Wakati Yanga wakiamua kuifanya kambi yao ya maandalizi ya msimu ujao hapa Dar esSalaam, timu ya Dodoma Jiji imeanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu na leo Julai 21 imeenda jijini Arusha kuweka kambi huku ikiachana na wachezaji 13 akiwemo Khamis Mcha ‘Vialli’ na Issa Abushehe.
Timu hiyo ilianza mazoezi jana na leo imeendelea nayo katika uwanja wa Jamhuri jijini hapa ambapo wachezaji kadhaa wapya na wale wa zamani walionekana.
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Mosses Mpunga amesema sababu ya kuweka kambi Jijini Arusha ni kutokana na jiji hilo kuwa na mazingira ya utulivu.
Mpunga amesema Arusha watakaa kwa siku kadhaa na kisha wataelekea sehemu nyingine ambayo bado uongozi haijaitaja kwa ajili ya kuendeleza kambi hiyo.
Wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo na walionekana mazoezi ni pamoja Randy Bangala (TP Les Croyant) Amani Kyata,Rashid Chambo (Coastal Union) Jimmy Shoji (Mbeya Kwanza) na Hassan Mwaterema (Kagera Sugar)
Wachezaji wa zamani walionekana mazoezini ni pamoja na nahodha,Mbwana Kibacha,Rajabu Mgalula,Augustino Nsata,Salmin Hoza,Emmanuel Martin,Joram Mgeveke,Seif Karihe na enrick Nkosi.
Mazoezi hayo yalisimamiwa na Kocha Masoud Djuma na msaidizi wake Mohammed Muya.
Mcha Abushehe watupiwa virago
Katika hatua nyingine inadaiwa uongozi wa klabu hiyo umewaacha baadhi ya wachezaji akiwemo Issa Abushehe na Khamis Mcha.
Mcha ambaye ameitumikia klabu hiyo kwa miaka minne alikuwa nahodha msaidizi kwenye kikosi hicho na msimu uliopita aliifungia mabao matano huku matatu akifunga kwa njia ya penalti.
Aliyeongoza ufungaji katika kikosi cha timu hiyo ni Anuary Jabir aliyefunga mabao saba huku Mcha akishika nafasi ya pili kwa mabao yake matano.
Abushehe ambaye ameifungia bao moja timu hiyo alijiunga dirisha dogo la usajili akitokea Coastal Union ya Tanga na alikosa mechi saba za mwisho kutokana na kuumia.
Uongozi wa timu hiyo bado haujaweka wazi majina ya wachezaji iliyowaacha lakini Mwansporti inajua wachezaji hao wametupiwa virago kwani kwenye mazoezi ya jana na leo hawakuonekana.
Wachezaji wengine ambao hawakuonekana mazoezini ni pamoja na Justin Mganga Daga Chenko,Omary Kanyoro,Makipa Yusuphu Mohammed Rahim Sheike na Hussein Msalanga ambaye inadaiwa tayari amejiunga na Ruvu Shooting.
Alipotafutwa Mcha amesema yupo safarini hawezi kuzungumza kitu chochote.
Kwa upande wake Abushehe amesema tayari ameachana na timu hiyo na jana aliwaaga viongozi,benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo.