Uongozi wa AFC Leopards umefanikiwa kumaliza kumlipa malimbikizo ya madeni ya mishahara wake wa msimu uliopita kocha wao, Patrick Aussems, na sasa anatarajiwa kutua leo jijini Nairobi.
Juzi kati, Aussems alifunguka kwa njia ya simu kuwa atarejea kuinoa kikosi hicho endapo tu uongozi utamlipa madeni yake akitishia kusepa akidai kupokea ofa kibao tena tamu zaidi kutoka klabu zinginezo.
Aussems aliondoka nchini Juni mwaka huu ikiwa ni wiki mbili kabla ya msimu 2021/22 kufika tamati na kurejea kwao Ubelgiji kwa ajili ya likizo.
Alitarajiwa kurejea nchini Agosti 12 mwaka huu, lakini siku zikapita bila yeye kutua. Aussems alifichua sababu zake za kudinda kurejea ilitokana na bodi ya Ingwe kuchelewa kutimiza ahadi yao ya kumlipa madeni yake yote.
Hilo sasa limekamilika na Aussems amedhibitisha kuwa anajiandaa kurejea kwenye kibarua chake.
Jumanne aliposti picha ya pasipoti yake na mabegi na kuziambatanisha na ujumbe wa kurejea kwake.
“Nairobi naja. Nina hamu kubwa ya kurejea uwanjani, kuendelea kufanya kazi na wachezaji wangu na pia kuwaona mashabiki wa Ingwe ambao wamekuwa wakitusapoti sana,” Aussems alitwiti.
Ingawaje hakubainisha tarehe atakayowasili nchini, kuna taarifa kuwa kocha huyo alitarajiwa kuwasili jana.
“Kocha wetu anawasili Alhamisi Agosti 26. Tulilazimika kubadilisha tarehe ya usafiri wake alipotuomba tufanye hivyo kutokana na hali tete iliyokuwepo kipindi cha uchaguzi mkuu.” ametufahamisha Katibu Mkuu wa Ingwe, Gilbert Andugu.
Aussems atarajea kipindi Ingwe ikiwa na mdhamini mpya anaewajeng zaidi ya Sh50 milioni kila mwaka. Ni udhamini ambao umeiwezesha klabu kuhakikisha wachezaji wao hawaondoki kama ilivyoshuhudiwa katika misimu miwili iliyopita.