Home Habari za michezo SAKATA LA KUTOKUWA NA CHETI….NABI AWALIPUA WANAOMSIMANGA…AWATAJIA KLOPP NA ANCELOTI…

SAKATA LA KUTOKUWA NA CHETI….NABI AWALIPUA WANAOMSIMANGA…AWATAJIA KLOPP NA ANCELOTI…


Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amecheka sana baada ya kusikia na kukutana na maswali juu ya taaluma yake ya ukocha, akidaiwa hana vigezo vya kukaa benchi la timu hiyo kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini, kisha akatoa kauli ya kibabe.

Nabi alisema, kiwango chake cha taaluma hiyo sio kinamruhusu kuinoa Yanga tu, bali hata klabu kubwa duniani ikiwamo Al Ahly ya Misri au Barcelona ya Hispania na kutaka watu wasiomfananishe na baadhi ya makocha wa timu nyingine ambao wamekuwa na tatizo la vyeti vya kuungaunga.

Kauli hiyo ya Nabi inakuja kukiwa kumenea uvumi juzi kuwa, huenda angekaa jukwaani katika mechi ya kwanza dhidi ya Zalan utakaopigwa juzi Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam na timu hiyo kushinda mabao 4-0, matatu yakifungwa na Fiston Mayela na jingine Feisal Salum.

Nabi amewashusha presha mashabiki wa timu yake akisema vyeti alivyonavyo sio tu Yanga anaweza kuifundisha hata Barcelona ya Hispania, Al Ahly ya Misri na klabu yoyote kubwa duniani zikimhitaji.

Kocha Nabi aliyepata ushindi wake wa kwanza wa mechi za kimataifa akiwa na kikosi cha Yanga tangu aajiriwa Aprili mwaka jana, alisema wapo makocha wengi wakubwa wenye leseni kama yake ya Uefa Pro wanazifundisha klabu kubwa Ulaya wakiwemo Carlo Anceloti, Jurgen Klopp, Xavi Hernandez na hata Pep Guardiola.

“Nimeziona hizo taarifa, nimeshangaa, nafikiri ni siasa za soka la hapa Tanzania, wanaosambaza hizi taarifa waambieni kuwa sio Yanga tu, bali hata Barcelona, Al Ahly, Real Madrid, Manchester City zikinihitaji naweza kwenda kuzifundisha kwa leseni niliyonayo,” alisema Nabi aliyewahi kuziona Al Ahly Benghazi ya Libya, Al Hilal na El Marrikh za Sudan na kuongeza;

“Nenda kawaulize Klopp ana leseni gani, nenda kwa Ancelotti (Carlo), Guardiola, Xavi au Jose Mourinho wana leseni ipi, nafikiri kama kuna kitu hakipo sawa, hilo ni swali kwa viongozi wa klabu, kazi yangu ni kuwaandaa wachezaji. Mimi sio kocha mdogo kama wanavyofikiria.”

SOMA NA HII  KOCHA YANGA "SIMBA TUMEWAFUNGA TOKA MAZOEZINI...TUNATAKA POINTI 3 TU...AMEZUNGUMZA HAYA

Kocha huyo aliyeongoza Yanga kwenye mechi 40 za Ligi Kuu Bara bila kupoteza tangu Aprili 25, 2021 alisema; “Ni bahati nipo hapa Yanga naheshimu hii klabu na mashabiki wake, nimechagua kuwa hapa, ila isiwe nafasi ya watu kunidharau na kuniona kama kocha mdogo hiyo siwezi kunyamaza.”

Aidha Nabi alisema anashangaa kuona taarifa hizo huku watu wakisahau kwamba aliiongoza Yanga katika michuano hiyo msimu uliopita, japo alitolewa raundi ya awali na Rivers United ya Nigeria na kama angekuwa na tatizo asingeweza kuiongoza.

“Nilitakiwa kuleta cheti changu ili kuwaonyesha, bahati mbaya vipo nyumbani Ubelgiji, lakini nimewasiliana na watu wa Shirikisho la Ubelgiji wakanitumia nakala hiyo nadhani tayari ilishakwenda CAF (Shirikisho la Soka Afrika),” alisema Nabi akionekara kukerwa na taarifa hizo na kuongeza;

“Kuna mafanikio ambayo tunayapata hapa Yanga ni vyema watu wakaweka heshima kwa makocha, kijana wangu(mwanae) anafuatilia taarifa za hapa katika mitandao akiwa Ubelgiji, ameshangaa sana kuhusu taarifa hizo.”