Home Habari za michezo MITIHANI MIZITO 6 YA MBRAZILI NDANI YA SIMBA….MGUNDA AMPA TUMBO JOTO…

MITIHANI MIZITO 6 YA MBRAZILI NDANI YA SIMBA….MGUNDA AMPA TUMBO JOTO…

Habari za Simba SC

Kambi ya wiki moja iliyoweka Simba huko Dubai, itamsaidia kocha mpya Oliviera Robertinho kuwajua wachezaji wake kabla ya kuanza majukumu ya mechi za Ligi Kuu Bara na michuano ya CAF, ambayo itaonyesha huyu ni kocha wa namna gani, aidha atabaki au inaweza kuondoka naye.

Imesalia michezo 11 ya Ligi Kuu Bara ambapo Robertinho atatakiwa kukusanya pointi 33, akipokea kijiti kutoka kwa mzawa Juma Mgunda ambaye chini yake ilichezwa michezo 16, alishinda mechi 11, sare nne, ilipoteza mmoja dhidi ya Azam na ilikusanya pointi 37.

Baada ya kocha huyo kutua alipewa kazi ya kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutwaa ubingwa wa Kombe la FA, ambapo kwenye michezo hiyo mitano kama atapoteza ni dhahiri kuwa itakuwa ngumu kwake kutimiza malengo hayo.

Chini ya Mgunda safu ya ushambuliaji ilitengeneza mabao 38, pia safu yake ya ulinzi haijamuangusha katika mechi 16, imeruhusu mabao manane tu jambo ambalo linaonekana kuwa mfupa mgumu kwa kocha huyo mpya kwani amekuja wakati timu ikiwa kwenye moto.

Baada ya Simba kurejea nchini, Januari 17 itacheza dhidi ya Mbeya City, timu hizo raundi ya kwanza zilitoshana nguvu kwa sare ya bao 1-1 mchezo uliopigwa Novemba 23/2022, Uwanja wa Mkapa, kazi itakuwa kwa kocha Robertinhos, kupata kati ya matokeo matatu, ushindi, sare ama kufungwa.

Simba itakuwa mwenyeji wa Singida Big Stars Januari 22, baada kupata sare ya bao 1-1 mechi ya mzunguko wa kwanza(Nov 11/22), na itaifuata Dodoma Jiji Februari 3, ambayo ilichapwa Uwanja wa Mkapa mabao 3-0 (Oktoba /22). Kisha itafuata michuano ya CAF.

Ambapo kocha huyo atapaswa kuangalia rekodi ya Mgunda ambaye alishinda mechi zote za CAF, hivyo atapaswa kuendeleza pale alipoishia mtangulizi wake akishindwa kelele zitakuwa nyingi. Mechi ambazo Mgunda alishinda CAF ni dhidi ya Big Bullets 0-2 Simba (Sept 10/2022), Simba 2-0 Big Bullets (Sept 14/2022)

Primeiro de Agosto 1-3 Simba (Oktoba 9/2022), Simba 1-0 Primeiro de Agosto (Oktoba 16/2022). Robertinho mbele yake ana majukumu dhidi ya Horoya AC ya Guinea, mchezo utakaopigwa ugenini kati ya Februari 10 na 11, Raja Casablanca Uwanja wa Mkapa kati ya Februari 17 au 18 na timu yake ya zamani Vipers ya Uganda itakuwa ugenini kati Februari 24 au 25.

Wakati kocha huyo anatambulishwa aliahidi kuifikisha Simba hatua ya nusu fainali na ikiwezekana fainali, “Naahidi kuifikisha timu nusu fainali ama fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika.” Watalamu wa soka walimulika jicho kulingana na ujio wa kocha huyo mpya, kwamba yapo mambo yatabadilika kikosini kulingana na mifumo yake.

Beki wa zamani wa timu hiyo, Kasongo Athumani Mgaya alisema aina ya ufundishaji wa Mgunda hautakuwa sawa na Robertinho :”Wazungu mara nyingi wanapenda mchezaji azingatie zaidi mfumo, tofauti na wazawa ambao wanamuacha huru mchezaji, hapo lazima baadhi yao watakaa benchi.”

Hoja yake iliungwa mkono na kipa wa zamani wa Simba na Yanga, Steven Nemes aliyesema :”Ni kazi ya wachezaji kuisoma kwa haraka mifumo ya kocha kisha waendane naye, maana hawana chaguo zaidi ya kukifanyia kazi kile kitakachokuja mbele yao kwani timu nyuma ilifanya vizuri.”

SOMA NA HII  MAN CITY, CHELSEA MAMBO SIO MAMBO TENA