Home Habari za michezo KISA KUFUNGA GOLI JUZI…DEJAN AENDELEA ‘KUPASUKA’ MAPYA SIMBA…AFUNGUKA NAMNA ANAVYOCHEZA NA WENZAKE...

KISA KUFUNGA GOLI JUZI…DEJAN AENDELEA ‘KUPASUKA’ MAPYA SIMBA…AFUNGUKA NAMNA ANAVYOCHEZA NA WENZAKE UWANJANI…


Wale waliokuwa wakimponda Dejan Georgijevic, straika mpya wa Simba kutoka Serbia ghafla wamepata ubaridi baada ya jamaa kutupia bao tamu la kideoni na kusahau kila kitu juu yake, sasa mwenyewe amevunja ukimya na kutamba; ‘Na bado nitafunga sana, kwani nakiamini kipaji changu’.

Dejan aliyesajiliwa hivi karibuni alifunga bao la pili la Simba katika dakika ya 81 baada ya kuwahadaa mabeki wa Kagera Sugar kabla ya kutumia nyavuni kwa guu la shoto na kuwapagawisha mashabiki wa Simba waliosahau kejeli walizokuwa wakizitoa juu yake na kumshangilia.

Katika mahojiano mafupi na straika huyo jana na kufunguka, amejisikia faraja kufungua akaunti ya mabao klabuni hapo, lakini anakiri alikuwa kwenye presha kubwa kutoka kwa mashabiki ndani na nje ya uwanja.

Dejan alisema tangu ametambulishwa Simba amekuwa akipokea jumbe nyingi za lugha ya kiswahili katika mtandao wake wa (Instagram) tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Alisema kuna nyakati alipata muda alikuwa anachukua baadhi ya ujumbe kutafsiri kwa lugha yake na kueleza mashabiki wengi wa Simba wanatamani kumuona anafanya vizuri na kufunga mabao katika mechi mfululizo.

“Jambo lingine mara zote nikiwa uwanjani pindi ninapokuwa na mpira, nikiwa napasha ili kuingia au kufanya tendo lolote mashabiki wa Simba wamekuwa wakishangilia kutokana na tukio hilo,” alisema Dejan na kuongeza;

“Baada ya kuona yote haya niliamini nina deni kubwa natakiwa kulilipa kwao ili wafurahi kama walivyo na imani nami, nashukuru kwa hilo nimefanikiwa na utakuwa muendelezo katika michezo ijayo.

“Nilikuwa natamani kufunga ili kutengeneza hali ya kujiamini na morali kuongezeka kwangu, kwani naamini katika ubora wangu ninao uwezo wa kufunga mfululizo ila kutokana na mazingira ya ugeni lazima nikubali kukabiliana nao.”

Straika huyo aliyewahi kukipiga Partizan, Spartal na NK Domzale, aliongeza; “Nimefurahi kufunga bao langu la kwanza la msimu kwenye mechi za kimashindano, naamini nitafunga zaidi, nimefurahi timu yangu kupata ushindi.”

Dejan alisema hadi amefanya maamuzi ya kuja kucheza Afrika katika klabu ya Simba alifanya uchunguzi wa kutosha na kuamini anaweza kufanya vizuri kufunga mabao mengi kama alipotokea.

SOMA NA HII  KISA NEMBO YA MDHAMINI WA LIGI KUU NBC...BODI LA LIGI KUZISHUSA DARAJA TIMU ZA LIGI KUU

Dejan alisema lazima akubali kushindana na changamoto ya ugeni katika timu, ligi na mambo mengine na itamchukua muda mfupi kuzoea vyote hivyo ili kufanya vizuri kama ambavyo malengo yake yalivyo.

Alisema kabla ya kufunga bao hilo alikuwa akishirikiana vizuri na wachezaji wenzake tangu mazoezi na kuna nyakati walikuwa wakishauriana jambo gani la kufanya ili kuwazidi mabeki na kufunga.

“Ndio maana unaona baada ya kufunga lile bao wachezaji wenzangu wote waliokuwa uwanjani na hata benchi walifurahi kama ilivyokuwa kwa upande wangu ni mwanzo mzuri kwangu naamini naenda kufunga mabao mengi zaidi msimu huu,” alisema Dejan na kuongeza; “Benchi la ufundi limekuwa likinitengeneza kiakili ili kuachana na presha kubwa dhidi yangu na kuniambia natakiwa kuwa mtulivu nitafunga hatimaye hilo limesaidia na nimekwenda kutimiza lengo.”

ZORAN MAKI

Kocha wa Simba, Zoran Maki alisema Dejan ni moja ya mastraika wazuri wenye uwezo wa kufunga, anaweza kuwa eneo sahihi wakati timu inafanya mashambulizi, anawasumbua mabeki wa timu pinzani pamoja na mengine.

Zoran alisema ni suala la muda Dejan atakuwa anafunga mfululizo baada ya kuzoea ligi, mazingira, viwanja, wachezaji wenzake pamoja na kupata muda wa kutosha kufanya mazoezi.

“Dejan anaweza kuwa na sifa zote ila bila ya kufunga ni kazi bure kwa maana hiyo baada ya kufunga itaongeza hali na morali ya kushindana kwake na kutamani kufanya hivyo zaidi katika mechi zijazo,” alisema Zoran.