Home Habari za michezo BAADA YA KUCHEZA MECHI MBILI ZA LIGI NA KUSHINDA KWA MBINDE…BOSI YANGA...

BAADA YA KUCHEZA MECHI MBILI ZA LIGI NA KUSHINDA KWA MBINDE…BOSI YANGA AIBUKA NA KUTAJA MECHI NGUMU ZIJAZO…


Uongozi wa Klabu ya Yanga umeweka wazi mikakati yao kuelekea michezo minne iliyopo mbele yao ikiwamo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara na idadi kama hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo inatarajiwa kuchezwa Septemba 10, mwaka huu.

Mkurugenzi wa mashindano wa Klabu ya Yanga, Saad Kawemba, alisema kikosi chao kinaendelea na mazoezi kujiandaa na michezo minne ambayo alidai ni migumu na yenye ushindani mkubwa ndani ya siku 11.

Alisema kati ya mechi hizo mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara, watacheza dhidi ya Azam FC na Mtibwa Sugar Septemba 6 na 13, mwaka huu, mechi ambazo alidai ni ngumu kupata ushindi.

“Tunahitaji kupata matokeo mazuri katika michezo hiyo miwili, lakini tuna mechi mbili za kimataifa dhidi ya Zalan FC, ambazo tutacheza Septemba 10 na 17 mwaka huu, tutarudiana.

“Katika michezo yote, tunahitaji kushinda, ikiwamo michuano ya kimataifa kwa akili ya kufikia malengo yetu ya kucheza hatua ya makundi,” alisema Kawemba.

Alisema wana matarajio makubwa ya kufanya vizuri katika michezo ijayo ikiwamo ya kimataifa kwa sababu malengo yao makubwa ni kuona timu hiyo inafanya vizuri na kucheza hatua ya makundi.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, alisema hakupata maandalizi mazuri ya msimu mpya kabla ya ligi kuanza, hivyo anatumia kipindi hiki kukiandaa kikosi chake.

“Nataka kutumia hizi siku kufanya mazoezi ya nguvu ili ifidie zile siku tulizokosa ‘preseason’, hivyo hatutakuwa na mchezo wa kirafiki,” alisema Nabi.

Alisema baada ya juzi kuanza mazoezi ya ‘gym’, jana kikosi chake kimeanza mazoezi ya uwanjani akiwa na lengo la kutengeneza muunganiko ambao anautaka.

“Tumecheza michezo miwili ya ligi licha ya kushinda mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania na 2-0 dhidi ya Coastal Union, bado sijaridhishwa na muunganiko wa timu yangu,” alisema.

Naye kiungo mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison, alisema kulingana na ratiba iliyopo mbele yao, wamelazimika kukatisha mapumziko yao na kuendelea na maandalizi ya michezo iliyopo mbele yao ukiwamo dhidi ya Azam FC.

SOMA NA HII  SALAMA JABIR AACHA KAZI EATV...ATAJWA KUWA NDIYE MSEMAJI MPYA SIMBA SC

Alisema mechi zilizopo mbele yao hasa mchezo dhidi ya Azam FC ni muhimu kupambana kupata matokeo mazuri ili kufikia malengo yao ya kukusanya pointi kila mechi.

“Tumekatisha mapumziko kwa ajili ya kurejea mazoezini kujiandaa na michezo iliyopo mbele yetu ikiwamo dhidi ya Azam FC, mchezo utakuwa wa ushindani mkubwa kwa sababu ya kila timu kutafuta matokeo,” alisema Morrison.