Home Habari za michezo BAADA YA KICHAPO CHA SIMBA…NABI AFUNGUKA HAYA..AMTAJA AZIZ KI

BAADA YA KICHAPO CHA SIMBA…NABI AFUNGUKA HAYA..AMTAJA AZIZ KI

Habari za Yanga SC

BAADA ya kukubali kichapo cha mabao 2-0, kutoka kwa Simba, kocha mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema alikuwa na sababu kubwa ya kumweka nje Stephen Aziz KI, lakini hilo limeisha na haliwazi tena kwani sasa amehamishia akili zote kwenye mechi ya kwanza ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika ugenini dhidi ya Rivers United.

Nabi amesema licha ya kufungwa na Simba, bado anaamini timu yake ni bora na haijapoteza muelekeo kwani bado inaongoza ligi ikiwa na nafasi ya kutwaa ubingwa lakini pia inaweza kufanya vizuri katika michuano mingine inayoshiriki ikiwemo Kombe la Shirikisho Afrika.

“Mechi na Simba imeisha na tumepoteza pamoja na kuna baadhi ya maamuzi hayakuwa sahihi ikiwemo kona iliyozaa bao la kwanza.

“Yote kwa yote tunaipongeza Simba kwa ushindi kwani mpira ndivyo ulivyo na sasa tunajipanga na mechi ijayo dhidi ya Rivers,” alisema Nabi na kuongeza;

“Hatutakiwi kuwa vichwa chini na kunyoosheana vidole, bado tupo kwenye njia yetu katika ubingwa wa ligi na mashindano mengine. Wachezaji wetu ni bora na wanaweza kufanya vizuri katika mechi zijazo na kutupa matokeo chanya.”

Pia kocha huyo raia wa Tunisia alisema mabadiliko aliyoyafanya kwenye kikosi kilichocheza na Simba yalikuwa ya kiufundi huku akisisitiza kutotaka kuwepo kwa matabaka baina ya wachezaji wake.

“Tulichagua kuanza na Bangala (Yanick), Aucho (Khalid) na Salum (Sure Boy) eneo la kiungo na baadaye tulivyoona tumezidiwa tuliwangiza Aziz Ki, na Mudathir (Yahya) ambao walirudisha uhai katika timu na kuleta ubora eneo la kati lakini kwa bahati mbaya tulitengeneza nafasi tulizoshindwa kuzitumia na mechi kumalizika hivyo.

“Kwa Aziz KI kutokuanza yalikuwa masuala ya kiufundi tu, huyu ni mchezaji mzuri lakini niliona kuwa haikuwa mechi muhimu sana kuanza, huko mbele bado tuna michezo mingine mingi,” alisema.

Nabi alisema tayari amepata mafaili ya Rivers na kushirikiana na wataalamu wengine kwenye benchi la ufundi la Yanga wameanza kuwasoma na kujua ubora na upungufu wao.

“Kila mechi ina mpango wake kutokana na mpinzani unayeenda kukutana naye, Rivers ni timu nzuri na tumeanza kuisoma.

“Tunataka tujue wapi ni bora na wapi ni dhaifu ili tujue tunaingiaje na kazi hiyo tunaifanya kwa umakini mkubwa kwa kushirikiana na wataalamu wengine,” alisema Nabi raia wa Tunisia

Baada ya mechi na Rivers ugenini, Yanga itarejea nchini kusubiri mechi ya marudiano itakayopigwa Aprili 30 mwaka huu na baada ya hapo mshindi wa jumla atatinga nusu fainali ya michuano hiyo ambayo bingwa mtetezi ni RS Berkane kutoka Morocco.

SOMA NA HII  HUKO SIMBA MAMBO NI MOTO, KIPA MPYA HUYU HAPA KUTUA KABLA YA SIMBA DAY