Home Habari za michezo DK KADHAA KABLA YA YANGA KUKIPIGA NA WATUNISIA…MTOTO WA NABI AJITOKEZA NA...

DK KADHAA KABLA YA YANGA KUKIPIGA NA WATUNISIA…MTOTO WA NABI AJITOKEZA NA HILI….BABA YAKE AKIFELI NDIO BASI TENA…

Yanga ina dakika 180 kuamua hatma yake kimataifa msimu huu dhidi nya Club Africain ya Tunisia. Ni mechi mbili ambazo zitaamua nani akacheze makundi ya Kombe la Shirikisho. Mechi ya kwanza ni leo, Novemba 2 na marudiano Novemba 9.

Nitakupa tathmini ya kikosi cha Club Africain kwa ubora na udhaifu wa kila mmoja wao na tathmini hii nimeshea pia na Kocha Nabi ambae ni mzazi wangu;

MOEZ HASSEN – KIPA

Ndio tegemeo. Moes Hassan (27) ambaye kipaji chake kimejengwa sana nchini Ufaransa alikokulia akianza kucheza soka la kulipwa akiwa na klabu ya Nice inayocheza ligue 1 ya Ufaransa. Baadaye kipa huyo alikwenda kucheza nchini Ubelgiji kwa msimu mmoja kabla ya kurejea tena Ufaransa kutua klabu ya Stade Brestois ambayo pia inacheza ligi kuu nchini humo.

Amekuwa pia akiitwa timu ya Tunisia na kwasasa amerudishwa tena Club Africain kwa mkopo ili apate muda wa kutosha wa kucheza baada ya kukaa sana benchi Ufaransa.

Ni kipa ambaye ana hesabu nzuri akiwa langoni hasa kwa mashuti ya chini,ni rahisi sana kutema mipira hasa ya juu kitu ambacho kama washambuliaji wa Yanga watafuatilia mashuti anayopigiwa wanaweza kunufaika.

SKANDER LAABIDI

Ni beki wa kulia aliyezaliwa miaka 23 iliyopita lakini pia ana ubora wa kucheza kama beki wa kati, huyu ni mlinzi ambaye ni zao asilia la timu ya vijana ya klabu hiyo, ana ubora mkubwa wa kukabiliana na mtu kwa mtu, sio rahisi kumpita akikutana na mshambuliaji mmoja.

Ni beki jasiri, anajiamini ingawa hali ya kujiamini sana kuna wakati amekuwa akijikuta anasababisha hatari langoni kwake, aliwahi kulaumiwa kwa makosa hayo mara kadhaa katika mechi za ligi ya Tunisia.

NADER GHANDRI

Beki mwingine bora wa Club Africain. Alijengwa na klabu hiyo akichipukia hapo ingawa badaye alikwenda nchini Ufaransa kujiongezea ubora zaidi akikaa huko kwa miaka mitatu kabla ya kutua Ubelgiji kwenye klabu ya Royal Antwerp inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza akikaa misimu miwili na baadaye kutimkia klabu nyingine ya nchini Bulgaria kisha kurejea Club Africain.

Ni bora kwenye mipira ya vichwa akiwa na nguvu na akili iliyotulia, makosa yake makubwa ni katika kasi sio mlinzi anayependa mbio kabisa na hata anaweza kufanya makosa makubwa na sio mzuri katika kutafuta mipira inapopotea kutokana na kukosa kasi.

NABIL LAAMARA

Lamaara (29) ni mlinzi wao wa kushoto raia wa Algeria, alianza kucheza soka la kulipwa akiwa na klabu ya daraja la kwanza ya Kouba ya nchini kwao,amewahi pia kuitumikia kwa muda mfupi klabu kubwa ya huko MC Alger akitumika hapo kwa misimu miwili pekee kabla ya baadaye kuchukuliwa na Club Africain mwaka jana 2021.

