Home Habari za michezo KUELEKEA MICHUANO YA CAF MSIMU HUU….KOCHA WA AS VITA AICHAMBUA YANGA ‘IN...

KUELEKEA MICHUANO YA CAF MSIMU HUU….KOCHA WA AS VITA AICHAMBUA YANGA ‘IN AND OUT’ …AITAJA AL HILAL…


Kocha Msaidizi wa AS Vita ya DR Congo Raul Shungu, amelishauri Benchi la Ufundi la Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans chini ya Kocha Mkuu Nasredeen Nabi, kwa kulitaka kuongeza nguvu kwenye maandalizi kama wanataka kufanya vizuri katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Young Africans imekuwa ikishindwa kufanya vizuri katika Michuano ya Kimataifa kwa miaka ya hivi karibuni, huku MSimu uliopita 2021/22 ikitolea hatua ya awali kwa kufungwa na Mabingwa wa Nigeria Rivers United jumla ya 2-0.

Msimu huu 2022/23 Young Africans imepania kufanya kweli katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, wakidhamiria kutinga hatua ya Makundi likiwandio lengo lao la kwanza walilojiwekea.

Kuna dalili zote za Young Africans ikakutana na wawakilishi Sudan Al Hilal, ambapo kikosi chao kinanolewa na Kocha Mashuhuri Barani Afrika Frolent Ibenge, endapo watawatoa Mabingwa wa Sudan Kusini Zalan FC.

Raul Shungu ametoa kauli hiyo kutokana na Young Africans kuanzia hatua ya awali, ambapo itacheza dhidi ya Zalan wakati Ali Hilal ikitarajia kucheza na Mabingwa wa Ethiopia St. George kabla ya washindi wa michezo hiyo kukutana.

Shungu amesema kuwa licha ya Young Africans kuwa na wachezaji wengi kutoka DR Congo lakini bado wanatakiwa kufanya kazi ya ziada ikiwa watakutana na Al Hilal ya Sudan, kutokana na kocha wake kuwafahamu vizuri wachezaji hao.

“Sioni sehemu ambayo Young Africans au Al Hilal zikishindwa kufanya vizuri katika michezo yao ya kwanza kwa sababu msimu uliopita Ibenge ameshinda ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na RS Berkane na amefanya usajili mzuri sawa na Young Africans, naona nafasi ya wao kukutana ni kubwa.”

“Nadhani utakuwa mchezo mgumu sana licha ya Young Africans kuwa na wachezaji wengi ambao ni wazoefu lakini tayari washafanya kazi na Ibenge hapa AS Vita, maana bado itawalazimu kufanya maandalizi makubwa ili kuweza kufikia malengo, kwa sababu Ibenge anawajua wachezaji na ni rahisi kuweza kubadilika,” amesema Shungu.

SOMA NA HII  SHUGHULI NZIMA ITAKUEPO ANFIELD WIKIENDI HII KATI YA LIVERPOOL NA MAN UNITED...

Young Africans itaanza kempeni ya kusaka taji la Afrika kwa kucheza dhidi ya Mabingwa wa Sudan Kusini Zalan FC mnamo Septemba 10 kabla ya kurudiana Septemba 17, Michezo yote ikipangwa kuchezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.