Home Azam FC WAKIFUNGWA NA SIMBA SC AU YANGA SC TU…AZAM FC WANAKIMBILIGA HUKU…

WAKIFUNGWA NA SIMBA SC AU YANGA SC TU…AZAM FC WANAKIMBILIGA HUKU…

Simba SC na Yanga SC zilivyoifanya Azam FC kuchanganyikiwa na magolikipa

Dar es Salaam Dabi ya 30 ilimalizika hapo juzi Jumapili kwa ushindi wa 3-2 kwa Yanga SC huku kipa wa Azam FC, Ali Ahamada akigeuka kituko.

Taarifa za chinichini zinasema Azam FC imeshaanza kutafuta kipa mwingine baada ya kutoridhishwa na kiwango cha Ali Ahmada tangu ujio wake hapa nchini.

Hii ina maana kwamba maisha ya kipa huyo Mfaransa mwenye asili ya Visiwa vya Wangazija vya Comoro, yanaelekea ukingoni.

Vyanzo vya ndani vinatanabaisha kwamba ingekuwa siyo ugumu wa mkataba, Ali angefungashiwa virago baada tu ya ile mechi.

Lakini mkataba wake unasema endapo klabu itauvunja au kuukiuka, itatakiwa kumlipa Dola 300,000, zaidi ya Sh 700 milioni.

Hii ndiyo sababu hadi sasa hakuna ‘breaking news’ yoyote kumhusu kipa huyo.

Lakini hata hivyo, mpango uliopo ni kumleta kipa mwingine na yeye kuwa kipa wa akiba, tena namba tatu.

Sababu ya hili ni kumfanya akasirike na avunje mkataba yeye mwenyewe.

KISA NI SIMBA SC NA YANGA SC

Ali anakuwa kipa mwingine aliyeathirika na maisha yake ndani ya Azam FC baada ya mechi ya Simba na Yanga.

1. VLADIMIR NIYONKURU

Kipa huyu Mrundi ambaye alijiunga na Azam FC katika msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu, alianza vizuri sana akifanya okozi za hali ya juu. Lakini mechi dhidi Yanga SC ya Machi 30, 2011 ndiyo iliyomponza.

Mabao mawili mepesi ya Jerry Tegete yalitosha kuamsha hasira za wafanya maamuzi wa Chamazi na kumuondoa kipa huyo kikosini. Nafasi yake ikarithiwa na mzawa Jackson Chove.

2. DEOGRATIUS MUNISHI ‘DIDA’

Wakiwa kwenye mbio za ubingwa za 2011/12, Azam FC walikwamishwa na kipa wa Mtibwa Sugar, Deogratius Munishi katika moja ya mechi za kushangaza katika historia ya soka la Tanzania.

Mechi hii ilifanyika Chamazi na kuvunjika dakika ya 89 baada ya Mtibwa Sugar kugomea penalti na kutoka uwanjani.

Mwamuzi akawasubiri hadi akapiga filimbi ya kuuvunja mchezo.

Baada ya filimbi, wachezaji wa Mtibwa Sugar wakarudi uwanjani…refa akawa ameshamaliza kazi yake.

Likaibuka sakata la kisheria na baada ya malumbamo, na kusababisha mchezo huo uliofanyika Aprili 24, 2012, urudiwe Mei 4, 2012.

Ni hii siku ya marudiado ndipo Dida alipowatenda kitu kibaya kwa kuokoa michomo ya wazi na Azam FC kupoteza 2-1.

Azam FC ikamsajili Dida na akaanza vizuri lakini mchezo dhidi ya Simba wa Oktoba 27, 2012 ukahitimisha safari yake.

Simba SC ilishinda 3-1 mchezo huu na baadaye Dida na wenzake watatu wakatuhumiwa kutumiwa na Simba kuihujumu Azam FC.

Taarifa za ndani zilisema Dida ndiye aliyekamatwa na nyama na kuwataja wenzake, Aggrey Morris, Erasto Nyoni na Said Morad.

Wote wakasimamishwa na kupisha uchunguzi wa TAKUKURU ambao haukubaini kitu. Wote wakasamehewa kasoro Dida ambaye kimoyomoyo wafanya maamuzi waliamini ndiye aliyechora ramani…akaachwa.

