Home Habari za michezo PAMOJA NA KUFUNGWA NA YANGA JUZI….WATUNISIA WASEPA NA MAYELE…MCHONGO UKO HIVI…

PAMOJA NA KUFUNGWA NA YANGA JUZI….WATUNISIA WASEPA NA MAYELE…MCHONGO UKO HIVI…

Habari za Yanga

Wakati Kocha Mkuu wa US Monastir ya Tunisia, Darko Novic, akiondoka na jina la Fiston Mayele, akidai ndiye aliyefanya mambo kuwaharibikia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi, Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema kazi bado haijaisha kwani lengo lake ni kuona wanamaliza kileleni mwa msimamo wa Kundi D.

Yanga ikiwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi, iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya US Monastir kwenye mchezo wa hatua ya makundi wa Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo kukaa kileleni mwa msimamo wa Kundi D kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kutokana na kufikisha pointi 10 sawa na Watunisia hao.

Akizungumzia mchezo huo Kocha wa US Monastir, Novic, alisema mechi ilikuwa ya ushindani mkubwa na kwamba wachezaji walipambana, lakini haikuwa bahati kwao kupata matokeo.

Alisema mchezo huo ulikuwa mgumu kwao kutokana na uwezo wa mshambuliaji wa Yanga, Mayele ambaye aliifanya safu yake ya ulinzi kuwa na wakati mgumu katika kuhakikisha wanamchunga.

“Yanga ni timu nzuri, ina wachezaji wazuri ukizingatia wale wanaocheza pembeni, lakini kama nitapata nafasi ya kuchagua mchezaji mmoja kwenda naye robo fainali basi nitamchukua yule straika (Mayele),” alisema Novic.

Katika mchezo huo, Mayele alifunga bao la pili akimalizia pasi ya upendo ya Mzambia Kennedy Musonda ambaye licha ya kutoa asisti hiyo pia ndiye aliyetupia bao la kwanza nyavuni.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga, Nabi yeye ameanza kupigia hesabu pointi tatu katika mchezo wa mwisho dhidi ya TP Mazembe, huku akisema lengo lao ni kuongoza kundi lao hadi mwisho.

Hii ni mara ya kwanza kwa Yanga kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho na mafanikio makubwa waliyokuwa nayo kwenye michuano hiyo ilikuwa ni kuishia hatua ya makundi tena ikimaliza mkiani mara mbili mwaka 2016 na 2018.

Nabi aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana dhidi ya US Monastir na kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali wakiwa na mchezo mmoja mkononi, lakini akasema bado hawajamaliza kazi.

Alisema mchezo ulikuwa wa ushindani mkubwa na ndani ya dakika 90 walitawala, hivyo wachezaji walifanya kitu kizuri kwa kupata ushindi huo uliowavusha na kusonga mbele kucheza robo fainali.

“Hatutaishia hapo tunatakiwa kupambana na kuheshimu mpira kwa ajili ya kusonga mbele, Tunaenda kucheza na TP Mazembe huku US Monastir wakimpokea Real Bamako nyumbani, tunatakiwa kupambana kupata pointi tatu ili tumalize kundi tukiwa juu,” alisema Nabi.

Aidha, kocha huyo alisema alimtumia Ibrahim Abdallah (Bacca) kwa sababu ya uwezo wake wa kupiga mipira ya kichwa kwa kuwa US Monastir wanauwezo wa kucheza mipira juu, iliyokufa na kona kwa ufanisi mkubwa.

Kwa mara ya kwanza Bacca alipata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga katika mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya US Monastir ambapo alicheza sambamba na Bakari Mwamnyeto.

“Baka anakuja na kufanya vizuri siku hadi siku ndio maana ameingia katika kikosi kuna vitu anatakiwa kuongeza kwa sababu ya ukabaji wake,” alisema Nabi aliongeza:

“Nawapongeza Simba pia kwa kutinga robo fainali hii ni ishara kubwa kwa mpira wa Tanzania, unakuwa na unapiga hatua kubwa na sasa ni muda wa kujipanga kwa mechi zijazo,” alisema kocha huyo.

SOMA NA HII  KAMATA MIL 5 KIULAINII KWA KILA MKEKA UTAKOWEKA KUPITIA SLOT YA ENDORPHINA YA MERIDIANBET..