Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA KESHO…WAZIRI Jr ATAMBA KUPELEKA ‘KILIO’ YANGA…MASUDI DJUMA ATOA MKWARA…

KUELEKEA MECHI YA KESHO…WAZIRI Jr ATAMBA KUPELEKA ‘KILIO’ YANGA…MASUDI DJUMA ATOA MKWARA…


Yanga haijafunga bao hata moja katika mechi zake tatu zilizopita za Ligi Kuu na wakati presha ya wapinzani wao Simba kupata matokeo mazuri ikiongezeka, straika wa Dodoma Jiji FC, Waziri Junior ametamba kuwafunga waajiri wake hao wa zamani na kuwavurugia mbio zao za ubingwa.

Dodoma Jiji itaialika Yanga katika mchezo wa raundi ya 24 ya ligi Jumapili hii katika mechi ambayo Wanajangwani watakuwa na hasira za kutoka sare mechi tatu mfululizo dhidi ya Simba, Ruvu Shooting na Tanzania Prisons wakati Dodoma Jiji ikiwa na morali kubwa baada ya kuvuna alama saba katika mechi tatu.

Waziri alisema wao kama timu wanajua wanaenda kukutana na timu kubwa ambayo pia inapambana kutaka ubingwa lakini amejiandaa kwa kushirikiana na wenzake kuhakikisha Yanga haitoki salama kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Alisema yeye kwake kuifunga Yanga haitokuwa jambo la ajabu wala la kubahatisha kwani amewahi kuifunga kwahiyo katika mchezo ujao pia amejiandaa kuwafunga na kubakisha alama tatu nyumbani ambazo zitawafanya kuisogelea nafasi ya nne katika msimamo.

“Kwangu siyo kitu kwa ajabu nimewahi kuzifunga timu kubwa zote kwahiyo hata mchezo wa Jumapili tumuombe Mungu tuamke tu salama siku hiyo nitafunga,” alisema Waziri, ambaye alijiunga na Dodoma Jiji katika dirisha dogo la usajili lililopita akitokea Yanga, ambako alitua akitokea Mbao FC.

Waziri amefunga mabao mawili katika mechi nane alizoitumikia Dodoma Jiji msimu huu na hakufunga bao mwanzoni mwa msimu alipokuwa Yanga ambako hakuwa akipata nafasi ya kutosha katika kikosi cha kocha Nasreddine Nabi.

Kocha wa Dodoma Jiji, Masoud Djuma alisema wamejiandaa vyema kukabiliana na Yanga ambayo wanajua itakuja katika mchezo huo kama mnyama mkali ambaye amejeruhiwa lakini kutokana na ubora wa kikosi chake kilivyo kwa sasa anaamini wataweza kupambana nao.

Alisema ligi imekuwa ngumu kila timu inapambana kutaka kushinda na kujisogeza juu huku zingine zikipambana zisishuke daraja lakini kama Dodoma Jiji wao mikakati ni kumaliza ndani ya nne bora na kwenda kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa.

SOMA NA HII  MOSES PHIRI AWAAGA WACHEZAJI WENZAKE ZAMBIA...MENEJA WAKE AFUNGUKA TIMU ATAKAYOICHEZEA TZ...

Dodoma Jiji iko katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa alama 28 baada ya michezo 23.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here