Home Habari za michezo KUHUSU MICHUANO YA CAF…ALEX SONG AIPIGIA ‘UPATU’ SIMBA…AFUNGUKA MATAMANIO YAKE YA MOYONI…..

KUHUSU MICHUANO YA CAF…ALEX SONG AIPIGIA ‘UPATU’ SIMBA…AFUNGUKA MATAMANIO YAKE YA MOYONI…..


KIUNGO mkabaji wa Klabu ya AS Arta/Solar 7 ya Djibouti, Mcameroon Alex Song, amesema kikosi cha Simba kinaundwa na wachezaji wengi wenye vipaji na kwamba kama watakuwa wanajituma zaidi muda utaongea kabla ya kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa katika klabu kubwa za nje.

Song aliyewahi kuzichezea klabu mbalimbali barani Ulaya zikiwamo Arsenal na Barcelona, kwa sasa anakitumikia kikosi cha timu ya As Arta/Solar 7 ambacho kipo hapa Dar es Salaam kikijiandaa na msimu mpya hususan Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo kitakutana na Al Merrikh ya Sudan katika hatua ya awali ya michuano hiyo.

AS Arta/Solar 7 inatarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Simba Septemba 3, mwaka huu, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Song alisema halifahamu vizuri soka la Tanzania ila alikuwapo katika Kilele cha Simba Day na kuona jinsi Watanzania wanavyopenda soka na timu yao.

Alisema kuhusu wachezaji wa Simba aliowaona siku hiyo wakati wakicheza mechi ya kirafiki dhidi ya St. George ya Ethiopia, alisema ni wazuri na anaamini wengi wao wana nafasi ya kucheza soka nje ya Afrika na kwamba kikubwa wanatakiwa kupambana na kujituma.

“Sijawahi kulifuatilia soka la Tanzania, sherehe za Simba nilifanikiwa kushuhudia mechi yao ya kirafiki dhidi ya St. George ya Ethiopia, kilichonivutia ni kuona mashabiki wengi kujitokeza na kujaza uwanja, hii ni ishara ya Watanzania kupenda cha kwao, lakini nimeona wachezaji wazuri na wakijituma zaidi watapata nafasi ya kucheza soka nje ya Afrika.

“Nina imani kufika kwetu kucheza soka Ulaya kunachangiwa na kuwasikiliza waliotuzidi, kuwa makini, kujituma, kufuata yale tunayopewa na kocha pamoja na kuhakikisha unathamini ile nembo ya jezi unayotumikia, ndiyo sababu kubwa ambayo imetufanya kufanikiwa na kucheza klabu mbalimbali Ulaya,” alisema Song.

Kuhusu kurejea Afrika na kucheza ndani ya kikosi cha timu hiyo inayoshiriki  Ligi Kuu ya Djibouti, alisema ni kwa sababu ya kutaka kuendelea kuacha uzoefu na kutoa somo kwa baadhi ya wachezaji vijana ili kufikia malengo yao.

SOMA NA HII  KAMA ULIKUWA HUJUI...HIZI HAPA SABABU ZA NDAANI KABISA ZA MORRISON KUSAINI YANGA JANA...

“Huku ukanda wetu wa Afrika ni nchi chache sana ambazo wachezaji wanatoka katika kituo cha soka, wengi wao hawana misingi ya soka kuanzia chini sasa kuwapo kwangu hapa katika Klabu ya AS Arta Solar ni kutoa somo kwa vijana na kuwaeleza ni namna gani ya kufikia malengo yao ya kucheza soka kama ilivyo kwangu,” alisema Song ambaye katika klabu hiyo yupo na nyota wa zamani wa Chelsea, raia wa Ivory Coast, Solomon Kalou.