Home Habari za michezo HII ‘UNBEATEN’ YA YANGA HAIKUJA HIVI HIVI….KARIBU BILIONI KUMI ZIMETUMIKA…UKWELI HUU HAPA…

HII ‘UNBEATEN’ YA YANGA HAIKUJA HIVI HIVI….KARIBU BILIONI KUMI ZIMETUMIKA…UKWELI HUU HAPA…

Tetesi za Usajili Yanga

KATIKA kujenga kikosi bora Yanga kinachowapa matokeo ya sasa, haikufikia mafanikio hayo kwa usiku mmoja tu. Yanga ilifanya mabadiliko makubwa ikiondoa kundi la wachezaji 12 na kuingiza wapya 26 kwa nyakati tofautikitu ambacho kinaweza kuwa kimeugharimu uongozi wa Yanga zaidi ya bilioni kumi za usajili na kuitunza timu kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kwa nyakati tofauti Yanga iliwatema, kuwauza wachezaji tofauti huku wengi wao wakishtua mashabiki. Lakini ililazimika kufanya hivyo ili kufikia malengo. Makipa wake watatu Farouk Shikhalo, Metacha Mnata na Ramadhan Kabwili walikwenda na maji kwa sababu mbalimbali.

Mabeki ni Paul Godrefy ‘Boxer’, Adeyun Saleh, Yassin Mustapha, Abdallah Shaibu ‘Ninja. Viungo Mapinduzi Balama, Mukoko Tonombe, Carlos Gumares ‘Carlinhos’, Deus Kaseke huku washambuliaji Michael Sarpong, Ditram Nchimbi, Waziri Junior na Saido Ntibazonkiza.

Kocha wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera wakati timu hiyo inaanza kufumua kikosi aliwahi kusema; “Wakati mwingine lazima ubadilishe gia kwa kutumia hawa wachezaji wenye asili ya Kifaransa. Ni watu wa kazi sana na wana malengo.”

Kwa nyakati tofauti waliwaingiza mastaa wapya 26. Wakianza na Fiston Mayele, Yannick Bangala, Khalid Aucho, Diarra Djigui, Kibwana Shomari, Yusuf Athuman, Farid Mussa, Erick Johora, Djuma Shaban, Bryson Raphael, Jesus Moloko, Zawadi Mauya, Dickson Ambundo na Heritier Makambo.

Baadaye waliimarisha zaidi wakiwaingiza Dickson Job, Aboutwalib Mshery, Ibrahim Abdallah ‘Bacca’, Salum Aboubakar ‘Sure Boy. Msimu huu wakawaingiza sita wapya wakiwemo Stephane Aziz KI, Bernard Morrison, Tuisila Kisinda, Lomalisa Mutambala na Gael Bigirimana.

SIKIA YA FEITOTO

Ukiangalia kuanzia msimu ambao Kocha Nasuruddine Nabi aliipokea timu hiyo kutoka kwa kocha wa muda Juma Mwambusi kuna kiungo mmoja tu amesalia katika timu hiyo mpaka sasa Feisal Salum ‘Fei Toto ambaye ndiye staa aliyekaa ndani ya timu hiyo kwa muda mrefu.

Rekodi zaidi ya Feisal ni kwamba sio tu kubaki kuwa staa pekee aliyekaa hapo kwa muda mrefu lakini pia amejihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza na akipewa cheo cha nahodha msaidizi.

BENCHI LA UFUNDI MOTO

Kwenye benchi la ufundi nako Yanga iliendelea kuliboresha ikimwongeza kocha mpya wa makipa Milton Nienov raia wa Brazil akichukua nafasi ya Mkenya, Razack Siwa. Nuenov akija kuungana na Nabi na wasaidizi wengine Cedric Kaze, Helmy Gueldich na madaktari wa timu hiyo.

HERSI-USAJILI MPAKA RAIS

Katika kusimamia usajili wote huo, Yanga dereva alikuwa Hersi Said ambaye akitokea kuwa bosi wa kampuni iliyofadhili maboresho hayo ya GSM mpaka baadaye akawa Rais wa klabu hiyo.

Hersi alisema kazi hiyo ya kujenga timu imara ukiacha usajili ambao ulifanyika haikuishia hapo, bali iliendelea mpaka nje ya uwanja kwa kuboresha posho za ushindi wa mechi ndogo na zile kubwa hali ambayo iliamsha mzuka mkubwa kwa wachezaji wao kuipigania klabu yao.

