Home Habari za michezo KUELEKEA MSIMU UJOA….TARAJIA KUKIONA KIFAA HIKI KIKIPIGA KAZI MSIMBAZI…PABLO AMPITISHA …

KUELEKEA MSIMU UJOA….TARAJIA KUKIONA KIFAA HIKI KIKIPIGA KAZI MSIMBAZI…PABLO AMPITISHA …


Simba imerejea jijini Dar es Salaam na juzi ilitarajiwa kuanza kambi kujiandaa na mechi zao za Ligi Kuu Bara na kiporo cha robo fainali ya Kombe la ASFC, huku kocha wa timu hiyo akimpigia hesabu kiungo fundi wa mpira ili amtumie kwa msimu ujao.

Ipo hivi. Mabosi wa Simba wamempa muda wa kutosha kocha huyo afanye tathimini ya kutosha ndani ya kikosi hicho ikiwemo awape mabosi hao orodha ya atakaowatema mwishoni mwa msimu na wale ambao anataka watue Msimbazi.

Tayari kocha huyo ameanza mchakato wake na  miongoni mwa wachezaji wa ndani waliomvutia Pablo kwa aina yake ya uchezaji ni kiungo wa Dodoma Jiji, Cleophace Mkandala anayemaliza mkataba na timu hiyo mwisho wa msimu huu.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zinasema Pablo amelipendekeza jina la Mkandala kwenye orodha ya wachezaji wazawa anaowahitaji msimu ujao katika nafasi ya kiungo mshambuliaji, huku pia kukiwa na orodha na nyota wa kigeni.

Inaelezwa Pablo alimuona Mkandala katika mechi ya duru la pili ya Ligi Kuu, kwani licha ya Simba kushinda mabao 2-0, nyota huyo aliwasumbua wachezaji wa Simba katika eneo la kiungo na kumfanya kocha huyo Mhispania kumtolea macho mwanzo mwisho.

Pablo alipomfuatilia Mkandala aliona muendelezo mzuri wa kiwango bora kwenye mechi nyingine tofauti, licha ya rekodi yake ya kuitungua Simba kwa misimu miwili mfululizo na kuamua kuliandika jina lake akiwataka mabosi wa Msimbazi wambebe.

“Achana na kina Victorien Adebayor, Stephen Aziz Ki na Moses Phiri ambao dili zao zipo sawa hadi sasa, kwa wachezaji wa ndani, jina la kwanza kupendekezwa na Pablo ni Mkandara anayekipiga Dodoma Jiji,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika.

Inafahamika kuwa Mkandala amegoma kuongeza mkataba mpya na Dodoma kutokana na kufanya mazungumzo mara kadhaa na viongozi wa Yanga na Azam ambao nao wanatajwa kumhitaji, lakini hesabu za Pablo ni kuona fundi huyo anatua Msimbazi.

Alipotafutwa Mkandala ili kuzungumza dili hilo, alisema ligi bado ina mechi nyingi na kipindi cha usajili hakijafika hivyo aachwe kwanza na muda sahihi ukiwadia kila kitu kitakuwa wazi juu ya yote ambayo yanazungumzwa.

SOMA NA HII  LIGI YA MABINGWA AFRIKA: SIMBA 1-0 KAIZER CHIEFS

“Bado siku ya mwisho ya kumalizika kwa mkataba wangu na Dodoma Jiji haijafika si vyema kuzungumza mambo ya usajili wakati huu ila mchezaji mzuri yoyote lazima atahusishwa na timu nyingi,” alisema Mkandala na kuongeza;

“Kilichokuwa mbele yangu wakati huu ni kuonyesha kiwango bora zaidi ili kuisaidia timu yangu kumaliza msimu kwenye nafasi nzuri naimani nami nitaonekana kutokana na mchango wangu hapo ndio nitakuwa na maamuzi sahihi.”

Naye Kocha wa Dodoma Jiji, Masoud Djuma alisema Mkandala ni miongoni wa wachezaji wazuri aliyokuwa nao kwenye kikosi chake na anatamani kubaki nae ili aweze kufanya nae kazi kwa muda mrefu.

“Miongoni mwa wachezaji wanaopenda kujituma kwenye mazoezi na mechi muda wote anapambana ili kutimiza majukumu yake, moja ya viungo wazuri niliwahi kuwaona,” alisema Djuma aliyewahi kuifundisha Simba.

Msimu huu Mkandala kwenye Ligi Kuu Bara amefunga bao moja na kutoa pasi za mwisho tatu, huku katika ASFC, amefunga mabao matatu na kutoa pasi za mwisho mbili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here