Home Habari za michezo EDO KUMWEMBE:- ANAKOPITA MZIZE NI ‘SHORT CUT’….SIKU AKIIBEBA YANGA NDIO TUTAMJADILI…

EDO KUMWEMBE:- ANAKOPITA MZIZE NI ‘SHORT CUT’….SIKU AKIIBEBA YANGA NDIO TUTAMJADILI…

Habari za Yanga

Na Edo Kumwembe/MwanaSpoti


Sikumbuki lini ilikuwa mara ya mwisho kwa mchezaji kutoka katika kikosi cha vijana cha Yanga na kuja kucheza timu ya wakubwa. Pale Azam nakumbuka kina Aishi Manula walitoka katika kikosi cha vijana. Wakapandishwa wakawa mastaa wakubwa.

Pale Simba nadhani Jonas Mkude anabakia kuwa kijana wa mwisho kupata bahati hiyo. Nadhani kilichosaidia wakati huo kilikuwa umaskini ambao uliwakabili watu wa Simba. Yanga walikuwa na Yusuf Manji. Azam walikuwa kama kawaida wapo katika utawala wa familia ya Bakhresa. Simba hawakuwa na nguvu kubwa ya kipesa.

Wakajaribu kutuingiza mjini kwa kudai sera yao ilikuwa ni kukuza makinda. Walikuwepo kina Mkude, Ibrahim Ajibu, Miraji Athuman na wengineo. Ni kipindi ambacho Yanga na Azam zilishika nafasi mbili za juu kwa miaka mitano mfululizo huku Azam akitwaa ubingwa mara moja wakati Yanga wakitwaa mara nne mfululizo.

Baadaye Manji akachomoka Yanga halafu Mohammed Dewji akaingia Simba. Yanga wakarudi kule ambako Simba walikuwepo. Walilazimika kumsajili mchezaji kinda kama Yohana Mkomola kwa ajili ya kuongoza safu yao ya mashambulizi. Walipitia kipindi kigumu. Leo wapo chini ya GSM wamerudi tena kununua washambuliaji wazuri wenye hadhi ya kuongoza safu ya ushambuliaji ya Yanga kina Fiston Mayele.

Bahati nzuri kwa Mzize imeangukia hapa. Ghafla ameletwa kutoka kusikojulikana na ameanza kucheza katika kikosi cha kwanza cha Yanga akimsaidia Mayele. Ana bahati nyingi. Bahati ya kwanza ni kwamba Yanga haikupata mtu sahihi wa kumsaidia Mayele. Mcongo mwenzake, Heritier Makambo anaonekana kuwa hoi.

Yusuf Athuman haonekani sana kuchukia kukaa benchi wakati Lazarous Kambole ambaye alionekana amekuja kumpa wakati mgumu Mayele ameshindwa hata kuvaa jezi ya Yanga na kucheza kwenye Uwanja wa Mkapa. Ni hapo ambapo Mzize ametoka kusikojulikana kuja kuwa msaidizi wa Mayele. Ana bahati.

Bahati yake ya pili ni ukweli kwamba ameikuta Yanga imetimia. Katika soka la kisasa siku hizi wakubwa huwa wananunua wachezaji. Hawana muda wa kukuza makinda kutoka katika timu za vijana. Inabidi uwe kijana mwenye kipaji cha hali ya juu. Kuanzia Tanzania hadi duniani kote pesa imetawala. Wenye ubavu wa pesa huwa wanaziba nafasi kwa kununua mastaa na sio kumuingiza kinda wa kikosi cha vijana.

Ni rahisi kwake kwa sababu mbili. Kwanza mashabiki hawampi presha kwa sababu wanajua kwamba hata asipofunga bado kuna wachezaji wengi wanaweza kufunga. Mashabiki hawawezi kumpa presha kinda aliye chini ya miaka 20 wakati uwanjani kuna Fei Toto, Aziz Ki, Tuisila Kisinda, Jesus Moloko, Fiston Mayele na wengineo.

Laiti kama Mzize angekuwa anacheza na wachezaji wa ovyo basi si ajabu tusingeona makali yake. Anacheza katika kikosi ambacho kinatengeneza nafasi nyingi. Anacheza katika kikosi ambacho muda mwingi wa mchezo kinatawala mchezo. Muda mwingi wa mchezo Yanga wanakaa na mpira. Ni rahisi kwake kufurahia kucheza.

