Home Habari za michezo SAKHO AFUNGUA HAYA KUHUSU KUCHEZA SIMBA HADI KUTIMKA KWAKE

SAKHO AFUNGUA HAYA KUHUSU KUCHEZA SIMBA HADI KUTIMKA KWAKE

Habari za Simba

MSENEGAL Pape Ousmane Sakho ambaye amejiunga na US Quevilly-Rouen ya Ligi Daraja la Kwanza Ufaransa ‘Ligue 2’, ameeleza kuichezea Simba ni kati ya maamuzi bora kufanya katika uchezaji wake wa soka la kulipwa akiwa Afrika.

Winga huyo, alisema kuichezea Simba kumefungulia milango mingi kwake ikiwemo kuwa sehemu ya kikosi cha timu yake ya taifa na kupata shavu la kukipiga Ulaya.

“Nilikuwa na wakati mzuri nikiwa na Simba, nilipata nafasi ya kuonyesha kipaji changu kwenye mashindano ya kimataifa, niliishi vizuri na wachezaji wenzangu ndani na nje ya uwanja kiasi cha kujihisi ni kama nilikuwa nyumbani,” alisema na kuongeza;

“Simba itaendelea kuwa kwenye moyo wangu, ilikuwa ni bahati iliyoje kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa (Senegal), nilikutana na Kaka zangu ambao wanacheza soka Ulaya, kiukweli shauku yangu ilichochea kwa sababu ni ndoto yangu kupiga hatua nashukuru Mungu wakati sahihi umefika.”

Wakati akiwa Simba, Sakho alitwaa tuzo ya goli bora la mwaka Afrika ambalo alifunga dhidi ya Asec Mimosas katika Kombe la Shirikisho Afrika, Februari 13 2022 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kupitia tuzo hiyo ndipo ulipokuwa mwanzo wake wa kuwa na mawasiliano na Sadio Mane ambaye alikutana naye Rabat, Morocco kwenye sherehe hizo na kwa mujibu wa taarifa kutoka Ufaransa nyota huyo wa Bayern Munich ndiye aliyefanikisha uhamisho huo.

Sakho ambaye atakumbukwa kwa staili yake ya ushangiliaji ya kunyunyiza ameitakia kila la kheri Simba kwenye maandalizi yao ya msimu ujao huku akiamini wanaweza kurejesha heshima yao.

“Msimu uliopita haukuwa mzuri lakini naamini kuwa timu itarudi na nguvu mpya msimu ujao na kufanya vizuri, kwakherini,” alisema.

SOMA NA HII  KWA TAKWIMU HIZI STRAIKA MPYA SIMBA...ANA KAZI YA KUFANYA...GEFLEA AMCHAMBUA