Home Habari za michezo HUKU TETESI ZA KUTEMWA ZIKIZIDI KUSAMBAA…HUYU HAPA AKPAN..AFUNGUKA A-Z KUHUSU SIMBA NA...

HUKU TETESI ZA KUTEMWA ZIKIZIDI KUSAMBAA…HUYU HAPA AKPAN..AFUNGUKA A-Z KUHUSU SIMBA NA MAMBO YALIVYO…


Dirisha kubwa la usajili msimu huu miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa kwa mvutano alikuwa kiungo wa Simba, Victor Akpan baada ya kuonyesha kiwango bora msimu uliopita akiwa Coastal Union.

Usajili wake ulikuwa wa kuvutana kutokana na awali matajiri wa Ligi Kuu Bara, Azam walikuwa wa kwanza kumtaka baada ya kuonyesha kiwango bora katika fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga.

Azam ilikuwa ya kwanza kumchukua Akpan katika kambi ya Coastal iliyokuwa kwenye moja ya hoteli Dar es Salaam akiwa katika maandalizi ya kwenda Lindi kucheza na Namungo, mwishoni mwa msimu uliopita.

Baada ya mvutano wa kimaslahi na Azam hadi kufika usiku mwingi, walishindwa kukubaliana na Simba kumchukua juu kwa juu kwenda kumsainisha mkataba wa miaka miwili alioanza kuutumikia hivi sasa.

“Nakumbuka kabla ya kukubali kujiunga na Simba wakala wangu alikuwa na ofa nyingine nje ya nchi na yalikuwepo mazungumzo tayari, ila ofa ya hapa ilikuwa kubwa na bora zaidi ya Azam na hiyo nje ya nchi,” anasema Akpan.

Makala haya inakuletea mahojiano maalumu na Akpan yaliyofanyika katika Hoteli ya Mercure iliyopo Ismailia, Misri wakati huo Simba ikiwa kambini kujiandaa na msimu.

SOKA ALIPOANZIA

Akpan anasema alianzia soka la vijana mitaani nchini kwao Nigeria na akaenda kwenye akademi mbalimbali, lakini baada ya hapo alipata timu ya Ligi Daraja La Kwanza, City Stars, ambayo alianza kucheza soka la ushindani.

Anasema alicheza timu nyingine za madaraja ya chini kama la nne na tatu, kisha akapata nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya Nigeria msimu mmoja, lakini baadaye akaamua kuja Tanzania.

“Nyumbani niliondoka kutokana na kutoona mafanikio kama vile ambavyo nilihitaji, ila niliamini nikitoka kutokana na kiwango changu kilivyo. Nashukuru naishi katika ndoto zangu, ingawa sijafika kwenye kiwango ambacho nahitaji,” anasema.

SIMBA YAMKATAA

Akpan anasema 2018 alipotua Tanzania mara ya kwanza klabu ya kwanza kufanya majaribio ilikuwa Simba wakati huo inafundishwa Masoud Djuma, lakini hakuonekana kumvutia.

Anasema awali, aliyekuwa kocha wa Wekundu hao, Patrick Aussems aliamini alikuwa na kiwango bora na ndio maana alifanya mazoezi hadi mwisho, lakini kutokana na wachezaji wa kigeni kuwa wengi alishindwa kusajiliwa.

“Baada ya kushindwa niliamua kwenda Zanzibar na nilipata timu ya JKU wakati huo dirisha lilikuwa bado halijafungwa nikacheza kwa nusu msimu,” anasema

“Nikiwa hapo JKU kuna timu ya Ligi Kuu Oman iliniona na dirisha dogo ilinisajili nikaenda kucheza kwa msimu mmoja, lakini likaibuka janga la Uviko -19, ligi ilisimama nikaamua kurudi zangu Tanzania.”

KURUDI TANZANIA

Akpan anasema hakutaka kurudi Nigeria baada ya mipango yake Oman kushindikana, alirudi Tanzania na bahati nzuri alikutana na ofa nyingine zaidi ya tatu.

Anasema miongoni mwa timu iliyoonyesha nia ya kumhitaji ni Namungo na Geita Gold, lakini aliamua kwenda Coastal Union kutokana na ukaribu wake na kocha Juma Mgunda.

“Nakumbuka wakati narejea nilikutana na Mwenyekiti wa Coastal, Steven Mnguto ambaye alinieleza mipango ya timu. Nilijikuta nakubali na kuamini kucheza, nikaachana na ofa za timu nyingine,” anasema Akpan.

NDANI YA COASTAL

Akpan anasema alicheza msimu mmoja ambao ulikuwa mgumu kutokana na ushindani wa ligi.

“Kuna nyakati msimu uliopita tulipambana kwelikweli na kuna nyakati tulishika hadi nafasi ya tatu, kuna muda tulishushwa chini zaidi ya nafasi ya kumi kutokana na ushindani,” anasema.

“Kujituma kwangu na kutaka Coastal isiwe timu ya chini kwenye msimamo wa ligi ikiwemo kucheza mechi za playoff kama msimu mmoja nyuma pengine ndio ilikuwa sababu ya kufanikiwa kwangu.”

SIMBA, YANGA

Miongoni mwa mechi ambazo Akpan msimu uliopita alicheza vizuri katika kiwango bora ni dhidi ya Simba ikiwemo kufunga bao na tatu dhidi ya Yanga – mbili za ligi na fainali ya ASFC.

Akpan anasema anapenda ushindani kucheza na timu kubwa ndio maana alipokutana na wachezaji wa timu hizo aliwapa changamoto.

