Home Habari za michezo KUELEKEA MSIMU UJAO…SIMBA KUSAJILI MAPRO SITA WAPYA WA KIGENI….PANGA KUPITA NA HAWA…

KUELEKEA MSIMU UJAO…SIMBA KUSAJILI MAPRO SITA WAPYA WA KIGENI….PANGA KUPITA NA HAWA…


KATIKA kuhakikisha wanakuwa na kikosi imara watakachokitumia katika michuano ya kimataifa msimu ujao, Simba SC imepanga kuachana na wachezaji sita wa kigeni mwishoni mwa msimu huu ambao mikataba yao inamalizika.

Hiyo ni katika kuhakikisha wanakuwa na kikosi imara kitakachofanikisha malengo yao ya kufika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa Afrika inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Baadhi ya wachezaji ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu ni Chris Mugalu, Meddie Kagere, Bernard Morrison, Rally Bwalya na Joash Onyango.

Mmoja wa mabosi wa Simba wenye ushawishi wa usajili, amesema kuwa, wamepanga kusajili wachezaji wapya sita wa kigeni watakaokuja kuchukua nafasi ya nyota hao watakaowaacha.

Bosi huyo aliongeza kuwa, pia wataachana na wachezaji wazawa wanne ambao wameshindwa kuonesha kiwango bora msimu huu.

Aliongeza kuwa, uongozi wa timu hiyo, hivi sasa upo katika mazungumzo ya kimyakimya na baadhi ya wachezaji watakaokuja kuichezea Simba akiwemo mshambiliaji wa US Gendarmerie, Victorien Adebayor.

“Mara baada ya malengo yetu kutotimia msimu huu ya kufika nusu fainali katika michuano ya kimataifa, haraka uongozi umeanza mikakati mipya kuelekea msimu ujao ambao ni muhimu kufika hatua hiyo.

“Mikakati tunayoanza nayo ni kutengeneza kikosi kitakachokuwa imara ambacho kitafika nusu fainali katika michuano ya kimataifa.

“Hivyo ni lazima tufanye usajili wa wachezaji wenye kiwango bora na uzoefu wa kucheza michuano hii ya kimataifa watakaotufikisha mbali,” alisema bosi huyo.

Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, hivi karibuni alizungumzia wachezaji watakaowasajili na kuwaacha akisema: “Lazima tufanye maboresho ya kikosi chetu kama kweli tunataka kufanya vizuri kimataifa.

“Wapo wachezaji watakaosajiliwa na kuachwa ambao hivi sasa ni siri yetu, kama tukiwaweka wazi tutashusha morali ya kupambana katika michezo iliyobaki.”

SOMA NA HII  HII HAPA TAARIFA MPYA KUHUSU VYUMA VINGINE VITAKAVYOSHUKA SIMBA....