“Tulianza na kuboresha posho za kuwapa morali wachezaji, kama mtakumbuka tulianza na kutoa kiasi cha Sh 10 milioni kwa kila mchezo ambao tutashinda ambazo ziliwapa morali wachezaji tukiamini kwamba tukiwekeza kwao klabu itapata matokeo bora,” alisema Hersi.

“Posho hizo ziliendelea kuongezeka zaidi mpaka kufika mamilioni, tunafurahia matokeo ya uwekezaji mzuri wa timu kutofungwa, rekodi ambayo sio tu Afrika sasa inapasua mpaka klabu kubwa za Ulaya.”

Aidha Hersi alisema haikushia tu kuboresha kikosi chao lakini kazi hiyo iliendelea kwa kufanya mabadiliko ya uendeshaji wa klabu kutoka mfumo wa kizamani na kwenda ule wa kisasa ambao uliunda safu bora ya utawala ambayo ipo nyuma ya mafanikio hayo.

“Hatukuyafanya haya kwa usiku mmoja, tulijenga uimara wa timu hii hatua kwa hatua utaona baada ya kuimarisha benchi la ufundi chini ya kocha Nabi.

“Mtaona jinsi ufundi na ubora wa wachezaji unavyozingatiwa, tunashirikiana kwa ukaribu mkubwa wengine nje ni ngumu kuona hili, lakini niseme matokeo yake ni mafanikio kama haya ya ubora yanavyoendelea kujionyesha.

“Ukiangalia sasa Yanga ipo ndani ya muendelezo wa maboresho ya mfumo wa uendeshaji, utaona sasa ndani ya klabu kila idara inafanya kazi yake, hakuna tena muingiliano wa kiidara na makosa ya kiutawala kama ambavyo ilikuwa huko nyuma, haya yote kwa ujumla ndio yanaleta hii timu ambayo haifungiki kirahisi. Niwashukuru wanachama wetu na mashabiki kwa hatua yao ya kuamini na kuwa wavumilivu na sasa mafanikio haya tunayafurahia kwa pamoja.

“Kama klabu tunaona bado tuna safari ya mafanikio zaidi katika kukisuka kikosi imara, hatuwezi kusema haya ni mafanikio yetu makubwa tuna uhitaji mkubwa wa mafanikio zaidi ya haya. Ninachowaambia wanachama na mashabiki wetu waendelee kuuamini uongozi wao na tuko makini kujenga kikosi imara kitakachotupa mafanikio zaidi.”

KOCHA NABI ATAMBA

Akizungumzia hatua ya mafanikio hayo ya kikosi chake Nabi alisema hatua ambayo wamefikia ni ndoto zake pamoja na uongozi kujenga kikosi imara na kwamba kwake bado haijafikia katika ubora anaoutaka.

“Nilipofika hapa nilikuta malengo makubwa ya uongozi wa klabu, waliniambia wanataka nini lakini tulikaa pamoja kama familia taratibu tulianza kuboresha kikosi chetu kwa jinsi tulivyoona changamoto, ”alisema Nabi ambaye hivikaribu presha ya matokeo ya Ligi ya Mabingwa nusra yamharibie kibarua.

“Naushukuru uongozi wa klabu kuanzia nafasi ya rais mpaka mfadhili wetu Ghalib Mohamed kwa kunisikiliza mahitaji yangu kama kocha, tulikuwa na nia ya dhati kwa pamoja kuibadilisha hii klabu na kuwa na timu imara ambayo tunaendelea nayo sasa ingawa haikuwa rahisi,” alisema Nabi.

“Hatujamaliza hiyo kazi siwezi kusema Yanga imefikia katika kiwango kikubwa cha mafanikio, tunahitaji umoja zaidi na kusikilizana kufika mbali zaidi,” alisema Nabi na kuendelea; “Tuna wachezaji bora lakini bado hatua ya maendeleo inaweza kutufikisha kutamani watu bora zaidi kulingana na mafanikio tunayojipangia kama klabu.”

SOMA NA HII  RASMI....WAKATI YANGA WAKIENDA MAREKANI...KUELEKEA MSIMU UJAO SIMBA WABARIKI SAFARI YAO YA MISRI...