Home Habari za michezo UKWELI MCHUNGU….KAMA KWELI TIMU ZA LIGI KUU ZINGEKUWA BORA…SIMBA INGEKUWA NAFASI YA...

UKWELI MCHUNGU….KAMA KWELI TIMU ZA LIGI KUU ZINGEKUWA BORA…SIMBA INGEKUWA NAFASI YA 5 AU 6….


MJADALA umeendelea kuwa mkali sana kwenye vituo vya redio, televisheni, mitaani, hasa kwenye vijiwe vya kunywa kahawa, mipira, vituo vya wauza magazeti, mabasi, ndani ya daladala na kwenye mitandao ya kijamii ndiyo balaa.

Ni ule ulioanzishwa na Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally ambaye yeye kama mdau wa soka, alidai kuwa timu zinazocheza Ligi Kuu msimu huu zimekuwa dhaifu kwa sababu nyingi zinapigana ili zisishuke daraja.

Akasema kati ya 16 zinazocheza Ligi Kuu, ni timu mbili tu za Simba na Yanga ndizo haziwezi kushuka, lakini zilizobaki zote 13 kama hazikuchanga karata sawasawa zinaweza kushuka.

Ahmed aliongea kitakwimu zaidi. Na ni kweli, kwani timu ya mwisho hadi ya tatu kuna tofauti ya pointi 11 tu. Timu zimeachana pointi chache sana. Msimu huu kumeonekana kuwa kila timu na ufalme wake.

Yanga inayoongoza ligi imekuwa ikiizidi timu ya pili Simba kwa pointi zisizopungua 10, huku Wekundu wa Msimbazi nao wakiwa kwenye utawala wao, kwani imeizidi Azam FC inayoshika nafasi ya tatu pointi zaidi ya 10. Ila kuanzia ya tatu hadi ya mwisho zenyewe pointi zao zinafuatana.

Akasema ni hatari kuwa na ligi ambayo timu zinashindana kubaki Ligi Kuu na si kushindana kutwaa ubingwa. Hata timu yake akaitaja kuwa ni moja kati ya zilizoonyesha udhafu msimu huu.

Baadhi ya wanamichezo hawakuipokea vizuri kauli hii. Kila mmoja alikuwa na sababu yake na kila mtu alikuwa na hoja yake. Mjadala umeendelea kuwa mkali mno. Jumamosi kwenye safu hii niliandika kuwa, inawezekana Ahmed akawa na hoja, kwani kama kuna timu zinashangilia sare, ujue kuna matatizo.

Nikasema ukitaka kujua timu kwenye Ligi Kuu ni dhaifu, angalia zikicheza na Simba au Yanga, zinakaa nyuma, zinahitaji zaidi sare kuliko ushindi, zikibahatika kupata bao moja, basi ni hilo hilo. Tena zitaanza kupoteza muda.

Ndiyo maana zikipata sare, wachezaji wao wanashangilia na kuzunguka uwanja, unaweza kudhani zimetwaa ubingwa. Timu inayosaka ubingwa haiwezi kushangilia sare dhidi ya Simba au Yanga. Jiulize Simba au Yanga, kufungwa mabao 2-0, 3-0, 3-1, ilikuwa lini?

SOMA NA HII  BAADA YA KUBANJULIWA NA YANGA JUZI....MAKI APUKUTISHA MIKONO SIMBA...ATOA TAHADHARI KWA TIMU ZA LIGI KUU...

Miaka ya nyuma, Simba au Yanga kupigwa idadi hiyo ya mabao ilikuwa ni kitu cha kawaida tu, tena ikiwa na wachezaji bora kabisa wanaochezea mpaka timu za taifa ikiwamo wanaoichezea Taifa Stars.

Zinafungwa na hazikamiwi, ila zinachezewa mpira haswa. Hakuna kupaki basi. Na haikuwa mara ya kwanza mbili au tatu kufungwa na timu mbalimbali kwa idadi kubwa ya mabao. Hii ndiyo unaweza kusema ligi bora na timu zilikuwa bora. Kwa hizi timu zinazoshangilia sare, zikicheza kutaka kusalia Ligi Kuu, badala ya kubishana inafaa tuangalie tatizo ni nini?

Naendeleza tena mjadala huu kwa kutoa hoja nyingine. Msimu uliopita, mastraika watatu wa Simba, Meddie Kagere, Chris Mugalu na John Bocco walifunga jumla ya mabao 44. Leo hii mastraika hao wote wana mabao saba tu, na yote amefunga Kagere.

Lakini eti bado Simba ipo kwenye nafasi ya pili. Tena kwa zaidi ya pointi 10. Kwa ligi yoyote bora, yenye timu bora, haiwezekani timu iwe na mastraika ambao mpaka timu inaelekea ukingoni hawajafunga hata bao moja, iwe ya pili, ikizipita timu zingine kwa mbali sana.

Mabao ya Simba kwa sasa yanafungwa na viungo tu. Nilitegemea udhaifu, ungetumiwa na timu zingine kuitupa chini kabisa ya msimamo kwenye nafasi ya nne mpaka ya sita.

Inawezekana tatizo linaanzia mbali sana. Huenda nchi kwa sasa haina wachezaji wenye viwango bora kama wale wa zamani, au wachezaji washindani, wapambanaji.

Au aina ya mafunzo wanayoyapata hayakidhi, na labda hawapati mazoezi ya kutosha ya fiziki mwanzoni mwa msimu.

Au huduma za baadhi ya timu kwa wachezaji wao, kama vile mishahara, chakula, posho, usafiri ni duni ukilinganisha na timu zingine, ndiyo maana inakuwa hivyo.

Mfano, Simba na Yanga zinasafiri kwa ndege mikoani, zingine zinakwenda kwa basi.

Hapo nadhani ndiyo hoja ianzie na mjadala ujikite hapo, badala ya kubishana na takwimu na ukweli ulivyo.

Unawezaje kusema ligi na timu ni bora, wakati kama Yanga isingekuwapo kwenye ligi, Simba hii ambayo mastraika wake kufunga ni tatizo ingekuwa bingwa? Nahitimisha mjadala.

Credit: Nipashe