Home Habari za michezo WAKATI SIMBA NA YANGA ZIKIUMIZA VICHWA….HAYA YA PHIRI NA MAYALE UNAYAJUA..?MAMBO YAO...

WAKATI SIMBA NA YANGA ZIKIUMIZA VICHWA….HAYA YA PHIRI NA MAYALE UNAYAJUA..?MAMBO YAO NI KIMYA KIMYA..

Wakati makocha wa Simba na Yanga wakikuna vichwa juu ya mechi za marudiano za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazopigwa wikiendi hii, nyota wa timu hizo Moses Phiri na Fiston Mayele nao wana kazi nzito.

Mayele na Phiri ndio vinara wa mabao wa timu hizo, pia wanachuana kwenye orodha ya wakali wa mabao kwa mechi za mchujo za michuano ya CAF, Mzee wa Kutetema akiwa ndiye kinara akiwa na mabao saba, huku Phiri akimfuata nyuma na mabao manne.

Mayele alifunga mabao sita, kwenye mechi za raundi ya awali dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini kabla ya wikiendi iliyopita kufunga dhidi ya Al Hilal ya Sudan katika sare ya 1-1 nyumbani. Timu hizo zinarudiana wikiendi hii mjini Khartoum, Sudan li kuamua atakayeenda makundi na wa kuangukia play-off ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa upande wa Phiri mwenye mabao manne pia katika Ligi Kuu Bara, alifunga mabao matatu raundi ya awali dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi akianza na bao moja mjini Lilongwe kisha kutupia mawili jijini Dar.

Wikiendi iliyopita, Simba ikicheza dhidi ya Primeiro de Agosto ya Angola, Mzambia huyo aliutupia tena bao moja na kushika nafasi ya pili nyuma ya Mayele, akilingana pia na staa wa Petro Atletico ya Angola, Tiago Azulao mwenye mabao manne pia ambaye msimu uliopita ndiye aliyekuwa Mfungaji Bora wa michuano hiyo akifunga sita.

Vita ya wakali hao wa Simba na Yanga ipo wikiendi hii tena wakati timu zao zikirudiana na wapinzani wao, Mayele akiwa ugenini wakati Phiri akiwa nyumbani na yeyote akitumia nafasi atakazopata atamaliza mechi hizo za mtoano kwa heshima, licha ya mabao hayo hayaingizwi kwenye kinyang’anyiro.

Kazi kubwa inaonekana kwa Phiri na Tiago ambao kila mmoja anatakiwa kufunga mabao zaidi ya matatu ili kufikia mabao ya Mayele.

Tofauti na miaka ya nyuma ya michuano hiyo CAF ilipokuwa ikiyahesabu mabao yote yakiwamo ya raundi za mchujo, kwa sasa mabao hayo yataishia kwenye hatua hiyo.

Ili Mayele na Phiri wanyakue tuzo ya Mfungaji Bora kutoka timu ya Tanzana kufikia rekodi zilizowekwa na Thuen Ally wa Simba na Mrisho Ngassa wa Yanga ni lazima wazipiganie timu zao zitinge makundi kama alivyofanya Tiago msimu uliopita.

Ngassa alitwaa tuzo mwaka 2014 sambamba na nyota watatu wa timu za ES Setif ya Algeria, Esperance ya Tunisia na As Vita, kabla ya Mbwana Samatta akiichezea TP Mazembe kubeba tuzo 2015 sambamba na Bakri Al Madina wa Al Merrikh na kuwa Mtanzania wa tatu kutwaa tuzo kwenye michuano hiyo.

Awali mchezaji wa Simba, Mzanzibar, Thuwen Ally akiichezea Simba alikuwa Mtanzania wa kwanza kubeba tuzo ya Mfungaji Bora wa Afrika katika michuano hiyo mwaka 1979 akifunga ‘hat trick’ ugenini Zambia wakati michuano hiyo ikiitwa Klabu Bingwa kabla ya kubadilishwa mwaka 1997.

SOMA NA HII  SAKATA LA KISINDA...KIGOGO TFF AVUNJA UKIMYA...AFUNGUKA A-Z WENZAKE WALIVYOBORONGA...KUMBE SABABU NI ....