Home Burudani MAMBO YAZIDI KWENDA KOMBO KWA MWAKINYO…AZIDI KUPOROMOKA KWENYE VIWANGO VYA DUNIA…

MAMBO YAZIDI KWENDA KOMBO KWA MWAKINYO…AZIDI KUPOROMOKA KWENYE VIWANGO VYA DUNIA…

Hassan Mwakinyo

Bondia Hassan Mwakinyo amezidi kuporomoka kwenye viwango vya ngumi Afrika na Duniani, licha ya hivi karibuni kumchapa Bondia kutoka DR Congo Kuvesa Katembo.

Kwa mujibu wa Mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec), Mwakinyo ameporomoka hadi nafasi ya 59 duniani na wanne Afrika kwenye uzani wa Super Welter.

Hapa nchini ameendelea kusalia namba moja kwenye uzani huo na wa tatu kwenye kila uzani (Pound for Pound) akiwa na nyota mbili na nusu.

Itakumbukwa, Mwakinyo aliwahi kuwa namba moja nchini na Afrika na kuwa kwenye 20 bora ya dunia kwenye uzani wake mwaka 2018 alipomchapa Sam Eggington na kuwa nembo ya Tanzania kwenye ngumi kimataifa wakati huu kabla ya kuporomoka.

Tangu wakati huo amekuwa na panda shuka, hadi juma lililopita Boxrec ilipoonyesha ameporomoka kwa mara nyingine, zikiwa yakipita majuma mawili tangu azichape na Katembo Aprili 23, mjini Dodoma.

Hata hivyo, matokeo ya pambano hilo bado hayajaingizwa kwenye rekodi na kwa mujibu wa Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), Chaurembo Palasa kama yataingizwa, huenda bondia huyo akaporomoka zaidi.

“Kushuka na kupanda inategemea na mabondia wa uzani wako huko duniani wanavyopigana na matokeo yao, hata hivyo, matokeo ya Mwakinyo na Katembo tumeshatuma Boxrec, kinachosubiriwa ni invoice, walipie ili yaingizwe.”

“Ingawa kuna mawili, ukicheza na bondia mwenye kiwango cha juu, hata akikupiga hauporomoki, hivyo Mwakinyo alicheza na Katembo ambaye alikuwa na nyota moja, matokeo yao yakiingizwa Boxrec kuna uwezekano mkubwa wa Mwakinyo kuporomoka zaidi,” amesema Palasa

Promota wa ngumi, Ally Mwazoa amesema licha ya Mwakinyo kuporomoka, bado ni nembo ya Tanzania kwa sasa kwenye ngumi, inahitajika kazi ya ziada ili arudi kwenye ubora wake.

SOMA NA HII  SIMBA YAIBIGA MKWARA WA KIBABE WYDAD