Kama angekuwa anacheza katika kikosi ambacho hakitawali mechi wala kutengeneza nafasi naamini kwamba yeye mwenyewe pia angeonekana kuwa sehemu ya tatizo. Wakati mwingine ni rahisi kumkuza kinda katika mazingira haya. Ananikumbusha mlinzi wa kulia wa Liverpool, Trent Alexander Arnold.

Trent anaweza kuwa kinda wa mwisho mwisho kukuzwa na timu kubwa na kuwa staa mkubwa klabuni pale England. Ilikuwa rahisi kwake kwa sababu kocha wake, Jurgen Klopp alikuwa ametengeneza kikosi ambacho muda mwingi kilikuwa kinatawala mchezo na kufunga mabao mengi.

Trent alikuwa ana maisha ya furaha uwanjani kama haya ambayo Mzize anayo. Ni mpaka pale Liverpool ilipoanza kupoteza makali ndipo watu wakaanza kuhoji udhaifu wake. Kwamba kumbe hakuwa mzuri katika ukabaji kuliko walinzi wenzake wa nafasi hiyo. Ni mmoja kati ya wachezaji wa England ambao walipata dakika chache pale Qatar. Hata safari yake ya kwenda Qatar ilikuwa hatihati.

Mdogo wetu Mzize tumuache kidogo. Watu wa Yanga wana furaha naye kiasi kwamba wameanza kumpa sifa nyingi zilizopitiliza. Wangempa muda aendelee kuzoea na kucheza kwa kukomaa zaidi. Ukweli ni kwamba ananifurahisha kwa namna anavyocheza. Lakini bado tutampima zaidi siku akianza kukabidhiwa Yanga. Kwa sasa Yanga ipo kwa Mayele.

Kuna presha kubwa ukikabidhiwa timu. Ni hapo ndipo unapopaswa kuonyesha ukomavu wa akili. Baadhi ya wachezaji huwa wanashindwa pale timu zinapoanza kuwategemea. Ni rahisi kuwa katika timu ambayo haikutegemei lakini sio rahisi pale unapotegemewa. Muulize vizuri Mayele pale anaposhindwa kufunga kwa mechi kadhaa mfululizo. Kichwa chake kinauma ghafla.

Mzize akianza kukabidhiwa timu pale ambapo Mayele anaweza kukosekana uwanjani kwa mwezi mmoja na nusu ndipo tutagundua ukomavu wake wa akili katika kucheza katika timu kama Yanga. Lakini pia pale Yanga watakapoanza kupoteza makali yao kwa ujumla ndipo tutaona uwezo wake wa kiakili katika kuiongoza Yanga.

Vinginevyo ni mchezaji ambaye amepata njia ya mkato (short cut) na anaonekana kuitendea haki. Tumezoea kuona hadi wachezaji wa ndani wafike hatua ya kucheza Simba au Yanga wanapaswa wawe wamezunguka katika timu zetu za mikoani kwa muda mrefu. Wakati mwingine huwa inachosha miguu yao mapema.

Kaka yangu Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ alicheza timu ya Africana ya Newala kwa miaka 10 na zaidi kisha akaenda Bandari Mtwara halafu Yanga. Kwa waliomuona msimu mmoja akicheza Bandari kisha Yanga wangeweza kudhani ni mchezaji mpya katika soka, lakini kumbe alitumika sana siku za nyuma.

Mzize anaweza kucheza muda mrefu kama hajatumika sana siku za nyuma. Zaidi ya yote ni kwamba akitimiza kipaji chake basi atakuwa amelisaidia taifa kupata mshambuliaji pale mbele. Kina Mbwana Samatta na John Bocco ndio hawa hapa wanakaribia kuondoka. Lakini pia kila siku tumezungumza namna ambavyo taifa lina wakati mgumu wa kuibua vipaji vyake.

Lakini hapo hapo itakuwa fahari kuona kuna mzawa mwingine ameibuka katika safu ya ushambuliaji ndani ya timu kubwa. Mtu pekee aliyekuwa anatuwakilisha vema kama mshambuliaji wa kati kwa klabu hizi kubwa ni Bocco ambaye umri umeanza kumtupa mkono. Wengine wakipewa nafasi huwa wanachemsha licha ya kutamba na timu za mikoani.

Kitu kikubwa kwake asisikilize sana anayoambiwa na mashabiki. Aendelee kupambana na kuwa fiti zaidi. Sina shida na uwezo wake wa kufunga, umbo kubwa, kasi na namna anavyokimbia kujitafutia nafasi ya kufunga. Yote haya yanahitaji uwe fiti. Kila la kheri kwake.

SOMA NA HII  HESABU ZA YANGA KWA MECHI ZAO ZILIZOBAKI ZIPO NAMNA HII

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here