Home Habari za michezo UKWELI LAZIMA USEMWE….SHIDA YA SIMBA NI HAPA TU…PAKIKAA SAWA YANGA WATAKIMBIA NCHI…

UKWELI LAZIMA USEMWE….SHIDA YA SIMBA NI HAPA TU…PAKIKAA SAWA YANGA WATAKIMBIA NCHI…

Kikosi cha Simba SC Msimu huu wa 2022/23

Dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa Desemba 15 mwaka huu, linailazimisha Simba kusajili idadi kubwa ya wachezaji ambao kiasili ni washambuliaji kulinganisha na wale wa nafasi nyingine kwani tathmini ya kiufundi inaonyesha tatizo si benchi la Juma Mgunda bali ni uhalisia.

Tathmini ya kiufundi inaonyesha kuwa uwepo wa kundi kubwa la wachezaji ambao kiasili ni walinzi, hapana shaka umekuwa ukilipa wakati mgumu benchi la ufundi la timu hiyo kati upangaji wa kikosi na mipango mingine ya kitimu pindi inapokuwa na mechi hasa pale inapotokea anawakosa baadhi ya wachezaji ambao kiasili ni washambuliaji.

Katika kikosi cha wachezaji 27 ambacho Simba inacho kwa sasa ukiwa umesalia mwezi mmoja dirisha kufunguliwa, wachezaji ambao kiasili ni walinzi na wanacheza katika nafasi hizo wako 17 huku 10 tu wakiwa ndio wale ambao kiasili wanamudu kucheza katika nafasi za kushambulia.

Wachezaji hao 17 wa Simba ambao kiasili ni walinzi ni makipa watatu, Aishi Manula, Beno Kakolanya na Ally Salim pamoja na mabeki Kennedy Juma, Shomari Kapombe, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Gadiel Michael, Henock Inonga, Joash Onyango, Mohamed Ouattara, Erasto Nyoni, Nassoro Kapama, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute na Victor Akpan.

Nyota 10 ambao wanamudu kucheza nafasi za ushambuliaji ni viungo washambuliaji Nelson Okwa, Clatous Chama pamoja, mawinga Pape Sakho, Augustine Okrah, Peter Banda, Jimmyson Mwanuke na Kibu Denis huku washambuliaji wa kati wakiwa ni John Bocco, Moses Phiri na Habibu Kiyombo.

Namba hiyo ya wachezaji wa nafasi za ushambuliaji inaweza kupungua kubakia tisa kutokana Mwanuke pia kutumika kama beki wa kulia kwenye mechi nyingi za Simba.

Na kutokana na tatizo la majeraha na changamoto nyingine, benchi la ufundi la Simba chini ya mzawa Juma Mgunda kwa sasa limejikuta likibaki na wachezaji watano tu wa nafasi za ushambuliaji ambao ndio inalazimika kuwatumia katika nafasi za winga, kiungo mshambuliaji na mshambuliaji wa kati.

Mwanuke, Banda, Okwa na Bocco wamekuwa wakishindwa kutumika kutokana na majeraha huku Clatous Chama akitumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu ambayo ilikamilika baada ya mchezo wa jana dhidi ya Namungo FC.

Machaguo ya wachezaji wa upande wa ushambuliaji ambayo Simba imebakia nayo katika siku za hivi karibuni ni Kibu, Sakho, Kiyombo, Phiri na Okrah ambao kati ya hao, ni Phiri, Sakho na Okrah ambao angalau wameonekana kuwa na kiwango bora kwa sasa.

Uchache huo wa wachezaji wa nafasi za ushambuliaji umefanya nyota wachache wa timu hiyo kuwa na mzigo mkubwa wa kubeba kuhakikisha wanafanya vizuri na pindi nyota hao wanapodhibitiwa vyema na timu pinzani.

Mfano katika mchezo dhidi ya Ihefu, kocha Juma Mgunda alikuwa na chaguo moja tu la mchezaji wa nafasi ya ushambuliaji katika benchi la Simba ambalo lilikuwa ni Kibu Denis huku wachezaji saba wakiwa ni wa nafasi za ulinzi.

Katika mchezo huo, kiujumla Simba ilikuwa na wachezaji 15 ambao kiasili hucheza nafasi za ulinzi, kati ya 19 waliokuwemo kwenye kikosi cha mechi hiyo.

Uthibitisho wa hilo unaweza kuuona katika mechi za hivi karibuni ambazo mshambuliaji tegemeo wa Simba, Moses Phiri ameshindwa kufurukuta, Simba imekuwa ikiangusha pointi ama kupata ushindi wa tabu tofauti na pale ambapo Phiri anakuwa katika ubora wa hali ya juu.

Katika msimu huu, mechi nyingi ambazo Phiri ameonyesha kiwango bora, Simba ilifunga mabao mawili au zaidi na ni mechi moja tu ambayo haikufanya hivyo ambayo ni ile ya marudiano ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya Primeiro de Agosto ya Angola ambayo walishinda bao 1-0 lililopachikwa na nyota huyo wa Zambia.

Mechi ambazo Simba imeonekana kuhaha pindi Phiri anaposhindwa kufurukuta ni dhidi ya Yanga iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, dhidi ya Azam waliyopoteza kwa bao 1-0, mchezo wa Singida Big Stars waliyotoka sare ya bao 1-1 na mchezo dhidi ya Ihefu waliyoshinda bao 1-0.

Kocha wa Simba, Juma Mgunda alisema kwa sasa wanafikiria zaidi michezo iliyo mbele yao na suala la usajili ni hadi pale muda utakapofika.

“Kipaumbele chetu kwa sasa ni mechi zinazofuata kwani muda wa usajili bado haujafika. Changamoto za kitimu zinaendelea kufanyiwa kazi na muda sahihi wa kuzungumzia usajili ukifika tutafanya hivyo.

“Kuna changamoto ambazo kwa namna moja au nyingine zimekuwa zikituathiri kama vile majeraha ya wachezaji lakini tunaendelea kupambana nazo na namhsukuru Mungu tumekuwa tukipata matokeo mazuri,” alisema Mgunda.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema wataimarisha kikosi katika dirisha la usajili lakini hilo litategemea ripoti ya benchi la ufundi.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI DHIDI YA YANGA...'TRY AGAIN' ATOA AHADI YA KIBABE SIMBA..AFICHUA 'WALIVYOCHEZA KAMA PELE'..