Kikosi cha Azam FC kitacheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Gor Mahia FC ya Kenya, kwa ajili ya kujiandaa na Michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyosalia msimu huu, pamoja na mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ dhidi ya Mtibwa Sugar.
Azam FC imethibitisha uwepo wa mchezo huo kupitia kurasa zake za Mitandao ya Kijamii, baada ya Benchi la Ufundi kupendekeza kuchezwa kwa michezo hiyo angalau miwili katika kipindi hiki cha Kalenda ya FIFA.
Mchezo huo dhidi ya Gor Mahia umepangwa kuchezwa Jumamosi (Machi 26) katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi nchini Kenya.
Kabla ya mchezo huo Azam FC itacheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya JKU kutoka visiwani Zanzibar kesho kutwa Jumatano (Machi 22), katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Benchi la Ufundi Azam FC Dani Cadena amesema wamelazimika kukitumia kipindi hiki kwa mchezo huo, ili kuwaweka sawa wachezaji wao waliosalia kikosini, baada ya wenzao kumeitwa kuziwakilisha timu zao za taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Cadena amesema kutakuwa na muda mrefu kwa wao kutocheza, hivyo wameona ni vyema kutotoa ruhusa ya mapumziko kwa lengo la kurejesha morali ya timu yaobaada ya kusuasua hivi karibuni.
“Ruhusa ambayo tumeitoa ni kwa wachezaji walioitwa timu za taifa, wengine wote tutaendelea na mazoezi kwa lengo la kujiweka imara zaidi kutokana na michezo migumu iliyokuwa mbele yetu,” amesema Dani Cadena