Home Habari za michezo SAKATA LA FEI TOTO KUITEMA YANGA SC…ABDI KASSIM KAIBUKA NA HILI LA...

SAKATA LA FEI TOTO KUITEMA YANGA SC…ABDI KASSIM KAIBUKA NA HILI LA KWAKE…

Tetesi za Usajili Yanga

SAKATA la kiungo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutaka kuondoka Yanga SC limemuibua kiungo na nahodha wa zamani wa timu hiyo, Abdi Kassim ‘Babi’ ambaye ameishauri klabu hiyo kumuachia mchezaji huyo akatafute changamoto mpya hususani nje ya nchi.

Babi ambaye enzi zake alijulikana kwa jina la Ballack wa Unguja ni mchezaji wa zamani wa timu za taifa za Tanzania na Zanzibar, huku akifanikiwa kucheza soka la kulipwa nchini Vietnam na Malaysia kabla ya kugeukia ukocha.

Sakata la Fei Toto kuondoka Yanga SC lilianza Desemba 23, kwa nyota huyo kuhusishwa kutua Azam na baadaye akawaaga mashabiki wa timu hiyo kupitia kurasa za mitandao yake ya kijamii, lakini mabosi wa Yanga SC wameweka ngumu wakisisitiza bado ni mchezaji wao halali na yeyote anayemtaka aende kwa mazungumzo.

Kocha huyo wa zamani wa Mashujaa FC ya Kigoma ambaye kwa sasa yuko kwao Zanzibar, alisema Yanga SC inapaswa kuachana na utamaduni wa kuwabania wachezaji wake wanapotaka kutafuta changamoto mpya.

Alisema ni wakati wa nyota huyo kwenda nje ya nchi na Yanga SC inapaswa kukaa mezani na kumalizana naye kwani ameshaonyesha nia ya kutotaka kuendelea kukaa klabuni hapo akitaka kubadili mazingira na kusaka maslahi mazuri zaidi.

“Mimi naona ni jambo la uamuzi kwa upande wa Fei kwa maana amekaa Yanga na anaijua vizuri mpaka anataka kuondoka basi anahitaji kubadilisha mazingira na maslahi kwa ujumla.

“Nashauri Yanga SC imruhusu aondoke akatimize ndoto zake huko anapopataka, wanatakiwa waangalie pande zote mbili ikiwemo ya Feisal siyo wanaangalia upande wao tu, mbona wakitaka kuvunja mkataba na kocha au mchezaji huwa wanakaa kikao na kukubaliana?” alisema Babi.

Alisema kinachomkumba Fei Toto kimewahi kumtokea wakati anacheza Yanga alipopata ofa ya kucheza nje ya nchi ambapo aliwekewa ngumu na klabu hiyo, hivyo imekuwa ni utamaduni wa Yanga SC kutowapa baraka wachezaji wake.

“Hiyo ndiyo tabia ya Yanga SC hata mimi walinilipa vikwazo sana kuondoka hapo wakati natakiwa niende Vietnam kucheza soka la kulipwa mwaka 2009, japokuwa baadaye waliniruhusu lakini kwa kutumia njia ya fedha iliyobaki Sh6 milioni ya usajili nikawaambia nawapa wao ndiyo nikapewa barua.”

SOMA NA HII  RASMI LIGI KUU BARA KUITWA NBC PREMIER LEAGUE