Huyu Lamaara beki wa kisasa wa kushoto, ubora wake ni katika kupandisha mashambulizi hasa akiwa na kasi anajua kupangua mabeki na kupiga krosi lakini pia hata kupiga mashuti shida yake ni kwamba anapoondoka huacha nafasi ambayo kama Yanga watakuwa na ubora wa kutumia nafasi hiyo itawanufaisha.

TAOUFIK CHERIFI

Kiungo wao bora wa ukabaji ni Taoufik (20), ambaye kuna wakati pia hutumika kama beki wa kati wanapokuwa na mapungufu, amejengwa na klabu hiyo wakiwa na imani kwamba kwa umri wake mdogo atakuja kuwapa mafanikio.

Ni mrefu kwa kimo lakini anahama kirahisi, ana ubora wa kujua kujenga mashambulizi lakini akiwa na ubora wa kupokonya mipira shida yake kubwa hana uzoefu wa kutosha katika mechi za Kimataifa.

AHMED KHALIL

Ahmed Khalil (20), huyu ni kiungo raia wa Tunisia anayecheza eneo la kiungo akiwa mzuri wa kujua kukaba lakini pia kuhama kupandisha mashambulizi ni mtoto wa staa wa zamani wa Kimataifa wa Tunisia Mohamed Khalil.

Unaweza kumfananisha na Khalid Aucho kwa kuwa anaweza pia kucheza kama kiungo wa kati juu wa ushambuliaji yaani namba 8, ni fundi mzuri anapokuwa na mpira.

Yanga wanatakiwa kuwa naye makini kwa kuwa anajua sana kupiga mashuti makali ni injini ya Club Africain kwa kuwa mashuti yake yamekuwa yakitumiwa na washambuliaji pia kama wakikutana na makipa wanaotema mipira, mashambulizi yao mengi yaanzia hapa kama yakitokea katikati ya uwanja.

Anapenda sana kukokota mipira lakini tabia yake hii wakati mwingine imekuwa ikimzalishia makosa makubwa hasa anapopokonywa mipira, Yanga wanatakiwa kumchunga zaidi kwa kumnyima utulivu.

Anaaminika hasa kwa mashabiki wao wa nyumbani akishika mpira ana nyimbo zake wanamuimbia kumchangamsha kwamba timu inakutegemea wewe, usipomdhibiti wakati akiimbiwa nyimbo hizo unaweza kupata madhara makubwa.

LARRY AZZOUNI

Larry Azouni (28),huyu ni staa wa Club Africain lakini pia taifa la Tunisia aliyezaliwa Machi 23,1994,jijini Marseille nchini Ufaransa anacheza kama kiungo wa kati pia ana ubora mkubwa akicheza eneo hilo, amejengwa akiwa kijana akicheza fainali za vijana Ulaya chini ya miaka 19 mwaka 2013 akiwahi pia kucheza Fainali za Mataifa Afrika mwaka 2017.

Azzouni ni mchezaji mzoefu akipita pia klabu kubwaa ya Olympique de Marseille, Lorient,Nymes Olympiques,akipita pia Ubelgiji kisha Ureno kabla ya sasa kutua Club Africain. Huyu ni kiungo asili wa kati na ndio roho yao nyingine, anajua sana kupiga mipira ya adhabu,mabeki wa Yanga na viungo wake hawatakiwi kucheza madhambi karibu na eneo lao la hatari, mabao kama ya Stephane Azizi KI anayafunga sana na ndio yanampa umaarufu.

Anajua sana kupiga pasi za hatari za kupenyezwa katikati ya walinzi, pasi kama anazopiga Aziz KI au Clatous Chama wa Simba hivi ndio vitu cyake bora,makosa makubwa ni kumwachia nafasi kubwa kufanya maamuzi yake atakughalimu, anatakiwa kuchungwa sana kama kuna kazi viungo wa Yanga watafanya ni kumchunga huyu kama atakuwa uwanjani.

