Home Habari za michezo HIZI HAPA SIKU 54 ZA JASHO, DAMU NA MAKASIRIKO KWA SIMBA NA...

HIZI HAPA SIKU 54 ZA JASHO, DAMU NA MAKASIRIKO KWA SIMBA NA YANGA…BINGWA WA LIGI KUJULIKANA NDANI YA SIKU HIZI…


WATANI wa jadi, Simba na Yanga zinachuana kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa sasa kila moja ikiwa na pointi sita sawa na ilizonazo pia Singida Bis Stars na kutenganishwa kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa tu.

Simba ipo juu ya Yanga kutokana na kufunga mabao matano katika mechi zao mbili, huku Yanga ikiwa na mabao manne, lakini ikiruhusu mabao mawili, ilihali Singida inawafuata nyuma na mabao yake matatu na kufungwa moja.

Timu hizo sambamba na Azam zote zinapigiwa chapuo kwenye mbio za ubingwa, lakini ligi ikiwa imesimama, wababe hao watakabiliwa na siku 54 ngumu na zitawaweka nyota wake katika kibarua kigumu cha kuweza kudhihirisha ukubwa wa majina yao.

Yanga inayowategemea nyota wake Stephane Aziz KI, Fiston Mayele na Bernard Morrison itakuwa na kibarua kizito ligi itakaporejea tena mapema mwezi ujao, kama Clatous Chama, Pape Ousmane Sakho na Augustine Okrah watakavyotaitiwa na siku hizo 54.

Ipo hivi. Siku hizo 54 za jasho na damu kwa vigogo hivyo vitatu ni kile kinachoanzia Septemba 6 hadi Oktoba 30, kila moja itakabiliwa na utitiri wa mechi za Ligi Kuu na zile za michuano ya kimataifa zitakazochezwa ndani ya kipindi kifupi kutoka mchezo mmoja hadi mwingine. Kwa mujibu wa ratiba iliyo mbele ya timu hizo, kila moja itakuwa na muda wa kupumzika usiozidi siku tano kutoka mechi moja hadi nyingine, ambao pia unaweza kupungua kutokana na uwepo wa mechi za kimataifa zitakazocheza ugenini nje ya Tanzania.

Katika kipindi cha kuanzia Septemba 6 hadi Oktoba 30, ratiba inaonyesha Simba na Yanga kila moja itakuwa na michezo 12 iwapo zitatinga katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ikiwa kila moja itacheza mechi 12 ndani ya siku hizo 54, muda wa maandalizi ya kitimu pamoja na kusafiri kutoka kituo kimoja hadi kingine kama watalazimika kufanya hivyo, utakuwa ni siku 45.

Kana kwamba haitoshi, ndani ya muda huo, timu hizo kila moja itakuwa na mechi ngumu itakayozikutanisha zenyewe katika ligi, pia zitaumana na Azam katika nyakati tofauti.

Yanga itaanza kibarua chake, Septemba 6 kwa kuivaa Azam na baada ya hapo, siku tatu baadaye itakabiliana na Zalan ya Sudan Kusini kisha Septemba 13 itacheza na Mtibwa Sugar nyumbani ikifuatiwa na mchezo wa marudiano dhidi ya Zalan, Septemba 16.

SOMA NA HII  KISA KIWANGO KIBOVU....MAGUIRE APEWA SAA 72 ZA KUSEPA MAN UNITED....WAKALA WAKE APEWA BARUA...

Baada ya hapo itasafiri kwenda Mbeya kuikabili Ihefu, Septemba 29, Oktoba 3 itacheza na Ruvu Shooting na kama itaitupa nje Zalan, itakuwa na mechi mbili za nyumbani na ugenini za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mechi ya kwanza itachezwa kati ya Oktoba 7 hadi 9 na marudiano Oktoba 14 hadi 16.

Ikumbukwe Ligi Kuu, Oktoba 13, Yanga itakutana na Namungo na Oktoba 23 itakuwa na mechi ya watani wa jadi dhidi ya Simba na mechi mbili za kumalizia ni dhidi ya KMC, Oktoba 26 na Oktoba 29 itacheza na Geita Gold. Kwa upande wa Simba, Septemba 7 itacheza na KMC, kabla ya Septemba 9 kucheza ugenini nchini Malawi dhidi ya Nyasa Big Bullets, kisha itaifuata Tanzania Prisons ugenini mechi ya Septemba 14 na Septemba 16 watarudiana na Nyasa Big Bullets.

Baada ya hapo watacheza na Mbeya City ugenini siku ya Septemba 28 na Oktoba 2 itakabiliana na Dodoma Jiji na iwapo itatinga raundi ya pili, kati ya Oktoba 7 hadi 9 itakuwa na mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Oktoba 12 itakuwa ugenini kukabiliana na Singida Big Stars ambao licha ya ugeni wao wameonekana kuwa moto ikishusha mastaa kutoka Latini Amerika.

Kati ya Oktoba 14 na 16, kutakuwa na mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kisha itaivaa Yanga, Oktoba 23 na mechi zake mbili zitakazobakia ndani ya siku 54 ni dhidi ya Azam FC, Oktoba 27 na Oktoba 30 itacheza na Mtibwa Sugar.

Kocha wa Simba, Zoran Maki alisema kuwa kikosi chake kipo tayari kukabiliana na ratiba iliyo mbele yao, licha ya kuwa ngumu lakini hawana namna ila kujipanga na kwenda nayo sambamba akisaka matokeo mazuri yatakayowabeba katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa.

“Ratiba imeshapangwa na tunachotakiwa ni kuhakikisha tunapata ushindi katika mechi zilizo mbele yetu ili tuweze kufikia malengo yetu. Ushindani ni mkubwa lakini nafuarahi kuona timu yangu inazidi kuimarika,” alisema Maki, huku Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema hawako tayari kuruhusu changamoto ya ratiba kuvuruga mipango yao.

“Ushindani ni mkubwa na kila mechi ni ngumu lakini pia ratiba itabana lakini nina kikosi kizuri chenye wachezaji wengi wazuri ambao wanaweza kutuwezesha kuimudu vyema,” alisema Nabi.