Home Habari za michezo SIKU TATU KABLA YA DIRISHA LA USAJILI KUFUNGWA…ISHU YA ONYANGO BADO PASUA...

SIKU TATU KABLA YA DIRISHA LA USAJILI KUFUNGWA…ISHU YA ONYANGO BADO PASUA KICHWA SIMBA…YANGA WAFUNGA FAILI…


Wakati timu nyingi za Ligi Kuu Tanzania Bara zikiwa zimekamilisha usajili wao, siku tatu zilizobakia zinaweza kubadili uamuzi kwa baadhi ya timu hizo kutokana na kile zilichokivuna au kukionyesha katika mechi mbili za mwanzo.

Dirisha kubwa la usajili litafungwa Jumatano, Agosti 31, saa 5:59 usiku na baada ya hapo timu hazitoruhusiwa kufanya usajili hadi dirisha dogo litakapofunguliwa Desemba.

Hata hivyo, pamoja na timu nyingi kuonekana kumaliza usajili, huenda siku nne zilizosalia zikaja na uamuzi wa tofauti na kupunguza baadhi ya wachezaji au kuongeza wengine.

Mwanzo mzuri wa Simba, Yanga, Singida Big Stars, Azam FC na Namungo FC unatoa ishara kuwa kuna uwezekano finyu kwa timu hizo kufanya usajili katika muda mfupi uliobaki.

Hata hivyo, taarifa za beki wa Simba, Joash Onyango kushinikiza kuachwa kutokana na kutofurahishwa na kutokuwa chaguo la kwanza la kocha Zoran Minojlovic zinaacha swali juu ya uwezekano wa Simba kukubali kumuacha au la.

Awali, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa hawatoongeza wala kupunguza mchezaji kati ya waliopo kikosini sasa.

Licha ya idadi kubwa ya washambuliaji iliyosajili, Ihefu SC inaacha swali kama itasajili katika kipindi hiki au haitofanya hivyo?, kutokana na safu yake ya ushambuliaji kutofunga bao lolote hadi sasa katika mechi mbili za mwanzo.

Katika kikosi cha sasa, Ihefu ina Jafary Kibaya, Isah Ngoah, Obrey Chirwa na Andrew Simchimba wanaocheza nafasi ya mshambuliaji wa kati.

Coastal Union, Geita Gold na Kagera Sugar ambazo kila moja imefunga bao moja katika mechi za mwanzo, pengine zinaweza kusaka watu wachache wa kuwaongezea nguvu katika safu zao za ushambuliaji.

Udhaifu ulioonyeshwa na safu za ulinzi za Dodoma Jiji, Geita Gold, Polisi Tanzania na KMC, Mtibwa Sugar, Mbeya City na Kagera Sugar unaacha swali kama zitasajili mabeki na makipa wa kuimarisha kuta zao au zitaendelea na waliopo.

Kocha wa KMC, Hitimana Thiery alisema hatofanya usajili katika nafasi ya ulinzi na atakachofanya ni kuwaimarisha waliopo.

SOMA NA HII  DIARRA KAMA KAWA DHIDI YA AL AHLY

Kocha wa Kagera Sugar, Francis Baraza alisema kwa usajili walioufanya hadhani kama wataongeza sura mpya zaidi ya kuboresha viwango vya waliopo kikosini.