Home Habari za michezo MASTAA SIMBA WAANIKA SABABU ZA YANGA KUPIGWA ZA USO SUDAN….

MASTAA SIMBA WAANIKA SABABU ZA YANGA KUPIGWA ZA USO SUDAN….

Wachezaji wa zamani wa Simba SC, Abdallah Kibaden na Bakari Malima, wameibuka na kusema kuwa sababu kubwa iliyopelekea Yanga kuondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni kutokana na kukosa uzoefu kama ilivyo kwa wapinzani wao Simba.

Wakongwe hao wametoa kauli hiyo kufuatia Yanga kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 2-1 dhidi ya Al Hilal ya Sudan baada ya mechi zote mbili ambapo kwa sasa watacheza mtoano kunako Kombe la Shirikisho Afrika kuwania kuingia makundi.

Kibadeni alisema licha ya Yanga kuwa na kikosi kizuri, lakini kimeshindwa kufuzu kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo kutokana na kukosa uzoefu.

“Kilichowafanya Yanga watolewe ni uzoefu, siyo jambo la siri kwamba Yanga hawana uzoefu katika michuano ya kimataifa kama ilivyo kwa Simba ambao imekuwa ikifanya vizuri, ingawa Yanga wana kikosi kizuri.

“Nadhani kwa sasa wao ni kuangalia walikosea wapi kwa sababu wametoka kwenye hatua moja na kwenda hatua nyingine ambayo ikiwa wataweza kujipanga na kurekebisha walipokosea, wanayo nafasi ya kufanya vizuri japo siyo safari ya mara moja,” alisema Kibadeni.

Kwa upande wa Malima ambaye amezitumikia Simba na Yanga, alisema: “Kwa sasa siyo wakati wa kulaumiana, zaidi ni kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kutokana na kukosa uzoefu wa kutosha kwenye michuano hiyo ya kimataifa kama ilivyokuwa kwa wapinzani wao Simba.”

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YA KARIAKOO DABI...OKRAH NA PHIRI WAAPA 'KUIHEMEA' YANGA...