Home Habari za michezo SIMBA QUEENS WATOA GUNDU MSIMBAZI…WABEBA UBINGWA WA TATU…KAZI IPO KWA TIMU YA...

SIMBA QUEENS WATOA GUNDU MSIMBAZI…WABEBA UBINGWA WA TATU…KAZI IPO KWA TIMU YA WANAUME…


Timu ya Simba Queens imefanikiwa kutetea taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (SWPL) kwa mara ya tatu mfululizo.

Ubingwa huo wa tatu wa Simba Queens umetiki baada ya leo kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mlandizi Queens.

Simba Queens ambayo ilikuwa inatafuta pointi tatu tu katika michezo yake mitatu iliyobaki itangazwe bingwa, imepata ushindi dhidi ya Mlandizi Queens leo ugenini katika uwanja wa Mabatini mkoani Pwani na kufikisha pointi 57 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine huku ikiwa bado na michezo miwili mkononi.

Simba Queens imepata mabao yake kupitia kwa Asha Djafari katika dakika ya 17 ambaye anafikisha mabao 26 msimu huku bao la ushindi likipachikwa dakika ya 56 na Sylivia Mwacha.

Ubingwa huo ni wa tatu mfululizo kwa Simba Jike hao baada ya kuutwaa kwa mara ya kwanza msimu wa mwaka 2019/2020, 2020/2021 na 2021/2022 huku wakiwa na misimu minne tu kwenye ligi hiyo.

Baada ya ushindi wa leo, kupitia ukurasa rasmi wa mtandao wa Instagram wa timu hiyo umeandika “Kazi tumemaliza, Simba tunatetea tena kwa mara ya tatu, Msimbazi mabingwa SWPL 21/22”.

Kwa upande wao Yanga Princess ambao walikuwa wakiusikilizia ubingwa huo kwa karibu wametoa dozi nzito ya mabao 5-1 ugenini mbele ya Ilala Queens.

Katika mchezo huo ambao umepigwa uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam mabao ya Yanga Princess yamepachikwa na Neema Chibara aliyefunga mawili katika dakika ya 2 na 45, Fatuma Mwisendi (30), Olga Tshilombo (37) na Fallone Mwanamundele.

Licha ya kuukosa ubingwa, ushindi huo umewahakikishia Yanga Princess nafasi ya pili wakifikisha pointi 50 na kuwaacha wapinzani wake Fountain Gate Princess katika nafasi ya tatu na alama zao 48.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA ALHAMISI