“Niliamini mechi hizo ndizo kubwa na zinatafuatiliwa na watu wengi nchini. Kwa hiyo nilitaka kuonyesha nina uwezo wa kucheza katika kiwango bora dhidi ya wachezaji kutoka timu kubwa licha ya kutoka Nigeria kuja kutafuta maisha timu ndogo.

SOMA NA HII  MAJANGA HAFIZ KONKANI AGOMA KUVAA VIATU VYA MAYELE, ISHU IKO HIVI

“Naamini hilo lilinisaidia kuonekana na pengine hadi timu kufanikiwa kucheza katika kiwango bora kwenye michezo yote dhidi ya Simba, Yanga na Azam.”

BAO DHIDI YA SIMBA

Kwenye mechi ya mzunguko wa pili msimu uliopita Simba dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Akpan alifunga bao moja katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Anasema nafasi anayocheza ni kiungo mkabaji, lakini kuna wakati Mgunda alimruhusu kusogea katika eneo la kushambulia kama ilivyokuwa wakati analipofunga bao hilo kwani wachezaji wa Simba hawakuwa katika eneo sahihi.

“Wakati napokea pasi kwa Simon Gustavo nilimuona Aishi Manula hakuwa katika eneo sahihi na kupiga mpira kule alipokuwa ameacha nafasi, nashukuru nilifunga bao muhimu kwa timu,” anasema.

“Lilikuwa moja ya matukio yenye furaha kwangu na timu kwani sio rahisi kuwafunga Simba – tena wakati huo walikuwa hawana matokeo mazuri mfululizo pamoja na uwepo wa nyota wengi bora.”

MIAKA MIWILI SIMBA

Akpan anasema miaka miwili aliyosaini kuitumikia Simba anaamini mashabiki wanataka matokeo mazuri ili kutwaa mataji tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.

Anasema msimu uliopita haukuwa mzuri kwa Simba na sasa watalazimika kuishi kwa presha kutoka kwa mashabiki wanaotaka matokeo mazuri.

“Nimeliweka hilo katika akili yangu tangu najiunga na Simba kuwa kutakuwa na presha kubwa, ila naamini nikipata nafasi ya kucheza nitafanya zaidi ya kile ambacho benchi la ufundi litakuwa likitegemea kutoka kwangu,” anasema.

“Simba kuna wachezaji wengi bora – waliokuwepo msimu uliopita nasi wapya. Natambua kutakuwa na ushindani mkubwa kuwania kucheza katika kila nafasi.

“Nataka kutoa mchango wa kutosha kwa timu ili kufanya vizuri katika mashindano ya ndani pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika ili kupata mafanikio tofauti na msimu uliopita.

“Mara zote naamini mchezaji mzuri lazima atakutana na changamoto. Kwenye nafasi ambayo nacheza kuna Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Erasto Nyoni na Sadio Kanoute ila ikitokea nimepata nafasi nitajitahidi kuonyesha kiwango bora.”

FAINALI NA YANGA

Akpan anasema katika historia ya kucheza soka hataisahau fainali ASFC kati ya Yanga dhidi ya Coastal Union ambayo walipoteza licha ya kucheza vizuri.

Anasema mechi hiyo ilimuumiza kwa kuwa ilikuwa ya mwisho kwake kuichezea Coastal Union na waliamini wanakwenda kutengeneza historia kubwa ya kwenda kuishangaza Yanga kwa kuifunga na kuchukua taji.

“Ubora wa kikosi chetu wakati ule, maandalizi tuliyofanya na ushirikiano tuliopata kutoka kwa mashabiki pamoja na viongozi niliamini tunawashangaza Yanga kwa kuwafunga,” anasema Akpan.

“Haikuwa siku yetu na Mungu hakupenda kwani tulikuwa bora zaidi ya Yanga, ila tulijikuta tunafanya kosa moja la kiulinzi dakika za mwisho na kuruhusu bao ambalo lilikuwa la kusawazisha. Siwezi kusahau tukio hilo.”

VIUNGO WAMVUTIA

Akpan anasema katika ligi kuna baadhi ya viungo kutoka timu pinzani na Simba ambao anawakubali kutokana na aina ya uchezaji kama Feisal Salum ambaye ni mshikaji wake nje ya maisha ya soka.

“Wapo wengi namkubali Mkude, Salum Abubakar, Gustavu, Kelvin Nashon na Mudathir Yahya. Nawaelewa kwenye viwango vyao pamoja na ubora ambao wamekuwa wakionyesha muda wote uwanjani,” anasema Akpan.

“Sio rahisi mchezaji kucheza katika kiwango bora muda wote, ila kwa hao ambao nimewataja wanacheza katika ubora.”

MABINGWA AFRIKA

Simba miongoni mwa malengo ya muda mrefu iliyojiwekea ni kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwemo kuchukua taji hilo ambalo wanalisaka kipindi kirefu.

Akpan anasema kutokana na usajili uliofanywa wachezaji waliokuwepo msimu uliopita, uimara wa benchi la ufundi na nguvu kutoka kwa mashabiki msimu huu watafanya vizuri katika mashindano hayo makubwa kwa ngazi ya klabu.

“Tunakwenda kucheza mashindano yenye ubora wa wachezaji hadi maeneo mengine, ila naamini maandalizi yetu na kiu ya mafanikio tutacheza kwa ubora na kufanya vizuri pengine zaidi ya msimu uliopita,” anasema.

MWALIMU KISWAHILI

Akpan anasema anapokuwa kambini muda mwingi anaishi na Augustine Okrah, nyota mpya aliyesajiliwa Simba akitokea Ghana na mbali na maisha yao mengine huwa anafanya kazi ya kumfundisha Kiswahili ili aelewe kwa haraka.