ABDENOUR IHEB BELHOUCINI

Winga wao wa kushoto ni huyu Abdenour Belhoucini ambaye ni raia wa Algeria (26), amejengwa na klabu ya kwao ya Usm Bel Abbés,alicheza pia kwa miaka miwili Qatar kabla ya kujiunga na Club Africain.

Huyu ni winga jasiri anayejua kukimbia kwa hesabu nzuri na kutoa pasi zenye athari kwa wapinzani lakini pia anajua kufunga kama atapewa nafasi ya kujaribu karibu na lango, beki atakayekabana naye anatakiwa kutuliza akili ili aweze kumdhibiti kwa kuwa kuna wakati ana hama hama upande wowote kujaribu maeneo tofauti ya kushambulia.

ADEM TAOUES

Winga wao wa kulia ni huyu ambaye amelelewa hapohapo klabuni kwao akiwa pia amepita katika msingi bora wa timu za vijana za timu ya Taifa la Tunisia, anaweza pia kucheza ka ma winga wa kushoto akiwa na faida ya kutumia miguu yote ingawa mguu wake wa kulia ndio wa hatari ndio maana anapewa nafasi ya kucheza kulia.

Ukiona anataka kutokea winga ya kushoto tambua kwamba anataka kujaribu kupiga mashuti kutokana na mguu wake wa kulia ndio silaha yake kubwa, anajua kuwatoka mabeki kutokana na mbinu zake akinufaika na kasi yake hatakiwi kucheza huru sana.

ZOUHAIER DHAOUADI

Dhaouadi ndio mchezaji au kiungo mshambuliaji wa nyuma ya mshambuliaji wa mwisho mwenye uzoefu mkubwa kuliko mwingine yoyote aliyezaliwa miaka 34 iliyopita akiwa amecheza mechi 31 za timu ya taifa ya Tunisia akiwa na ubora pia wa kutumika kama winga wa kushoto.

Kwasasa amebadilishiwa majukumu akicheza kama kiungo mshambuliaji nyuma kidogo ya mshambuliaji wa mwisho kutokana na ubora wake kutumia makosa madogo ya mabeki wa timu pinzani akisahaulika kidogo anaweza kufunga na kuiweka Yanga katika mazingira magumu.

MOHAMED ALI OMRI

Ana miaka 26 na ni kiraka katika eneo la ushambuliaji ingawa asili yake ni mshambuliaji wa mwisho kama anavyotumika hapo kwasasa, amezichezea klabu mbalimbali za hapo Tunisia lakini pia Libya.

Sio mchezaji hatari sana lakini ubora wake ni kwamba sio mtu anayekata tamaa anapenda kujaribu lakini pia anajua kufunga na kutumia nafasi vitu ambavyo vimekuwa vikimtanguliza kupata nafasi mbele ya kocha wa timu hiyo, ana mbinu za miguuni katika kuwatoka mabeki kama kuwapindua kwa haraka na kufunga kama akikutana na mabeki wanaofanya makosa yanayojirudia.

Yanga inaweza kushinda mechi ya hapa nyumbani lakini lazima wachezaji wetu wahakikishe wanaongeza umakini mkubwa kwanza kutumia nafasi watakazotengeneza lakini pia kasi ya kutengeneza mashambulizi.

Kama wachezaji wa Yanga watatanguliza mafanikio ya timu kwa kuangaliana nani anaweza kufunga kirahisi wanaweza kupata matokeo makubwa ambayo yatawabeba ugenini lakini bila kusahau kucheza kwa nidhamu kubwa ya kukaba kwa nguvu na kushambulia nawatakia kila la kheri wananchi wenzangu.

Mwandishi wa makala hii ni mtoto wa Kocha wa Yanga, Nasredeen Nabi anayeitwa Hedi Nabi. Ameiona timu hii muda mrefu nchini kwao ikicheza mechi mbalimbali.

SOMA NA HII  WAKATI MADILI YAKIZIDI KUMMIMINIKIA ....MANDONGA AMTAKA TENA KAONEKA...ATAMBA SAFARI HII LAZIMA AUWEE MTU....

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here