Home Habari za michezo REDONDO :- MAFISANGO ALIKUWA HAITAKI TENA SIMBA…SIKU YA KIFO CHAKE ‘TULIFURAHI MNOO’..

REDONDO :- MAFISANGO ALIKUWA HAITAKI TENA SIMBA…SIKU YA KIFO CHAKE ‘TULIFURAHI MNOO’..

Habari za Michezo

Kama kuna nyakati ngumu kwa kiungo wa Polisi Tanzania, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ ni kusimulia ishu ya kifo cha rafiki yake kipenzi, Patrick Mafisango aliyefariki dunia Mei 17, 2012.

Marehemu Mafisango na Redondo walikuwa zaidi ya marafiki, walijiita ‘Brothers’ walipanga mipango mingi ya maendeleo ya kisoka na maisha kwa jumla.

Anasimulia siku mbili kabla ya kifo cha Mafisango alimwambia wanatakiwa kwenda kucheza Ufaransa na aliamini ni rahisi kutoboa kimaisha, huku akimsisitiza kutocheza tena Ligi Kuu Bara.

“Angekuwa hai sidhani kama tungekuwa Tanzania, kwani alikuwa na ndugu zake Ufaransa na alisema hata soka lingetushinda tungetoboa kimaisha kwa kufanya mishe nyingine, hakupenda kuona nakosa furaha, kila aliyekuwa karibu yake muda wote alicheka, alikuwa mcheshi sana.

“Bado nawasiliana na baadhi ya wadogo zake ambao wapo Ufaransa na kuhusu mtoto wake wa kiume Haruna Niyonzima ndiye yupo karibu zaidi ingawa nampigiaga simu kujua hali yake mara moja moja.”

SIKU YA KIFO CHAKE ALIKUWA NAYE

Anasimulia ilivyokuwa; “Ishu ilikuwa hivi, Ligi Kuu ilikuwa imeisha alinipigia tukakutana tukala msosi pamoja, akaniambia ameitwa timu ya taifa Rwanda, akasema ataenda huko kisha ataenda Congo kwao, pia aliniambia kesho twende tukafurahie maisha.

“Siku ilipofika nilikwenda kwake saa 2:00 asubuhi muda ambao haikuwa kawaida yangu kwenda kwake, tukapanga ratiba ya kutoka, pia ilikuwa ni siku ambayo alitakiwa kuongeza mkataba Simba lakini akasema hawezi kuchukua pesa yao, kwani hajioni kucheza Ligi Kuu tena, wakati huo na mimi nilikuwa natoka Azam FC kwenda Simba kwa lengo la kucheza naye.

“Tulikaa kwake hadi saa 10:00 jioni, baada ya hapo tukaenda Magomeni tutakaa hadi saa 4:00 usiku kisha tukatoka tukaenda mitaa ya Mango Garden Kinondoni, kuna baadhi ya jamaa tulienda kuonana nao tukakaa hadi saa 6:00 usiku, baada ya hapo tukaenda kwangu, tukala ugali maharage na kuku.

“Baada ya kumaliza kula akapitiwa na usingizi ghafla, nilivyoona hivyo nikawaambia watu tuliokuwa nao, kila mmoja anaweza kwenda jamaa amelala na pombe nikahisi amelewa, huwezi kuamini aliamka ghafla akawarudisha watu wote tukaanza safari ya kwenda Maisha Club disco.

“Tukafika huko akaanza kutunza pesa zote alizokuwa nazo na kila aliyempa alikuwa anamwambia utanikumbuka, baada ya muda akanifuata tukaenda sehemu isiyokuwa na kelele tukaanza kuongea, ila yeye alinitaka mimi niondoke nikalale na akaniuliza ni saa ngapi, ilikuwa saa 8:25 usiku, akasema bia hataki tena saa zake za kunywa zimeisha, akaendelea kunifosi niondoke, nikakataa ikabidi tuondoke wote, ilipofika saa tisa kasoro tukaenda hadi Kinondoni nyumbani.”

Anasema Mafisango na baadhi ya watu aliokuwa nao wakaondoka kwenda Keko kabla hajaingia ndani akashangaa anamuona mmoja wao karudi na bodaboda kalowa damu, akamuuliza kimetokea nini akajibiwa papa kapata ajali.

“Basi nikatoka naye kuwahi eneo la tukio tukawatoa wote kwenye gari na tukaita taxi kuwawahisha Muhimbili, bahati mbaya alikuwa amepoteza damu nyingi, manesi wakaja kuniambia jamaa amefariki dunia, nikapoteza fahamu, niliamka saa mbili usiku nikajikuta nipo nyumbani, nikauliza papa yupo wapi nikaambiwa hayupo duniani nikazima tena.

“Baada ya kuamka alfajiri nikaenda msibani, haikuwa rahisi kwangu kukaa sawa, Mafisango nilikuwa nikimtambulisha kwa ndugu zangu wanakuwa ndugu zake, alizingatia zaidi furaha ya maisha yake kuliko maudhi, kauli yake ilikuwa Mungu amekupa uhai ili ufurahie, mtu wa vaibu muda wote, kila ifikapo kumbukumbu yake nafanya Dua ya kuwaombea waliotangulia akiwemo Mafisango.” alimazia kwa kusema ‘I just miss him’ siwezi kumsahau na naamini wote ni wa Mola na kwake tutarejea.

SOMA NA HII  TIMU ZA SAUZI ZAENDELEA KUIBOMOA YANGA....KOCHA MWINGINE HUYU HAPA NAYE ANASEPA...