Home Habari za michezo KOCHA MPYA SIMBA KUANZA KAZI NA MWEZI WA MECHI NGUMU….ANASIKU 34 ZA...

KOCHA MPYA SIMBA KUANZA KAZI NA MWEZI WA MECHI NGUMU….ANASIKU 34 ZA KUJITETEA …

Siku yoyote kuanzia leo Simba itamtambulisha Kocha Mkuu mpya raia wa Ureno lakini akitua tu atakutana na siku 34 ngumu ambazo zinaweza kumbeba au kumuweka katika wakati mgumu ndani ya kikosi cha timu hiyo.

Ndani ya siku hizo, kocha huyo akisaidiwa na Juma Mgunda atakuwa na jukumu la kuiongoza Simba katika mechi sita mfululizo za Ligi Kuu itakazocheza kwenye viwanja vya mikoani ratiba ambayo kwa kiasi kikubwa imeshikilia hatima ya ubingwa wao msimu huu.

Ugumu wa ratiba hiyo inayomkabili kocha huyo mpya wa Simba unatokana na historia yao ya kutofanya vyema sana katika mechi zao ambazo wamekuwa wakicheza viwanja tofauti na ule wa Benjamin Mkapa ambao wanautumia kwa mechi zao za nyumbani ingawa viongozi wanaonekana kuimarisha idara zote ili wasitetereke.

Katika mechi 10 zilizopita za Ligi hiyo ambazo Simba imecheza nje ya Dar es Salaam, imepata ushindi mara mbili tu, ikitoka sare sita na kupoteza mechi mbili.

Ratiba hiyo ngumu kwa kocha mpya na Simba itaanzia leo katika mchezo baina ya Simba na Mbeya City itakayochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya na baada ya hapo itakuwa na siku nne za kusafiri na kujiandaa na mechi dhidi ya Polisi Tanzania itakayochezwa kwenye Uwanja wa Ushirika, mkoani Kilimanjaro, Novemba 27.

Desemba 3, Simba itakuwa mkoani Tanga kumenyana na Coastal Union na baada ya hapo itaelekea Mwanza kukabiliana na Geita Gold, Disemba 18 kisha siku tatu baadaye itakabiliana na Kagera Sugar ugenini.

Baada ya kumalizana na Geita Gold na Kagera Sugar, Simba itakuwa na kibarua kingine Disemba 26 dhidi ya KMC ambao mechi zao za nyumbani dhidi ya Simba wamekuwa wakicheza katika viwanja vya nje ya Dar es Salaam.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Ratiba ni ngumu kweli lakini mwisho wa siku hatuko peke yetu wenye hiyo ratiba hivyo hatupaswi kuanza kuilalamikia. Tunatakiwa twende tukakabiliane nayo maana sio sisi peke yetu hata wengine pia nao inawabana.”

“Changamoto ipo kiukweli, ligi ngumu na muda hautoshi lakini hatuna namna, inabidi upambane kwa kweli ili ufanye vizuri.”

Mgunda ambaye ni kipenzi cha mashabiki alisema: “Tunalazimika kuheshimu na kufuata kile kinachopangwa na mamlaka inayosimamia ligi hivyo kwa vile ratiba tayari ipo, tutajipanga kuhakikisha tunakabiliana nayo na kuona ni kwa jinsi gani tutapata matokeo mazuri.”

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema: “Wanasimba katika maeneo husika jiandaeni kikamilifu kuipa sapoti timu iweze kuvuna alama tatu kwenye kila mchezo husika.”

Ugumu wa ratiba ambao Simba watakabiliana nao ni kama ule ambao walikutana nao Oktoba ambapo walicheza mechi sita za mashindano tofauti ndani ya siku 29 ambazo waliangusha jpointi nne kwa kupoteza mmoja kati ya hiyo na kutoka sare moja.

Ilikuwa na mechi mbili za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Primeiro de Agosto ya Angola ambazo ilishinda na kutinga hatua ya makundi, lakini pia ikawa na mechi nne za Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji, Yanga, Azam na Mtibwa Sugar ambapo ilishinda mbili, kupoteza moja na kutoka sare katika mechi moja.

SOMA NA HII  AMRI KIEMBA AFUNGUKA YA MAYONI BAADA YA KUIONA SIMBA IKIKOSA HUDUMA ZA CHAMA NA LUIS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here