3. MWADINI ALLY

Alikuwa kipa muhimu sana kwa Azam FC hasa baada ya kuondoka kwa Dida.

Lakini mechi ya Yanga ya Machi 19, 2014 ndiyo iliyoondoa umuhimu wake kikosini.

Timu ikiwa kambini kujiandaa na mchezo huo, Mwadini akaomba ruhusa aende kwao Zanzibar msibani.

Azam FC wakamruhusu lakini ni kama walihofia kitu. Wakatuma mtu hadi Zanzibar kuhakikisha kama kweli kuna msiba.

Majibu yakaja kwamba hakukuwa na wiki hiyo wala mwezi uliopita. Siyo kwa akina Mwadini wala majirani zake.

Majibu haya yakatosha kuwaaminisha wafanya maamuzi wa Chamazi kwamba Mwadini anawachezea. Siku ya mechi, Kocha Marius Omog akaambiwa asimpange…akapangwa Aishi Manula.

Hiyo ndiyo mechi ya kwanza ya Aishi kwenye Ligi Kuu akiwa na Azam na kuanzia hapo, Mwadini akapoteza namba na Aishi akatawala.

4. RAZACK ABALORA

Mrithi huyu wa Aishi Manula alianza vizuri na kuitwa mikono mia na watangazaji wa mpira hapa nchini.

Lakini mechi dhidi ya Simba SC ya Machi 4, 2020 ndiyo iliyohitimisha safari yake Chamazi.

Bao la Erasto Nyoni na lile la Kagere yalitosha kuwashawishi wafanya maamuzi wa Chamazi kuachana na huduma ya kipa huyo Mghana.

5. MATHIAS KIGONYA

Zambia walimuita safe gloves kutokana na okozi alizokuwa akizifanya akiwa klabu ndogo ya Forest Rangers.

Azam FC ilimsaini na alijitambulisha kwenye mechi dhidi ya Simba katika mchezo wa sare ya 2-2.

Aliokoa penati ya Chama na kufuta michomo mingi ya ana kwa ana. Lakini fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba SC mwaka huu kule Zanzibar ndiyo iliyomhukumu.

Wafanya maamuzi walikerwa sana na kuamua kusitisha huduma yake katika viunga vya Chamazi.

Baada ya hapo Azam FC imepitia vipindi vigumu katika idara ya ulinda mlango na ujio wa Ali Ahamada ulionekana kuwa suluhisho…lakini ndiyo kama mlivyoona.

Katika mchezo wa 2-2 dhidi ya Yanga, Ali alifanya makosa yaliyoikoa Yanga. Katika mchezo huu wa 3-2, Ali amefanya makosa yaliyowapa ushindi Yanga.

Na sasa jukumu imekuwa dhidi yake na kupita mlango uleule waliopita wenzake wakati wa kuondoka.

Na sasa Azam FC inahusishwa na makipa kadhaa wa ndani na nje, akiwemo Beno Kakolanya wa Simba ambaye mkataba wake unaisha mwishoni mwa msimu huu, yaani amebakisha miezi sita, na Djigui Diarra wa Yanga ambaye naye mkataba wake unaisha mwishoni mwa msimu huu.

Kabla ya Ali Ahmada, ilikaribia kidogo wamchukue Aishi Manula ambaye mkataba wake na Simba ulikuwa umeisha…lakini mmoja wa wakurugenzi hakutaka kuingia kwenye malumbano na Simba.

Kimsingi wakurugenzi wa Azam FC hawataki malumbano na Simba na Yanga SC ya kugombea wachezaji.

Hata usajili wa Feisal Salum haukuja kwa sababu za kiufundi, ni kwa kauli ya kukera ya Ali Kamwe kwamba matajiri wa Azam hawana hela za kumnasa mchezaji huyo.

Kama mawazo haya yangekuwepo wakati dirisha kubwa la usajili, Aishi angekuwa amesharudi Chamazi.

Lakini uvamizi wa kuangalia CV ya Ali Ahmada umewagharimu na sasa wanahaha kupata kipa mwingine…lakini yote ni kutokana na Simba na Yanga.

SOMA NA HII  KWA HAYA ALIYOSEMA OKRAH......MASHABIKI SIMBA MJIANDAE KUMWAGILIA 'MWOYO' MSIMU MZIMA AISEE...