Home Habari za michezo KUHUSU ALIPO MWAMBUSI…IHEFU WASHIKWA NA KIGUGUMIZI….KATWILA ‘AKODOA’ MACHO…

KUHUSU ALIPO MWAMBUSI…IHEFU WASHIKWA NA KIGUGUMIZI….KATWILA ‘AKODOA’ MACHO…

Mwambusi

Kocha Juma Mwambusi hajaonekana kwenye benchi la Ihefu katika mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu Bara, huku mabosi wa klabu hiyo wakishikwa na kigugumizi kueleza juu ya mustakabali wa kocha huyo wa zamani wa Yanga na Mbeya City.

Mara ya mwisho kwa Mwambusi kuonekana kwenye benchi la Ihefu ilikuwa ni dhidi ya Ruvu Shooting Desemba 16 mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam Complex na kushinda mabao 2-0.

Tetesi za awali zilieleza kocha huyo aliondoka baada ya kuuguliwa na mama yake na kumfanya akose mchezo dhidi ya Namungo, Mtibwa Sugar na KMC na michezo hiyo ikaongozwa na kocha msaidizi, Zubery Katwila.

Mwambusi alipotafutwa alisema yupo katika kikao, kisha akasisitiza kama kuna lolote la Ihefu atafutwe Katwila, ambaye alipoulizwa alisema anayepaswa kujibu ishu ya kocha mkuu ni mabosi wa klabu na sio yeye kwani naye (Katwila) ni muajiriwa kama yeye (Mwambusi).

Hata hivyo, katibu mkuu wa timu hiyo, Zagalo Chalamila alipoulizwa na Mwanaspoti hakuweza kuweka wazi kama kocha huyo bado wapo naye au wameshaachana naye kwa kuwa hakuna taarifa inayoeleza tangu kuondoka kwake.

“Tutatoa taarifa rasmi juu ya hilo muda utakapofika kama yupo au tumeachana naye, lakini kwa sasa tuliache kama lilivyo, ila mambo mengine yanaendelea kwenye timu vizuri ikiwemo mchakato wa usajili wa wachezaji nao tunalifanyia kazi,” alisema Chalamila.

Mmoja wa watu wa ndani wa timu hiyo alisema kuna mgawanyiko wa viongozi ambao wanataka Mwambusi aondoke na wengine abaki lakini wengi wanataka aondoke sababu ya misimamo yake mikali.

“Tatizo la kwanza linaanza kwa wachezaji wanaomlalamikia kocha anawapa mazoezi magumu tofauti na walivyomzoea Katwila, pia baadhi ya viongozi walionekana kuingilia mambo ya kiufundi, kitu ambacho Mwambusi hakupendezwa nacho,” kilieleza chanzo hicho kilichoomba kuhifadhiwa jina.

Katwila amekuwa ndani ya kikosi hicho tangu msimu wa juzi akitokea Mtibwa Sugar na akashuka nayo daraja Ihefu lakini msimu huu amefanikiwa kuipandisha na kuanza vibaya kwa msimu ndipo mabosi wakamtambulisha, Mwambusi kama kocha mkuu.

Ihefu inayoshika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 20 kwa sasa inajiandaa kuikabili Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Januari 16 huku mchezo wa duru la kwanza Ihefu ikiivunja rekodi ya Yanga ya kucheza mechi 49 bila ya kupoteza kwa kuifunga mabao 2-0 pale Highland Estate.

SOMA NA HII  ABDI BANDA - SIMBA WANATUMIA MBINU CHAFU NA WANASIASA KUSHINDA MECHI ZA KIMATAIFA...