Home Habari za michezo WAKATI KAKOLANYA AKIWAACHA KWENYE MATAA…SIMBA WAINGIA CHIMBO NA KUMLETA HUYU…

WAKATI KAKOLANYA AKIWAACHA KWENYE MATAA…SIMBA WAINGIA CHIMBO NA KUMLETA HUYU…

Tetesi za usajili Simba

Mlinda Lango wa Geita Gold FC, Arakaza Mc Arthur, anatajwa kuwindwa na Simba SC ambayo inajipanga kuongeza nguvu katika safu hiyo baada ya mlinda mlango wake namba mbili, Beno Kakolanya, kusajiliwa na Singida Big Stars ya mkoani, Singida.

Kakolanya ameshasaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Singida Big Stars, hivyo Wekundu wa Msimbazi inasaka Mlinda Lango atakayesaidiana na Aishi Manula.

Taarifa za zilizopatikana jijini Dar es salaam zinaeleza kuwa Simba SC imeanza mchakato wa kuzungumza na Arakaza ambaye ni raia wa Burundi kwa ajili ya kujiunga na klabu hiyo ya Dar es salaam.

“Sasa hivi tunahitaji kufanya usajili mkubwa na kuangalia kipa ambaye atakuja kuchukuwa nafasi ya Kakolanya na kuleta ushindani na kipa namba moja (Manula),” kimeeleza chanzo cha habari kutoka jijini Dar.

Kwa upande wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, amesema suala la usajili kuelekea msimu ujao limeongezewa mikakati kwa sababu wanataka kunasa wachezaji wenye viwango vizuri na kwa kufuata mapendekezo ya benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Roberto Oliviera ‘Robertinho’.

Ahmed amesema ni mapema kuzungumzia ni mchezaji yupi wanazungumza naye kwa sababu viongozi kwa kushirikiana na kamati ya usajili wanaendelea kufanyia kazi tathmini ya awali ili kufikia malengo ya klabu.

“Kuhusu suala usajili tayari tumeanza mikakati, tunaelewa tumekosea wapi na kitu gani tunapaswa kufanya ili tuwe bora msimu ujao, ni jambo jema kutambua kila hatua ya usajili wa wachezaji ambao tumelenga kuwasajili kupitia viongozi na ripoti itakavyoonyesha mahitaji yetu,” amesema Ahmed.

Naye Mlinda Lango Arakaza, amesema taarifa hizo naye anaziona na kuzisikia mitandaoni kwa sababu hajafuatwa na kiongozi yoyote na bado ana mkataba Geita Gold FC.

“Hakuna mchezaji ambaye hatamani kucheza timu kubwa, nitakuwa tayari kama watakuja na ofa nzuri lakini kwa sasa nawapa kipaumbele Geita Gold FC ambao wameonyesha nia ya kuniongezea mkataba mwingine,” amesema Arakaza.

SOMA NA HII  SEKESEKE LA MORISSON KUDAIWA KUGOMBANA NA KOCHA LAZUA JAMBO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here