Home Habari za michezo ROBERTINHO MAJI YA SHINGO SIMBA…MABOSI WATAKA MKATABA WAKE UVUNJWE…ISHU NZIMA IKO HIVI…

ROBERTINHO MAJI YA SHINGO SIMBA…MABOSI WATAKA MKATABA WAKE UVUNJWE…ISHU NZIMA IKO HIVI…

Habari za Simba

Kocha Mkuu wa Simba, Mbrazil, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ juzi Jumanne usiku aliwagawa viongozi wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, baadhi yao wakishinikiza avunjiwe mkataba.

Tukio hilo la aina yake lililotokea mara baada ya mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba dhidi ya Azam FC uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, uliochezwa juzi Jumanne kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

Awali uongozi wa Simba ulimpa kocha huyo mechi tatu za kushinda ili hatma yake ijulikane ikiwemo dhidi ya Azam FC na michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakaocheza na Vipers SC ugenini kabla ya kurudiana nyumbani.

Mmoja wa mabosi wa Simba, ametupenyezea kuwa, kocha huyo mara baada ya mchezo dhidi ya Azam baadhi ya viongozi walishinikiza avunjiwe mkataba wa miaka miwili aliosaini Januari 3, mwaka huu.

Bosi huyo alisema viongozi wametaka Robertinho aondoke, kisha Kocha Msaidizi, Juma Mgunda akabidhiwe timu amalizie michezo ya ligi na kimataifa iliyobaki.

Aliongeza kuwa, hadi kufikia jana Jumatano, viongozi hao walikuwa wakiendelea na vikao vya kuamua hatima ya kocha huyo baada ya kuonekana kushindwa kutimiza makubaliano yaliyokuwepo katika mkataba.

“Ni mipango ya Mungu pekee itakayoamua kumbakisha Robertinho, kwani tayari baadhi ya viongozi wamegawanyika hadi hivi sasa, wapo wanaotaka avunjiwe mkataba mara baada ya mchezo wa ligi dhidi ya Azam.

“Lakini wapo wale ambao wametoa michezo miwili ya kimtaifa dhidi ya Vipers wa ugenini kabla ya kurudiana nyumbani ambayo kocha huyo aliwekewa malengo ya kushinda yote, mwingine huu wa Azam ambao tumepata sare.

“Sare hiyo dhidi ya Azam imewakera baadhi ya viongozi na kufikia hatua ya kutaka avunjiwe mkataba na timu apewe Mgunda amalizie michezo iliyobakia,” alisema bosi huyo.

Hivi karibuni, Robertinho mara baada ya mchezo dhidi ya Raja Casabalanca, aliwaomba mashabiki na viongozi kumpa muda wa kukiandaa kikosi chake akisema: “Nimekosa muda mzuri wa kukiandaa kikosi changu, tangu nimekabidhiwa timu tumekuwa na michezo ya mfululizo ya kimashindano, hivyo naomba nipatiwe muda kuiandaa timu.”

SOMA NA HII  METACHA NDIO BASI TENA YANGA....GAMONDI 'ASIMAMIA UKUCHA' JAMBO LAKE...