Home Habari za michezo SIKU KADHAA BAADA YA KUTEMANA NA GEITA…MPOLE AVUNJA UKIMYA..AFUNGUKA MENGI YA NYUMA...

SIKU KADHAA BAADA YA KUTEMANA NA GEITA…MPOLE AVUNJA UKIMYA..AFUNGUKA MENGI YA NYUMA YA PAZIA…

Siku chache baada ya kuvunja mkataba na Klabu ya Geita Gold, kinara wa mabao wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, George Mpole amefichua kilichomfanya afikie uamuzi wa kuondoka kwenye timu hiyo, aliyoifungia mabao mawili hadi sasa katika ligi ya msimu huu.

Akizungumza Mpole aliyefunga mabao 17 msimu uliopita na kumpiku Fiston Mayele wa Yanga aliyemaliza na mabao 16, alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuhitaji changamoto nyingine nje na timu hiyo.

Mpole, amevunja mkataba wake uliokuwa umebaki miezi sita akisisitiza amefanya hivyo ili akasake maisha kwingine, akisema ana ofa nyingi mezani mwake na mambo yakiwa sawa kabla ya dirisha halijafungwa ataweke bayana anapokwenda kucheza, licha ya kuhusiswa na Klabu ya FC Lupopo ya DR Congo.

“Ni kweli tumefikia makubaliano ya kuvunja mkataba na mimi ndiye niliyeomba kufanya hivyo kwa kuilipa timu miezi sita iliyobaki, lengo ni kupata nafasi ya kuitumikia timu nyingine nje ya Geita,” alisema na kuongeza;

“Ninazo ofa nyingi kwa timu zinazoshiriki ligi ya ndani na nje mambo bado hayajakamilikia tukifikia makubaliano nitaweka wazi ni timu gani nitaitumikia kwa sasa ieleweke kuwa ni mchezaji huru na nipo tayari kupokea ofa za timu zinazohitaji huduma yangu.”

Mpole aliyeifungia Geita bao la kwanza kwenye mchezo dhidi ya Polisi Tanzania ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1, kisha akaongeza jingine alipoinyoa Singida Big Stars kwa 2-1, alisema bado anaamini ana nafasi ya kufanya vizuri kwenye timu yoyote atakayopata nafasi ya kuichezea.

Alisema yeye ni mchezaji maisha ni popote anachokiangalia ni ofa kubwa itakayoendana na mahitaji yake ndiyo atakayoingia nayo kwenye makubaliano na atacheza timu yoyote ambayo itaweza kumpa maslahi yake kwa wakati na si vinginevyo.

SOMA NA HII  PAMOJA NA UJIO WA KOCHA MPYA..UBOVU WA SIMBA HUU HAPA...USAJILI NA SAKATA LA MO DEWJI VYATAJWA..