Home Michezo MABOSI WA YANGA WAWEKA MIL 150 MEZANI…WACHEZAJI WALIPWA BONUS ZAO ZOTE

MABOSI WA YANGA WAWEKA MIL 150 MEZANI…WACHEZAJI WALIPWA BONUS ZAO ZOTE

MABOSI WA YANGA WAWEKA MIL 150 MEZANI...WACHEZAJI WALIPWA BONUS ZAO ZOTE

YANGA ina dakika 90 za kuthibitisha ubora wao kwenye Kombe la Shirikisho Afrika itakapoikaribisha US Monastir ya Tunisia, huku mastaa wa timu hiyo wakiwapiga mkwara wapinzani wao kuwa leo ndio watajua hawajui, kwani wanapigwa mapema tu Kwa Mkapa.

Mechi hiyo ya kisasi itapigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwa Mkapa baada ya awali, Yanga kulala ugenini kwa mabao 2-0 na ikitoboa baada ya dakika 90 hizo za kibabe itafuzu moja kwa moja robo fainali bila hata kusubiri pambano lijalo la kufungia Kundi D dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.

Yanga inashika nafasi ya pili kundini ikiwa na pointi saba, ikiwa nyuma ya Monastir iliyotangulia robo mapema ikiwa na pointi 10 hadi sasa, huku Mazembe inayovaana na Real Bamako ugenini ni ya tatu na alama zao nne na wenyeji wa mchezo huo wa Bamako ina pointi mbili.

Dakika za pambano hizo zinaonekana kuwa kwa Yanga zaidi kwani wapinzani wao hawana cha kupoteza na tayari benchi la ufundi la timu hiyo limesema kuna baadhi ya mastaa wao hawatacheza kwa sababu tofauti kitu kilichowapa mzuka wenyeji waliowekwa mamilioni mezani.

Mtego wa Yanga ni kwamba licha ya kujua Monastir imefuzu lakini kosa lolote la kushindwa kushinda mchezo huu, utaiweka rehani ndoto yao ya kufuzu robo fainali endapo Mazembe atashinda ugenini dhidi ya Real Bamako na kulifanya pambano la mwisho baina yao Aprili 2 kuwa gumu zaidi kwao.

Wakiwa mazoezini Yanga ilifanya mazoezi makali ya mbinu kwanza wakipewa mbinu nyingi za kukabiliana na Monastir kwa kuzuiwa kabisa kuona mtu anaruka bila kusumbuliwa lakini kuhakikisha hawatengenezi mipira mingi ya adhabu karibu na lango lao.

Kule mbele sasa Yanga imekuwa ikijipanga kwa soka la kasi na kutakiwa kutumia nafasi wakijua kwamba waarabu wao watashuka uwanjani bila kipa wao namba moja Ben Said ambaye ana kadi mbili za njano, ambaye amekuwa kizuizi kikubwa kwa timu yake kufungwa kutokana na umahiri wake.

Msimu huu ni mechi moja tu kwa Yanga ilicheza na kumaliza dakika 90 bila kufunga bao dhidi ya Club Africain hapa nyumbani, lakini zingine zote wamefunga mabao na leo itategemea utulivu na shabaha ya washambuliaji wao kinara Fiston Mayele na Kennedy Musonda waliotengeneza kombinesheni ya kibabe hadi sasa.

Pambano hilo litachezeshwa na waamuzi kutoka Chad akiwemo Alhadi Mahamat, akisaidiwa na Bogole Issa na Issa Yaya huku mezani atakuwepo Pousri Alfred.

Nje ya uwanja Wananchi wataitika wito wa uongozi wao chini ya Ofisa Habari, Ally Kamwe ambaye kwa wiki nzima amekuwa akihamasisha sambamba na viongozi wake wa juu kuhakikisha mashabiki wanajaa uwanjani, mpaka jana hali ilikuwa inaonyesha mashabiki watakuwa wengi uwanjani wakiwa na hamasa ya matokeo ya kushinda mfululizo nyumbani.

Kabla ya mchezo wa leo wachezaji wa Yanga hakuna atakayekuwa hana noti yoyote kwenye pochi yake kwani wamelipwa bonasi zao lakini Tunafahamu kuwa matajiri wao wataweka kiasi kisichopungua sh 150 milioni mezani kama watashinda.

Mzuka huo utawafanya wachezaji wa Yanga leo kuwa na akili mbili tu kuhakikisha hawaruhusu bao  pia wanalishambulia lango la Monastir kama nyuki kusaka mabao.

Kocha wa Yanga Nasreddine Nabi alisema katika mchezo huo ambao utakuwa sawa na fainali kwao wataingia na tahadhari zote lakini kitu kikubwa watahakikisha wanakuwa na utulivu kuweza kutumia nafasi za kupata matokeo.

Nabi alisema wamekuwa na wiki ya mazoezi makali ya kujipanga katika ulinzi lakini pia jinsi ya kutumia makosa ya Monastir kuweza kusaka ushindi kabla ya kwenda kucheza mchezo wa mwisho.

“Hii ni mechi kubwa na muhimu kwetu, nadhani kama makocha tumemaliza kazi yetu mazoezini, hii ni nafasi ya wachezaji kwenda kuamua hatma ya timu yao kushinda, tunaweza kushinda licha ya kwamba tunajua haitakuwa rahisi, kitu ambacho wachezaji wangu wanatakiwa kukifanya ni kuongeza utulivu na kutumia nafasi,” alisema Nabi.

“Hii ni fainali kwetu ili tuweze kuwa sawa na malengo yetu, tumekuwa na wiki nzuri ya maandalizi, tumekumbushana juu ya mapungufu yetu nadhani timu ipo tayari kwa mchezo wetu huu muhimu.

Kocha wa Monastir Mserbia Darko Novic jana akizungumza na waandishi wa habari alisema timu yake haina presha yoyote kuekelea mchezo huo kwa kuwa wameshafuzu hatua inayofuata wataingia na akili mionja tu kulinda heshima yao.

“Huu ni mchezo tofauti na ule ambao tulicheza Lubumbashi  (dhidi ya TP Mazembe) ulikuwa ni wakati mgumu kwetu lakini kesho (leo) hatutakuwa na kazi ngumu kwa kuwa tumeshafuzu, tutaingia bila presha ya matokeo tunaamini itakuwa ni mechi ngumu lakini sisi tunaangalia hatua inayofuata sasa,”alisema Novic

SOMA NA HII  HII HAPA RATIBA YA MICHEZO YOTE YA LIGI KUU YA NBC KWA SIKU YA KESHO....

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here