KILA mmoja hawezi kuamini kile ambacho Stars watakifanya leo wakati watakapokuwa wakivaana na Uganda kwenye mchezo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa Afrika AFCON 2023.
Huu ni mchezo wa pili Stars wanavaana na Uganda baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Misri wiki iliyopita, Stars kuibuka na ushindi wa bao 1-0 na kukaa kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa kundi D.
Stars itaingia uwanjani leo saa 2:00 kwenye uwanja wa nyumbani, Benjamin Mkapa ikiwa inahitaji matokeo ya aina moja tu yaani ushindi ili kuendelea kuwa na matumaini ya kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2023) yatakayofanyika mwakani nchini Ivory Coast.
Stars katika hatua hii ya kuwania kufuzu michuano hiyo mikubwa barani Afrika imepangwa kundi D ikishika nafasi ya pili baada ya kucheza mechi tatu na kuvuna pointi nne nyuma ya vinara Algeria wenye alama tisa huku Niger ikiwa ya tatu na pointi 2 na Uganda ikiburuza mkia na alama moja, lakini hii ikiwa ni kabla ya mechi ya jana kati ya Niger na Algeria.
HESABU ZIKO HIVI
Kama Stars itashinda mechi ya leo itafikisha alama saba na kubakiza mechi mbili nyumbani dhidi za marudiano dhidi ya Algeria ambayo katika mechi ya kwanza Stars ilichapwa 2-0 ugenini na mchezo mwingine utakuwa dhidi ya Niger ambayo kwenye mchezo wa kwanza walitoka sare ya bao 1-1 na jana trimu hizo zilikutana pamoja.
AMROUCHE ATAAMUA
Kimbinu kutokana na namna kocha mkuu wa Stars, Adel Amrouche alivyopanga kikosi chake kwenye mechi iliyopita bado Stars inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda mbele ya Uganda licha ya kwamba imekuwa ikiwasumbua mara kwa mara.
Amrouche kule Misri alianza na kipa Aishi Manula na mabeki Dickson Job aliyecheza kulia na Novatus Dismas kushoto huku Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca wakisimama katikati na timu kuonekana kucheza vizuri kwenye eneo la ulinzi.
Eneo la kiungo walianza Himid Mao, Mzamiru Yassin na Mudathir Yahya huku washambuliaji watatu wakiwa ni Simon Msuva, Said Junior na Mbwana Samatta na jambo lingine la kufurahisha ni baada ya kocha huyo kuwaongeza wachezaji wawili wazoefu, Mohammed Hussein na Shomary Kapombe kwenye kikosi hicho kuelekea kwenye mchezo huu ambao Uganda wanautolea macho pia.
MECHI IKO HAPA
Ukiachana na mbinu za makocha Amrouche na Milutin Sredojevic ‘Micho’ wa Uganda, lakini pia mechi hii inaweza kuamuliwa na ubora wa mchezaji mmoja mmoja au kundi katika nafasi zao.
Stars kwenye mechi iliyopita ilionekana kuwa imara zaidi kwenye eneo la kiungo walipocheza Mao na Mzamiru wakiwapiku viungo wa Uganda waliokuwa wakiongozwa na staa wa Yanga, Khalid Aucho.
Uganda ni imara zaidi kwenye safu ya ushambuliaji inayoongozwa na mkongwe Emmanuel Okwi na Farouk Miya hivyo mabeki wa Stars ambao watapata nafasi wanatakiwa kuwa makini zaidi na watu hao bila kumsahau Fahad Bayo ambaye ni hatari eneo la mbele, lakini iwe isiwe Uganda watakufa kwa Mkapa leo.
CHUKUA HII
Pamoja na kushinda mechi iliyopita, rekodi zinaonekana Stars imekuwa mnyonge kwa Uganda kwani katika mechi 20 zilipokutana Uganda imeibuka na ushindi mara 12 na Stars kushinda nne tu, ikiwemo ya juzi huku nne zikimalizika kwa sare.
Lakini pia Stars imeichapa Uganda mechi mbili zilizopita mfululizo kwa ushindi wa bao 1-0 lakini katika mechi tano za hivi karibuni timu hizo zilipokutana kiujumla wake Stars imeshinda mbili na Uganda kushinda tatu na katika mechi hizo timu iliyoshinda haikuruhusu bao hata moja.
WASIKIE WENYEWE
Kocha Amrouche amesema kikosi chake kimejipanga kushinda mechi ya leo na kila mchezaji anamorali nzuri huku akiwataka kucheza zaidi kitimu akiamini kuwa wanaweza kuichapa Uganda.
“Wamekutana wachezaji kutoka klabu mbalimbali lakini kikubwa wanatakiwa kucheza kitimu. Tumejiandaa kushinda na kila mchezaji anajua umuhimu wa mchezo huu kwetu,” alisema Amrouche ambaye mechi ya leo itakuwa ya pili kwake tangu ameichukua Stars mapema mwezi huu.
Kwa upande wa Uganda, Micho alisema walikutana na mechi ngumu katika mchezo uliopita lakini kwa sasa hawataruhusu tena makosa na wanachohitaji ni ushindi tu.
“Mechi iliyopita tulicheza vizuri lakini tukafanya makosa kadhaa yaliyotugharimu, hapa Tanzania naamini tutacheza vizuri na lengo ni kushinda tu”, alisema Micho, Mserbia mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika na mwaka 2007 aliwahi kuinoa Yanga.
Nahodha wa Stars, Samatta aliwaita mashabiki uwanjani huku akiahidi ushindi kwa Watanzania.“Tumeona juhudi za watu mbalimbali katika mechi hii, tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani kutusapoti na sisi tupo tayari kupambana na kuipatia nchi ushindi, hii itakuwa mechi nyingine ya rekodi kwetu,” alisema Samatta anayeichezea klabu ya Genk ya Ubeliji.
Jumla hadi jana, wadau na serikali walikuwa wameshanunua tiketi 31, 000 huku Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa imenunua tiketi 20,000 na wadau wengine wakiwa wamenunua 11,000 ambazo zitagawiwa kwa mashabiki leo.
msimamo
GROUP F
P PTS
Algeria 3 9
Tanzania 3 4
Niger 3 2
Uganda 3 1
MECHI ZIJAZO JUNI
Tanzania vs Niger
Uganda vs Algeria
Septemba
Niger vs Uganda
Algeria vs Tanzania