Home Habari za michezo KIPANGA FC WAZIFUNIKA SIMBA NA YANGA CAF….YAWA TIMU YA KWANZA KUVUKA KUTOKA...

KIPANGA FC WAZIFUNIKA SIMBA NA YANGA CAF….YAWA TIMU YA KWANZA KUVUKA KUTOKA TZ…KIMBEMBE KIPO HUKU…


KIPANGA ya visiwani hapa imekuwa timu ya kwanza ya Tanzania kusonga mbele kwenye michuano ya CAF, baada ya kuingoa Al Hilal Wau ya Sudan Kusini kwa mikwaju ya penalti 4-3 na kuifuata Azam FC ilipangwa kuanzia raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Dakika 90 za mchezo huo wa marudiano uliopigwa Uwanja wa Amaan, mjini Unguja, ziliisha kwa sare ya 1-1 na kufanya matokeo ya jumla ya mechi zao mbili kuwa 2-2 baada ya awali kutokla sare kama hiyo katika mechi ya kwanza iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, Wasudan wakiwa wenyeji.

Wageni walitangulia kupata bao la kwanza dakika ya 25 kupitia Mostafa Abaker baada ya mabeki wa Kipanga kufanya uzembe wakati wa kuokoa mpira wakiwa langoni mwao na mfungaji huyo kumchambua kipa Mohamed Khamis Seif. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili maafande hao wa jeshi la wananchi, walikuja kivingi kwa kutengeneza nafasi kadhaa na dakika ya 74 Mundhir Ali Vuai akafunga bao la kusawazisha likiwa la pili kwake kwenye michuano hiyo kwani katika mchezo wa kwanza ndiye aliyeitanguliza Kipanga kabla ya Wasudan kusawazisha.

Ndipo pambano hilo likapelekwa kwenye matuta na Kipanga kupata penalti 4-3, huku kipa wake, akiibuka shujaa kwa kudaka mikwaju mitatu ya penalti za Al Hilal na penalti yamwisho iliyoivusha Kipanga ilifungwa na Vuai.

Kwa matokeo hayo Kipanga iliyorejea kwenye michuano ya CAF kwa mara ya kwanza tangu iliposhiriki mara ya mwisho mwaka 2005, itakutana na Club Africain ya Tunisia kwenye hatua hiyo ambayo Azam itakayoanzia huko, itacheza na Al Akhdar ya Libya iliyoitoa Ahli Khartoum ya Sudan kwa mabao 3-0 ya ushindi wa nyumbani kabla ya juzi usiku kutoka suluhu mjini Khartoum.

Hii ni mara ya pili kwa timu ya Zanzibar kufuzu raundi ya kwanza tangu 2019, Malindi ilipoing’oa Mogadishu City ya Somalia.

Wawakilishi wengine wa Tanzania, Yanga na Geita Gold zipo uwanjani kwa mechi za marudiano za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho na baadae KMKM itakuwa ugenini mjini Benghazi, Libya ikikabiliana na Al Ahli Tripoli, ikiwa na kumbukumbu ya kucharazwa 2-0 nyumbani wiki iliyopita.

SOMA NA HII  BAADA YA KUWAGOMEA...GEITA WAAMUA KUMALIZANA MAZIMA NA NTIBAZONKIZA...