi ili washinde mitihani, wachaguliwe kuchezesha na wengine wanaroga ili wapangwe kuchezesha mechi kubwa. Alisema ushirikina na uchawi sio tu kwamba upo kwa timu na wachezaji hata wao waamuzi umeshamiri na kuota mizizi na ili mwamuzi afanikiwe apangwe mechi nyingi kuchezesha, achezeshe mechi kubwa anaamini lazima ndumba zifanye kazi.

Naye mwamuzi mmoja mbobezi na mahiri alinieleza wapo baadhi ya waamuzi anapoingia uwanjani lazima awe na kinga vinginevyo anaweza akaharibu kazi, kwani baadhi ya timu na wachezaji wanawaroga sana waamuzi ili wafanye makosa yatakayowanufaisha wao.

SOMA NA HII  KOCHA SIMBA AKWAMISHA DILI LA MKUDE..."YUPO NA ATAKUWEPO HAONDOKI....AMEZUNGUMZA HAYA

Mwamuzi mmoja niliyewahi kumlalamikia miaka ya nyuma kwa kuchezesha vibaya moja ya mechi ya timu ya Ruvu Shooting dhidi ya timu pendwa za Kariakoo alinipigia simu akaniambia nisimlaamu kwa kilichotokea, hakuwa yeye kulikuwa na nguvu za ziada zilizomuelekeza katika kufanya makosa.

Mwamuzi huyo alidai ushirikina na uchawi kwenye mpira wa miguu umekuwa mkubwa na wa kutisha, ukiingia uwanjani kichwakichwa bila kinga yoyote utaziona dakika 90 kama tanuru la moto uwakao. Aliongeza kwamba aliwahi kuchezesha timu fulani hivi za Ligi Kuu (alinitajia) ghafla akajikuta hauoni mpira, macho hayaoni akalazimika kusimamisha mpira kwa kisingizio cha mapumziko ya kunywa maji akakitumia kuwasiliana na babu yake ambaye ni mganga wa jadi, alimjulisha tukio hilo, na babu akatuma ‘askari wa vita’ waliopambana na kuishinda nguvu iliyokuwa ikimfanya asiuone mpira uwanjani.

Waamuzi wengi niliozungumza nao kwa nyakati na maeneo tofauti wameeleza kwamba ushirikina na uchawi katika kazi hiyo upo kwa kiasi kikubwa wakidai wapo wengine wanaoamua kuwaroga wenzao ili wasifanikiwe – waharibikiwe.

“Tunarogana sana waamuzi wa soka mwamuzi anaweza kumroga mwamuzi mwenzake ili afeli mtihani, asichaguliwe kuchezesha au aharibu mchezo ili aadhibiwe au aondolewe kwenye kazi ya uaamuzi,” alisema mwamuzi mmoja kwa sharti la kutotajwa.

“Wakati fulani nilipokuwa nikichezesha mechi ya ligi nilikuwa naona miba uwanjani iliyokuwa inanifanya nishindwe kukimbia na wakati fulani nikawa kama navutwa miguu na mtu ambaye sikuwa namuona. Nilichezesha kwa shida mchezo ule na nilishtakiwa kwenye Kamati ya Saa 72 walioniadhibu kwa kuniondoa kwenye ratiba kwa kushindwa kuumudu mchezo bila kujua nilikumbana na majanga gani uwanjan.”

Mwamuzi mwingine alidai kwamba akiwa uwanjani – Uwanja wa Taifa – kwa sasa Benjamin Mkapa akichezesha mechi iliyohusisha moja ya timu kubwa ya Dar es Salaam alijikuta wakati fulani hawaoni wachezaji, anauona mpira tu hivyo akawa hawezi kupiga filimbi katika makosa yaliyokuwa yakifanyika ambayo watazamaji walikuwa wakiyaona na kusababisha kuchezesha chini ya kiwango na kuadhibiwa, japo hakutaja adhibu aliyoadhibiwa.

 “Matukio ya ushirikina na uchawi kwa waamuzi yapo mengi tu. Siku moja nikichezesha mechi ya Ligi Kuu huko mikoani timu moja ilipokuwa ikishambulia nilikuwa nashikwa na kichomi nashindwa kabisa kukimbia, lakini ikipoteza mpira na kushambulia nilikuwa kawaida, kichomi sikukisikia kabisa,” alinieleza mwamuzi mwingine. 

Mwamuzi mwingine alinieleza ilitokea siku moja akichezesha timu fulani mchezaji akitenda kosa mkono ulikuwa mzito kuweka filimbi mdomoni na kusababisha kuchelewa kuipiga kwa wakati akawa anaipiga kwa kuchelewa wakati tayari mpira umeondoka eneo la tukio, umechezwa pasi kadhaa hali iliyosababisha aadhabiwe kwa kushindwa kuumudu mchezo. 

Waamuzi wengi niliozungumza nao wanasema wanakumbana na majanga makubwa uwanjani na kwamba wakati fulani wanapoonekana kushindwa kuumudu mchezo siyo kwamba wanafanya kwa makusudi kwa sababu yoyote ile ikiwemo ya kuhongwa ili wapendelee timu fulani kama wengi wanavyodai, bali wanazidiwa na ushirikina na uchawi.

“Siyo rahisi kuamini tunayokumbana nayo uwanjani waamuzi. Ushirikina upo tunarogwa na tunarogana sana. Yanatokea makosa ya kushindwa kuumudu mchezo. Kabla ya kuadhibiwa ni vizuri tukasikilizwa nini kilitokea uwanjani na kusababisha hali hiyo kutokea. Nguvu za giza ni kubwa, zinatupoteza uwanjani,” anasema mmoja wa waamuzi. Hayo ni baadhi ya maelezo ya waamuzi kuhusu ushirikina na uchawi unavyochukua nafasi katika kazi ya uamuzi.

Jumamosi ijayo nitaeleza kidogo kuhusu matukio kadhaa ya ushirikina na uchawi yaliyowahi kutokea na kuikumba timu ya Taifa ‘Taifa Stars.’

Makala haya yaliandikwa na kuchapishwa kwanza kwenye wavuti na gazeti la MwanaSpoti,

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here